MAONI YA MHARIRI: Mabalozi wa nyumba kumi ni muhimu

Muktasari:

Mfano ni mauaji ya raia, askari polisi na viongozi wa Serikali ambayo yamefanyika katika wilaya za Rufiji, Ikwiriri na Kibiti na kuua zaidi ya watu 30, huku wauaji wakiwa bado hawajafahamika.

Matukio ya uhalifu yamekuwa yakiongezeka kila kukicha. Kumekuwa na aina mbalimbali za uhalifu zinazoripotiwa kwenye vyombo vya habari na vituo vya polisi nchini.

Mfano ni mauaji ya raia, askari polisi na viongozi wa Serikali ambayo yamefanyika katika wilaya za Rufiji, Ikwiriri na Kibiti na kuua zaidi ya watu 30, huku wauaji wakiwa bado hawajafahamika.

Wakati mauaji hayo yakiteketeza maisha ya watu wasio na hatia, kumekuwa pia kukiripotiwa ujambazi katika maeneo mbalimbali nchini jambo ambalo linaonyesha kuwa kuna mahali kuna tatizo.

Inawezekana kuongezeka kwa idadi ya watu, teknolojia mpya, ugumu wa maisha na kukua kwa miji ikawa chanzo cha uhalifu huo, lakini tatizo kubwa ni pale tulipoacha misingi ya utamaduni wetu na kukubali kuacha mambo yaliyokuwa yanatuunganisha.

Wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere, tunakumbuka jinsi umoja na ushirikiano vilivyokuwa vinapewa kipaumbele kiasi kwamba watu wa kijiji kimoja au mji mmoja ilikuwa rahisi kufahamiana.

Mgeni yeyote ambaye angeingia mtaani alipaswa kutambulishwa ili afahamike kwa watu wengine na huo ulikuwa utaratibu uliotumika nchini kote.

Kiungo kikubwa cha umoja na ushirikiano huo, ilikuwa ni kupitia mabalozi wa nyumba kumi, ambao licha ya kazi nyingine walikuwa wanahakikisha watu wao wote wanafahamika.

Nyumba kumi hizo zilisaidia watu wote kufahamiana na hivyo kuwa rahisi kusaidiana wakati wa matatizo na pengine ndio maana hata uhalifu ulikuwepo kwa kiwango cha chini sana.

Lakini, soko huria na mabadiliko ya teknolojia na tawala yamefanya mambo mengi yabadilike na ndio maana suala la balozi wa nyumba kumi limekuwa si jambo la msingi tena, wamekuwa hawana nguvu kama ilivyokuwa zamani.

Siku hizi imekuwa kawaida watu kuishi katika mtaa moja, lakini bila kufahamiana, inaweza kuwa mjini au vijijini. Hilo ni tatizo ambalo wengine wanaweza kusema limesababishwa na mabadiliko ya utandawazi, lakini hatuwezi kuiacha hoja kuwa kufifishwa kwa mabalozi wa nyumba kumi kumechangia hilo.

Uhalifu na ujambazi unaotokea sehemu mbalimbali ni kutokana na watu wengi kutofahamiana hivyo kuwafanya wanaotenda maovu hayo kutofahamika kwa jamii. Ndio maana tumefurahishwa na kitendo cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutangaza kuwa kitafanya utafiti kuona jinsi mabalozi wa nyumba kumi wanavyoweza kusaidia kupunguza matukio ya uhalifu.

Akiunga mkono uamuzi huo, Jaji mstaafu Joseph Warioba amesema utafiti huo ni muhimu kwa sasa kutokana na kuenea kwa matukio ya uhalifu na uvunjifu wa amani nchini. Waziri Mkuu huyo wa zamani amesema ulinzi wa amani unatakiwa uanzie kwenye nyumba kumi na huo ni kiungo muhimu kati ya wananchi na Serikali. Na ameshauri kuwa ili hilo lifanikiwe vizuri, ni vyema likaondolewa katika mfumo wa vyama na kuhamishiwa ngazi ya Serikali.

Warioba amefafanua kuwa utafiti huo unaweza kuja na majibu yanayofikiriwa na wengi ikiwamo wanaoamini wajumbe wa nyumba kumi ni muhimu katika suala la ulinzi na usalama wa nchi.

Sisi tunaona jambo hili limechelewa na lilipaswa kuanza zamani, lakini ilimradi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeonyesha nia ya kufanya utafiti huo, sisi tunadhani hilo ni jambo jema na linapaswa kuungwa mkono.

Siri pekee ambayo Mwalimu Nyerere alitujengea ni mshikamano na umoja, lakini hatuwezi kuwa na hayo yote kama tutakubali kuvunja nguvu ya mabalozi wa nyumba kumi. Tunashauri utafiti huo ufanyike kwa haraka ili mapendekezo yake yatumike kukomesha uhalifu nchini.