UCHAMBUZI: Tujitahidi kupambana na ebola

Muktasari:

Ugonjwa huu unafahamika ulimwenguni kwa kuua watu wengi na kwa haraka kutokana na kirusi kinachosababisha ugonjwa huu kinachofahamika kama ebola (ebora virus).

Mlipuko wa ugonjwa wa ebola umekuwa ukiripotiwa miaka ya karibuni katika nchi ambazo Tanzania inapakana nazo, jambo ambalo limekuwa likizua hofu kwa wananchi.

Ugonjwa huu unafahamika ulimwenguni kwa kuua watu wengi na kwa haraka kutokana na kirusi kinachosababisha ugonjwa huu kinachofahamika kama ebola (ebora virus).

Katika takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za Januari 13, 2016 zilionyesha kuwa jumla ya watu 11,315 walikufa kutokana na ebola ambapo idadi hiyo ilijumlisha mtu aliyefia Marekani na watu sita nchini Mali.

Katika takwimu hizo watu 4,809 (Liberia), 3,955 (Sierra Leone), 2,356 (Guinea) na wanane (Nigeria) na idadi hiyo ilipatikana kwa kuthibitisha, kuhisi na makadirio.

Kwa takwimu hizi ni kiashiria jinsi ebola ilivyo hatari kwa mazingira na nchi itakayopata mlipuko ambao ueneaji wake huwa wa haraka kutokana na dalili zake.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha inapambana kuzuia mlipuko wa ugonjwa huu, kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari na kuzisambaza kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Pia, Serikali imehakikisha sehemu za mipakani na vituo ambavyo wageni wanaingia kutoka nchi mbalimbali vinakuwa na wataalamu wa afya, mfano katika Uwanja wa Ndege wa Songwe.

Jitihada hizi za Serikali ziimarishwe kuliepusha Taifa na maambukizi ya ugonjwa huo, unaoweza kuathiri sekta ya utalii. Lakini, pamoja na jitihada hizo bado kuna haja ya kuimarisha ulinzi maeneo ya mkipakani kutokana na wingi wa watu na magari ya mizigo na abiria.

Tanzania tumekuwa tukifanya biashara na nchi jirani kutokana na uwepo wa bandari ambayo imekuwa inapokea meli kubwa kutoka mataifa makubwa.

Bidhaa husafirishwa nchi mbalimbali kupitia malori, magari madogo ambayo madereva wake hukutana na watu tofauti kwenye nchi wanazosafiri.

Uangalizi unatakiwa kuwapo sehemu za mipakani kuhakikisha hakuna mtu atakayeingia nchini na maambukizi yoyote ya ugonjwa huu hatari.

WHO inasema huchukua siku mbili hadi wiki tatu kugundulika kama mtu ameshaambukizwa ebola. Ni lazima kuhakikisha hakuna mtu atakayeweza kurudi na virusi.

Dalili za mwanzo huwa ni uchovu na homa, kupata maumivu ya tumbo, koo, misuli, kichwa na mgonjwa hupatwa na kichefuchefu na kumsababishia kutapika, kuharisha vitakavyoambatana na utokaji wa damu mwilini.

Ulinzi wa ugonjwa huu si kwa Serikali pekee bali mapambano yawe kwa kila mmoja kutokana na kupata uelewa wa dalili za awali.

Katika mipaka yetu sehemu nyingi kumekuwa na njia ‘bubu’ au maarufu njia za ‘panya’ ambazo baadhi ya watu hufanya biashara haramu.

Serikali kwa kutumia vyombo vya dola imekuwa ikipambana na sehemu hizi hatarishi ambazo kwa namna moja zinaweza kutuletea virusi hivi.

Hivi karibuni nchini Congo kulikuwapo taarifa za kugundulika wagonjwa wa ebola. Tanzania kupitia Wizara ya Afya ilitangaza kutojihusisha kibiashara na eneo hilo ambalo lilipata mlipuko.

Suala la kuzingatia ni kuwa ugonjwa huu husambaa na Congo ni moja ya nchi ambayo tumekuwa na uhusiano wa kibishara kwa muda mrefu, lakini kuna haja ya kuwa makini.

Ni muhimu kwa Wizara ya Afya kuzingatia zile sehemu muhimu ambazo zinaweza kutuletea virusi vya ebola, hususan kuzuia njia za panya.