MAKONDE: Maywether kiboko, ana walinzi mabaunsa 30

Mayweather (mwenye jaketi la bluu na njano) na mabaunsa wake.

Muktasari:

  • Awali nilistuka na kuhoji hao ni kina nani, jirani yangu akanijibu ni Maywether huyo anaingia na hao unaowaona ni walinzi wake …walikuwa 30 niliwahesabu haraka haraka. Ni mabaunsa aisee, wameshiba!

Mkutano wa wadau wa ngumi za kulipwa duniani ulifanyika Desemba 11 hadi 17, Miami, Florida nchini Marekani.

Zaidi ya wadau 500 walihudhuria mkutano huo uliofanyika kwenye Hoteli ya Diplomat and Star, Florida.

Katika mkutano huo, Tanzania iliwakilishwa na Juma Ndambile, ambaye ni promota wa ngumi za kulipwa na meneja wa bondia, Francis Cheka.

Spoti Mikiki ilifanya mahojiano na Ndambile aliyehudhuria mkutano huo kuelezea kilichojiri.

Swali: Unaweza kutueleza mkutano ulikuwa na madhumuni gani hasa?

Ndambile: Kikubwa ilikuwa kujadili maendeleo ya ngumi duniani na upande wa Afrika, pia ilikuwa mjadala nini mipango ya bara hilo katika ndondi.

Kuna hili Baraza la Ngumi Duniani, WBC, wanashirikiana na African Boxing Union (ABU), hivyo katika kongamano lile sisi wajumbe kutoka nchi za Afrika tuliiwakilisha ABU.

Swali: Kazi kubwa za ABU ni zipi?

Ndambile: ABU ni African Boxing Union, kazi yake ni kusimamia masuala ya ngumi za kulipwa Afrika …sasa sisi tulifanya mkutano wetu kama ABU na kuweka maazimio yetu kuachilia mbali lile kongamano la WBC ambalo lilihusisha wajumbe wa dunia kote.

Kati ya mambo hayo ni kuinua mchezo wa ngumi za kulipwa Afrika, mkakati wa ushirikiano na mabaraza, mashirikisho na vyama vya ngumi kimataifa pamoja na ushirikishwaji katika kuwania mikanda ya WBC na mataji mbalimbali.

Swali: Tukio gani kubwa lilitokea katika mkutano ule?

Ndambile: Miongoni mwa tukio kubwa nililoliona, lilikuwa ni kumuenzi bingwa wa zamani wa dunia wa uzani wa juu, Muhammad Ali aliyefariki dunia mwaka jana kwa ugonjwa wa kutetemeka.

“Ililetwa sanamu ya Muhammad Ali katika kongamano lile na baadhi ya mabondia, akiwamo Klitschko, Lennox Lewis, Evender Hollyfield na wengine wengi walipewa fursa ya kumzungumzia na kutaka aenziwe kwa hamasa na mchango wake katika ngumi, vilevile mwanae, Leila Ali alimzungumzia baba yake.

Swali: Leila alimzungumzia nini baba yake?

Ndambile: Alimzungumzia kipaji chake na namna alivyoitangaza Marekani kupitia ngumi duniani kote na jinsi ambavyo alivyoenziwa na hadi uzee alienziwa na hata anafariki, bado alikuwa anaheshimika.

Swali: Kwa kuwa ni mkutano wa wadau wa ngumi, naamini ulikutana na watu mashuhuri, nani ulikutana naye mkafanya mazungumzo kwa maendeleo ya ngumi Tanzania?

Ndambile: Nilikutana na wengi, lakini kati yao ni bondia Floyd Maywether …nilipambana hadi kufanikiwa kuzungumza na Maywether kama dakika 10 hivi.

Unajua ilikuwa Desemba  11 kwenye kongamano tukiwa hoteli ya Diplomat and Star, ghafla tukaona kundi kubwa la watu linakuja eneo ambalo kongamano linafanyika.

Awali nilistuka na kuhoji hao ni kina nani, jirani yangu akanijibu ni Maywether huyo anaingia na hao unaowaona ni walinzi wake …walikuwa 30 niliwahesabu haraka haraka. Ni mabaunsa aisee, wameshiba!

Ulinzi ule sijapata kuona, mabaunsa wanamlinda bondia huyo kwa  staili ya kumzunguka na yeye Maywether kuwa katikati.

Akiwa anatembea, huwezi kumuona Maywether, haonekani kabisa, anakuwa amezungukwa na walinzi wake, uwepo wake kwenye lile ngongamano lilinianifanye nipange mikakati ya kumfuata na kuzungumza naye mawili matatu juu ya ngumi za kulipwa.

Swali: Ulifanikiwa kumpata?

Ndambile: Nilitumia juhudi binafsi bila kumshirikisha mtu yoyote maarufu kwenye kongamano lile, lakini nilikwama kutokana na walinzi.

Unajua hata Wamarekani wenyewe wanapata kazi kumuona Maywether, kiukweli ndiye mshiriki pekee wa kongamano lile aliyekuwa na walinzi wengi, hivyo nikawa nimeshindwa kuonana naye kwa kutumia juhudi zangu binafsi.

Swali: Baada ya hapo ulifanya nini sasa?

Ndambile: Sikukata tamaa, niliamua nipitie upande wa pili ili kufanikisha dhamira yangu ya kuzungumza na Maywether, nilimfuata Rais wa WBC nikamuomba anisaidie kunikutanisha na Maywether, alikubali tukaongozana hadi alipokuwa Maywether.

Rais wa WBC alinitambulisha kwa Maywether kwamba mimi ni promota kutoka Tanzania, tulisalimiana na pale ndipo nikapata nafasi ya kuzungumza naye masuala ya ngumi na kumpongeza kwa mafanikio yake.

Nilimkaribisha Tanzania, lakini kikubwa ni kufanya utalii hasa kupanda Mlima Kilimanjaro.

Swali:  Aliupokeaje mwaliko wako?

Ndambile: Aliposikia habari za Mlima Kilimanjaro alishtuka kidogo, akaniambia habari za Mlima huo anazisiki, huku akashangaa kwa kuhoji…kumbe Mlima huo huko Tanzania!

Tulizungumza mambo kadhaa juu ya Mlima Kilimanjaro na kunihoji mahali ulipo na namna anavyoweza kufika, alionekana kuvutiwa na kuja kupanda Mlima Kilimanjaro.

Pale pale nikaamua kutumia nafasi hiyo kumkaribisha nikiamini kabisa hicho ndicho kitu pekee ambacho kinaweza kumvutia Maywether kuja Tanzania, pia nikiamini ujio wake utakuwa moja ya nafasi ya kutangaza utalii wetu maana yule si mtu mdogo katika dunia hii ana nafasi yake kama mtu mashuhuri na tajiri.

Kimsingi naweza kusema Maywether  alikubali na kuahidi kufanya hivyo, tukabadilishana ‘contact’ (mawasiliano) akaniambia niwe ninamkumbusha.

Swali: Unasema ulitumia dakika 10 kuzungumza na Mayweather, mbali na Mlima Kilimanjaro, mambo gani mengine mliyazungumza?

Ndambile: Tulikuwa ‘tunapiga stori’ za hapa na pale, mambo mbalimbali na akanipa kofia yenye chata yake yake ya TMT ikimaanisha The Money Team.

Unajua baada ya kumwambia kuhusu Mlima Kilimanjaro, alivutika sana halafu yule jamaa ni tajiri, kwa uhalisia anahitaji ushawishi ili kuja Tanzania, mimi kama Juma Ndambile siwezi kwa asilimia 100, nimefanya ushawishi kwa eneo nililolimudu ameonyesha nia lakini sasa Serikali lazima ihusike katika hili na hasa watu wa Tanapa.

Kwa kuwa amekubali kuja Tanzania na juzi juzi tu hapa alijibu email yangu niliyomwandikia kupitia  Maywether Promotions, kilichobaki ni sisi kujipanga katika hili, sana sana ni Serikali kulibeba hili ili kufanikisha ujio wake.

Swali: Ulizungumzia Mlima Kilimanjaro kwa Mayweather pekee kwanini isiwe kwa wengine pia?

Ndambile: Huyu nilipata muda mzuri wa kuzungumza naye mambo mengi, nilitumia nafasi nikamchomekea hili la kuja, naye kakubali. Halafu huyu jamaa ni bilionea nikaona nimng’ang’anie, na wengine niliongea nao lakini si kama nilivyofanya kwa Mayweather.

Ninaamini ujio wake Tanzania, kwanza utasaidia kutangaza vivutio vyetu vya utalii duniani, maadamu nimekamilisha kupata mawasiliano naye na kujaribu kumshawishi aje, ujio wake sasa unabaki kuwa mikononi mwa Serikali. Nitawaambia wahusika suala hili watu wa Tanapa na Waziri wa Michezo, Nape Nnauye nitamtafuta ili kuona tunafanyaje kumleta bondia huyu Tanzania.

Swali: Akina nani wengine uliopata kuzungumza nao?

Ndambile: Nilizungumza na bingwa wa dunia wa uzani wa juu, Wladimir Klitschko, promota wa kimataifa wa ngumi, Don King na bondia na bingwa wa zamani wa uzani wa juu, Evender Holyfield.

Swali: Kubwa ni lipi hasa mlilokuwa mnazungumza na watu hao?

Ndambile: Tulizungumza mambo mengi, na hawa walikuwa na nia ya kuja Tanzania na zaidi hiyo ya kupanda Mlima Kilimanjaro.

Evender alisema yuko tayari kuja wakati wowote mipango ikikamilika, pia Don King na Klitschko ambao nao wameonyesha nia ya kuja baada ya kuwashawishi kuja kupanda Mlima Kilimanjaro.

Swali: Hao wengine akina Holyfield, Don King ulinzi wao ukoje na wao walikuwa na mabaunsa 30?

Ndambile: Tofauti na Maywether, Evender, Klitschko na Don King ulinzi wao haukuwa mkubwa, kila mmoja analindwa na mlinzi mmoja mmoja, hivyo nilipata fursa ya kuzungumza nao muda mrefu zaidi.

Ukweli nilikuwa kama wakala wa utalii, nilifanya kazi ya kuwatia chumvi na kila mmoja ameonyesha nia ya kutembelea Tanzania, lakini kama nilivyosema awali, kuwaleta kama Juma siwezi, lazima Serikali ichukue nafasi kwa asilimia 100 kwani ujio wa watu hawa ni wa kitaifa.

Swali: Tuachane na hayo, vipi uwakilishi wa Tanzania kwenye mkutano huo?

Ndambile: Uwakilishi wetu ulikuwa mzuri, nilifurahi kusikia mabondia watano wa Tanzania wamegeuka gumzo kwenye kongamano kwa kutambulika. Mabondia; Twaha Kiduku, Cosmas Cheka, Julius Kisarawe, Ibrahim Class na Meshack Mwankemwa walitajwa kuwa wanapewa nafasi ya kuwania mikanda ya ABU na kisha kuwania taji kubwa la ngumi duniani la WBC.

ABU na WBC wamekuwa wakishirikiana hivyo hiyo ni nafasi ya mabondia hao kutumia fursa iliyotolewa na ABU.

Vilevile, kongamano hilo lilipitisha mchakato wa WBC Amateur Professional na mabondia wa timu ya taifa ama wa ridhaa watakuwa na nafasi ya kuwania taji la WBC hata kama hawapigani katika ngumi za kulipwa.

Swali: Hebu tuambie, Juma Ndambile ni nani hasa?

Ndambile: Kabla ya kuwa promota, niliwahi kucheza mapambano kadhaa huku pambano langu la mwisho nilipigana 2005 na Jafar Majia nikapoteza kwa pointi na ndipo nilipoamua kuelekeza nguvu zangu kwenye upromota.

Swali: Tangu uwe promota, umekwishaandaa mapambano mangapi?

Ndambile: Nimeandaa mapambano kadhaa makubwa ikiwamo la ubingwa baina ya Francis Cheka na Ajetovic, lakini lengo ni kuandaa pambano kubwa la kimataifa ambalo maandalizi yameanza na litakuwa pambano kubwa kushinda mapambano yote.

Swali: Nimesikia wewe ni meneja wa Francis Cheka, ina ukweli hii?

Ndambile: Ni kweli, lakini si kwa Cheka tu, mimi pia ni meneja wa mabondia; Cosmas  Cheka, Twaha Kiduku, Mohamed Matumla, Lulu Kayage na  Julius Kisarawe na tayari nimefungua kampuni nchini Marekani kwa ajili ya kusimamia masuala mbalimbali ya michezo. Kampuni yangu inaitwa Tanganyika Industry Ink ambayo mimi ni makamu wa rais na rais ni raia mmoja wa Marekanm, lengo ni kushirikiana kufanya mapambano makubwa ya ngumi na hata kuibua vipaji vya riadha.

Swali: Umejifunza nini kwenye kongamano la Marekani?

Ndambile: Nimejifunza mengi, lakini kongamano lile limedhihirisha Tanzania bado ina safari ndefu ili kufikia mafanikio ya ngumi, siyo kama Maywether ana muujiza au kazaliwa na fedha, la hasha ni kipaji tu, nilitamani siku moja kumuona bondia wa Tanzania analindwa vile.

Kiukweli hata robo hatuingii. Ngumi za Tanzania zinahitaji mabadiliko makubwa, si za kulipwa hata ridhaa, zinahitaji usimamizi wa uhakika, japo tuone mabondia wetu wanakuwa sio wa mchezo mchezo. Inatakiwa mabondia waheshimike, ndicho ninakifikiria kwa sasa, kurejesha hadhi ya ngumi japo hatutofikia hatua ya wenzetu lakini mchezo uwe na hadhi.

Swali: Mbona unaonekana kama mazingira ya wenzetu yamekushtua?

Ndambile: Ukweli kuna kazi kubwa. Hivi vyama vya ngumi visione kama vimemaliza kusimamia ngumi kuwa sasa ijiendeshe, bado kazi ni kubwa.

Wenzetu wako vizuri, yaani ukizungumzia ngumi kwa wenzetu unazungumzia mchezo mkubwa sana, nitajitahidi kutumia kile nilichokipata kuboresha kwa kiasi fani kwa manufaa ya nchi na mabondia wetu.

Vyama vya ngumi, TPBC, PST, TPBO na vingine, vina kazi. Uongozi si maneno, ngumi za Tanzania bado sana.