Prime
Wamiliki wa baa Kinondoni walalama kutwishwa zigo hili...
Muktasari:
- Wamedai kuwapa jukumu Wamiliki wa baa kukabiliana na kundi hilo ili waweze kukidhi matakwa ya leseni ya kufanyabiashara zao ni kuwaonea kwani biashara ya baa haibagui mtu kila mteja huwa wanamhudumia.
Dar es Salaam. Baadhi ya wamiliki wa baa wilayani Kinondoni wamezitaka mamlaka kuingilia kati udhibiti wa vitendo vya biashara ya ngono inayofanywa na baadhi ya wanawake maarufu ‘madada poa’ wakisema si jukumu la wamiliki wa baa kuwazuia.
Wamependekeza, endapo itaonekana inafaa, kundi hilo litambuliwe rasmi na kupewa leseni maalumu ili kutenganisha shughuli zao na biashara halali za baa.
Wamesema kuwatwisha jukumu la kukabiliana na madada poa ili kutimiza masharti ya leseni za biashara ni kuwaonea, kwa kuwa biashara ya baa haiwabagui wateja na kila anayefika hupatiwa huduma.
Wamiliki hao pia wamesisitiza kuwa wataendelea kuzingatia masharti ya Sheria ya Leseni za Vileo ya mwaka 1968 pamoja na kanuni za kudhibiti kelele zinazotokana na muziki, lakini changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni uwepo wa madada poa, hali inayochangia baadhi ya baa kutafsiriwa kuwa maeneo ya ukahaba.
Hoja hizo ziliibuliwa jana Ijumaa, Juni 26, 2026, katika kikao chao kilichodumu kwa saa tano katika Manispaa ya Kinondoni.
Kikao hicho kiliwakutanisha wamiliki wa baa, vilabu vya usiku na kumbi za starehe pamoja na maofisa wa wilaya kujadili changamoto zinazowakabili na utekelezaji wa sheria za biashara ya vileo.
Katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule aliwataka wamiliki wa baa kuhakikisha wanadhibiti vitendo vya ukahaba katika maeneo yao na kuendesha biashara kwa kuzingatia masharti ya leseni walizopewa.
Amesisitiza kuwa kutotekeleza maelekezo hayo kutasababisha kuendelea kwa operesheni za kufunga biashara zinazokiuka sheria.
Kikao hicho kilifanyika kufuatia operesheni ya kufungwa kwa baa 13, Februari 22, mwaka huu kwa madai ya kukiuka Sheria ya Leseni za Vileo ya mwaka 1968, ikiwemo kupiga muziki unaosababisha kelele na kufanya shughuli zisizoruhusiwa na leseni zao.
Miongoni mwa baa zilizofungwa ni Element, Big Joe, Velvet, Tips Coco Beach, Uncle's, Tips Mikocheni, Polosi ya Mikocheni, Babiloni Kona (Bwawani Mwananyamala), Kwa Joyce, Serengeti Bar, Hotea Bar, Raphael Kajubuli ya Makumbusho na Baikas Lounge.
Akizungumzia ugumu wa kudhibiti shughuli za madada poa, mmiliki wa baa ya Kwa Joyce Bar, Joyce Cosmas, amesema si rahisi kwa wamiliki wa baa kuwazuia au kuwafukuza kwa nguvu zao wenyewe, akisisitiza kuwa jukumu hilo linapaswa kubebwa na Serikali.
Amesema uchuuzi wa ngono ni shughuli inayofahamika ingawa haijatambuliwa rasmi na Serikali, hivyo endapo itaonekana inafaa, kundi hilo litambuliwe na kutengewa maeneo maalumu ya kufanyia shughuli zake.
"Kusema uwafungie wasifike kwenye baa si rahisi, kwa sababu wanapokuja pia wanaleta wateja. Wana maisha yao yanayoendelea, hivyo ukiwafukuza hapa utakutana nao sehemu nyingine. Mwisho wa siku hali itakuwaje?" amehoji.
Joyce amesema ni wakati wa Serikali kulitazama upyasuala hilo na namna ya kushughulikia huku akipendekeza watu wanaojihusisha na biashara hiyo wapewe vibali vya kufanya shughuli zao kwa utaratibu wa kisheria, ingawa amekiri kuwa jambo hilo haliendani na maadili na desturi za Kitanzania.
"Ukweli ni kwamba madada poa wako kila mahali mitaani. Wapo pia ambao hawajionyeshi wazi, bali wanafanya biashara ya ngono kupitia simu. Wanaoonekana kwenye baa, vilabu vya usiku na sehemu za starehe ndiyo wanaonekana zaidi," amesema.
Kwa mujibu wake, kundi hilo linaweza kutazamwa kama makundi mengine ya watoa huduma kwa kuwa linaendelea kuwepo katika jamii.
Amesema Serikali inaweza kuwatambua, kuwatoza ada za leseni na kuwatengea maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli hizo.
"Hawa madada poa wanapata kipato kupitia shughuli hiyo. Ingawa Serikali haijairasimisha, wateja wao ni watu wa kada mbalimbali, wakiwemo wenye nafasi kubwa hata serikalini na makundi ya jamii. Hivyo si jambo la kulipuuzia," amesema mmiliki huyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Baa na Kumbi za Starehe Tanzania (Ubakuta), Mponjoli Mwakabana amesema wafanyabiashara wa baa hawana mamlaka ya kuwachagua au kuwabagua wateja wanaowahudumia.
"Sisi tunabanwa na Sheria ya Leseni za Vileo ya mwaka 1968, hasa kuhusu suala la kelele. Hayo mengine tunapakaziwa tu. Kama mamlaka zinajua kuna watu wanaojihusisha na biashara hiyo, basi zina uwezo wa kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria," amesema.
Ma-DJ wasimamiwe
Ofisa Biashara wa Manispaa ya Kinondoni, Philipo Mwakibete amesema mfanyabiashara anayekiuka sheria anaweza kutozwa faini ya kati ya Sh200,000 na Sh1 milioni au kufikishwa Mahakama ya Biashara.
Hata hivyo, amesema mamlaka hupendelea kutoa elimu badala ya kuchukua hatua kali ili kuepusha kudhoofisha biashara.
"Kwa kuwa changamoto iliyotukutanisha hapa ni kelele, tukubaliane kila mmoja akanunue kifaa cha kudhibiti kelele ili tutakapofanya ukaguzi tukute taratibu zimezingatiwa," amesema.
Amesema wafanyabiashara wanaopiga muziki kwa sauti kubwa, hususan wakati wa wikiendi, wanapaswa kuomba kibali kutoka mamlaka za utamaduni na kueleza eneo watakalofanyia shughuli hizo.
Pia, amewataka kuwa na wasimamizi wa ma-DJ wao badala ya kuwaacha waamue wenyewe kuhusu muziki unaochezwa.
"Ombi langu ni kuhakikisha mnawasimamia ma-DJ wenu. Msiwaachie waamue peke yao kuhusu muziki unaochezwa. Zingatieni hilo," amesema.
Brela yasisitiza uzingatiaji wa sheria
Ofisa wa Leseni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Paulo Peter amesema taasisi hiyo inatumia Sheria ya Leseni za Biashara, Sura ya 101, kusimamia utoaji wa leseni za biashara mbalimbali, ikiwamo baa, vilabu vya usiku na kumbi za starehe.
Amesema kifungu cha 17 cha sheria hiyo kinawapa mamlaka maofisa kufanya ukaguzi na kuchukua hatua endapo biashara itabainika kufanya shughuli tofauti na zilizoainishwa kwenye leseni.
Ameongeza kuwa kifungu cha 14 kinatoa mamlaka ya kusitisha leseni iliyotolewa kimakosa au kwa kutumia taarifa za uongo, huku kifungu cha 26 kikiruhusu kuzuiwa kwa biashara endapo shughuli zake zinaweza kuhatarisha usalama wa watu, uchumi au taifa.
"Tunao uwezo wa kuzuia biashara endapo tutajiridhisha kuwa leseni haitumiki kwa shughuli iliyoidhinishwa au biashara inayofanyika ni kinyume cha sheria, mfano madanguro na shughuli nyingine zisizoruhusiwa," amesema.
Paulo amesema mamlaka zitaendelea kuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara watakaobainika kukiuka masharti ya sheria.
Aidha, amesema wamiliki wengi wa baa, vilabu vya usiku na kumbi za starehe bado hawajasajili majina na nembo za biashara zao Brela, akiwataka kufanya hivyo ili kulinda utambulisho wa biashara zao na kupata fursa mbalimbali za kiuchumi.
"Tunawasihi wote kusajili biashara zenu. Mbali na kulinda utambulisho wa biashara, usajili unawawezesha kupata mikopo, kushiriki zabuni na kutofautisha biashara zenu na za wengine," amesema.