MAONI YA MHARIRI: Wananchi ardhi ni mali msiuze kiholela

Muktasari:

Ukiondoa wanaouza kiholela, wapo wananchi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini waliofikia hatua ya kutoa ardhi zao bure, bila kujali thamani yake kwa maisha yao ya sasa na hata kwa vizazi vya baadaye.

Kasi ya wananchi kuuza ardhi ovyo, inazidi kuwa kubwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Ukiondoa wanaouza kiholela, wapo wananchi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini waliofikia hatua ya kutoa ardhi zao bure, bila kujali thamani yake kwa maisha yao ya sasa na hata kwa vizazi vya baadaye.

Tamaa, kutojali na ukosefu wa elimu kuhusu thamani ya ardhi, ni baadhi ya vitu vinavyowasukumua watu wengi kuuza ardhi zao kinyemela.

Kinachosikitisha zaidi ni kuwa wapo baadhi ya wananchi wanaouza ardhi yote na kisha kubakiwa na eneo dogo lisilotosha hata kwa matumizi ya familia.

Uzoefu wetu unaonyesha kuwa wananchi wengi wamekuwa wakirubuniwa na watu wenye fedha na mwishowe kuuza ardhi zao kwa kiasi kisicholingana na thamani halisi ya maeneo husika

Uuzaji ovyo wa ardhi sio tu umekuwa ukisababisha migogoro ya kifamilia, lakini wauzaji hujikuta wakiwa hawana chochote muda mfupi baadaye na hivyo kulazimika kuvamia maeneo ya watu wengine.

Tukiamini kuwa ardhi ni mali na urithi wenye thamani kubwa, tunalazimika kuwatanabahisha Watanzania kuwa makini kabla ya kuamua kuuza maeneo wanayomiliki.

Hata katika mazingira ambayo mwananchi analazimika kuuza ardhi yake, ahakikishe anabaki na sehemu kwa ajili ya makazi ya familia na kwa kufanyia shughuli za kiuchumi kama kilimo na ufugaji.

Njia nyingine tunayowashauri wale wanaoona haja ya kuuza ardhi zao, ni kuingia mikataba ya matumizi ya ardhi na watu wanaojitokeza kwa ajili ya uwekezaji badala ya kuwauzia moja kwa moja tena kwa bei ya chee.

Kwa upande mwingine, vyombo husika serikalini na kwenye sekta binafsi, havina budi kutoa elimu kwa umma kuhusu ulinzi wa ardhi. Lakini pia vijihimu sasa kuanzisha mipango ya kuwawezesha wananchi kuyapima na kutathmini maeneo yao, kwa kuwa huo ndiyo urithi na mtaji pekee wa maendeleo kwa wananchi wengi.

Upimaji wa ardhi na hatimaye kutoa hati miliki utasaidia na kuwaepeusha wananchi na kadhia nyingi, ikiwamo tabia ya muda mrefu ya baadhi ya watendaji hasa vijijini kuwanyanganya ardhi wananchi kwa kisingizio cha kuwapa wawekezaji.

Tunatambua kuwa Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba tano ya mwaka 1999, inavipa vijiji mamlaka ya kutoa ardhi isiyozidi ekari 50 kwa ajili ya uwekezaji, lakini katika maeneo mengi hili halifanyiki kwa masilahi ya walio wengi.

Ni heri uwekezaji huo ungekuwa unafanyika na hatimaye kuinufaisha jamii, lakini katika baadhi ya maeneo, idadi kubwa ya wanaoitwa ‘wawekezaji’, wamekuwa wakitumia ardhi hizo kama tiketi ya kuombea mikopo. Wakifanikiwa wanatelekeza maeneo hayo na kuyaacha yakiwa mapori yasiyoendelezwa.

Ili tuendelee kama alivyowahi kusema Rais wa Awamu ya Kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, pamoja na mambo mengine tunahitaji ardhi kama rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Kama tulivyosema hapo mwanzoni, ardhi ni mali, urithi na mtaji wa maendeleo.

Kwa kupitia ardhi inayomilikiwa kihalali na yenye hati, mwananchi kwa mfano, anaweza kwenda katika taasisi za kifedha akakopa kwa ajili ya ustawi wake binafsi na maendeleo ya nchi yake.