TFS Shinyanga yaja na utalii wa ikolojia kuongeza mapato
Muktasari:
- Utalii huo utafanyika katika maeneo ya asili kwa lengo la kufurahia na kujifunza kuhusu mazingira na viumbe hai huku ukichangia uhifadhi wa mazingira na kuwanufaisha wananchi wa eneo husika, kukiwa na gharama ya Sh1,500 kwa walio na miaka 15 na kuendelea na bure kwa walio chini ya hapo.
Shinyanga. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Shinyanga ameanzisha utalii wa ikolojia katika msitu wa Lubaga, utakaosaidia kutunza mazingira na uhifadhi wa viumbe hai na kuongeza mapato katika kitengo cha misitu mkoani Shinyanga.
Hayo yameeleza leo Juni 27, 2026 na Mwakilishi wa Kamanda wa Hifadhi ya Misitu Kanda, Aloyce Kileng’wa katika hafla ya uzinduzi wa utalii ikolojia uliofanyika katika msitu wa Lubaga uliopo Manispaa ya Shinyanga, ikioongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita.
“Wazo hili limetekelezwa kwa lengo la kukuza mapato katika sekta yetu kwa kutengeneza vivutio katika baadhi ya maeneo ya msitu huu, ambapo wananchi wa Shinyanga na wageni watanufaika na huduma hii,” amesema Kileng’wa.
Naye, Kamanda wa Wakala wa Hifadhi ya Misitu Mkoa wa Shinyanga, Fabian Balele ameeleza kuwa katika kutekeleza wazo la utalii ikolojia wamehakikisha hakuna miti iliyoharibiwa kwani lengo ni kutunza na kuhifadhi mazingira.
“Katika utekelezaji wa utalii ikolojia tumehakikisha miti haijaharibiwa katika msitu huu, tumeangalia maeneo yenye nyasi ndio ambayo tumeweka vivutio hivyo na bado tunaendelea na utalii ikolojia tunatarajia kuleta wanyama,” amesema Balele.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Frola Kajumula ameeleza kuwa utalii ikolojia unasaidia kama tiba kwa watu wenye matatizo ya afya ya akili kwa sababu katika utalii huo kupunguza msongo wa mawazo. Ameipongeza TFS kwa kupiga hatua hiyo na kukuza uchumi.
Kwa upande wake, mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Nkinda, amesema rasilimali zilizopo zinaweza kubadilishwa kuwa fursa katika kukuza uchumi wa nchi na kuweka mazingira ya kuimarisha afya ya akili.
“Nitoe wito kwa shule, vyuo taasisi za kiserikali na binafsi kutumia eneo hili kufanya utalii wa ndani na kama sehemu ya wanafunzi kuja kujifunzia kutunza na kuhifadhi mazingira, kukuza uchumi wa mkoa,” amesema Nkinda.