MAONI: Upepo wa madiwani kujiuzulu utaishia wapi

Wimbi la madiwani wa Chadema kuachia ngazi limeanza kuchukua taswira ya kitaifa na kuongeza mjadala baada ya mawimbi yake kwenda kila kona.

Wengi wa wanaojiuzulu wanatoa sababu zilezile na hali hiyo huenda ikaendelea kwa miaka mingi.

Tayari madiwani zaidi ya kumi wameachia ngazi katika majimbo ya Arumeru, Arusha Mjini, Monduli, Hai na Iringa.

Wengi wao walisema wanaridhika na utendaji wa Serikali ya awamu ya tano na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na uamuzi wao ni sehemu ya kumuunga mkono Rais John Magufuli.

Wanajipambanua kuwa si aina ya wanasiasa wanaopinga kila kitu kwa kuwa walichokitafuta tayari kinafanyika na hawana sababu ya kuhoji wala kukosoa.

Wapo waliopokea shutuma kwamba busara yao ilirutubishwa na vitita vya fedha kutoka kwa makada wa CCM ili kuwashawishi kufikia uamuzi huo.

Hata hivyo, kuna wabunge wa upinzani wanaounga mkono baadhi ya hatua za Serikali katika udhibiti wa rasilimali za umma na kuweka nidhamu ya matumizi ya fedha za wananchi, lakini hawajalazimika kujivua uongozi na wameendelea kuwa upinzani.

Mtikisiko wa hivi karibuni uliotokea katika Jimbo la Iringa Mjini baada ya madiwani watatu wa chama hicho kujiuzulu ni sawa na kengele ya tahadhari kwa chama hicho inayoashiria matukio mengine ya kushtua katika maeneo mengine.

Wao walikuja na sababu tofauti kidogo, kwamba wamechoshwa na uongozi wa kidikteta ndani ya chama hicho na hivyo kufikia uamuzi wa kuachia ngazi.

Pamoja na kuwa hawakutangaza kuhamia chama kingine, bado uwepo wao kwenye chama utaendelea kutiliwa shaka. Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) anasema hatua hiyo si tishio kwa chama na kuwa watakaoendelea kukiuka maadili wataendelea kuchukuliwa hatua.

Madiwani wengi wanaotangaza kujivua nafasi ya udiwani kutoka Chadema hawako tayari kutaja hatua inayofuata ambayo mara nyingi ni kuhama chama.

Pia, inawezekana bado wanatafakari usalama wao kisiasa kama ni busara kubaki kwenye vyama vya upinzani au kurejea CCM na kutazamwa na wenzao kama ng’ombe waliokatika mikia.

Wakati huu ambao CCM inajaribu kujiumba upya kwa kutumia kauli ya kurudisha chama kwa wanachama ni vigumu majeruhi wa kisiasa aliyepokelewa kutoka upande wa pili kupata jukwaa la kupaza sauti.

Kwa utaratibu mpya wa CCM lazima mgeni afundishwe misingi ya chama ili arudi kwenye mstari na kuaminika.

Kwa mfano, aliyekuwa diwani wa muda mrefu wa Kata ya Muleba Mjini(CUF), Hassan Milanga aliona usalama wake ni kuhamia CCM baada ya kushindwa kutetea nafasi yake katika uchaguzi uliopita.

Ni diwani wa kwanza kupitia (CUF) Mkoa wa Kagera. Alidumu kwa zaidi ya miaka 20. Kwa miaka yote alilindwa na wana CCM hadi kwenye sanduku la kura wakilipiza kisasi cha jina lake kuenguliwa.

Kushindwa kwake pia ulikuwa mwanzo wa kuandikwa kwa historia mpya kwa chama cha (NLD) kupata ushindi kupitia kwa Edward Mwinamira. Anatajwa kuwa diwani pekee wa chama hicho nchini.

Aliyekuwa mgombea wa Ubunge Jimbo la Kyerwa kupitia Chadema, Benedicto Mutungirehi tayari naye amerejea CCM akifuata nyayo za aliyekuwa mgombea wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali.

Baada ya Mikoa ya Kaskazini na Kusini kutikiswa na wimbi la madiwani wa Chadema kujivua nafasi zao usalama Kanda ya Ziwa unabaki kwenye shaka.

Inawezekana tayari viongozi wamepima uzito wa mawimbi hayo na kuweka miundombinu. Hofu ya walioko nyuma yao inaongezeka na wanajiuliza wataponaje?

Uhai wa ngome ya Kanda Ziwa umesimama katika Manispaa ya Bukoba inayoongozwa na Chadema baada ya kuteka viti vingi vya madiwani mwaka 2015.

Kwa kuwa matukio ya madiwani kujivua nafasi zao yanatokea kwenye halmashauri na manispaa zinazoongozwa na Chadema, huwezi kupuuza uwezekano wa upepo kugeuka na kuelekea Bukoba.

Upepo hauwezi kumuacha salama mmoja wa madiwani aliyetajwa kumpigia kura mgombea umeya kupitia CCM aliyepata kura zaidi ikilinganishwa na idadi ya madiwani wa chama chake.

Pia, wapo madiwani ambao kwa miaka miwili wanajua ugumu wa kutetea nafasi zao, kwao hii inaweza kuwa sababu ya kutangaza kuiunga mkono Serikali kwa mema inayofanya.

Pamoja na yote hayo, gharama za madiwani kujivua nafasi zao zinabebwa na wananchi ambao jasho lao litatumika kufanya uchaguzi mdogo wa kupata madiwani wengine.

Mzigo huu wa kidemokrasia unaweza kuwa mkubwa zaidi kadri idadi siku zinavyokwenda.