MO aanza na KIUNGO mzambia

Muktasari:

Kama ulidhani Mohamed Dewji “MO” anatania, basi umeula wa chuya; ameliamsha dude.

Kama ulidhani Mohamed Dewji “MO” anatania, basi umeula wa chuya; ameliamsha dude.

Juzi Mo alitangazwa kuwa mshindi wa zabuni ya hisa za kuwa mmiliki mwenza wa klabu ya Simba akimiliki asilimia 50 na hivyo kuwa na haki ya kuingiza wajumbe saba kati ya 14 kwenye bodi ya uendeshaji klabu. Saba wengine wanawakilisha wanachama. Hiyo ndiyo Simba.

MO anataka kuifanya Simba kuwa klabu kubwa, tajiri na yenye kukusanya mataji. Wanaokusanya mataji ni wachezaji na Mo ameanza kwa kumtazama Jonas Sakuhawa kutoka Zambia.

Simba mwakani watashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kukosekana kwa takriban miaka mitano baada ya mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa 2012.

Lakini msimu huu wameanza kujipanga mapema kwa kusajili wachezaji ili kuboresha kikosi chao ambacho kitakwenda kwenye michuano hiyo kwa kutaka kusajili wachezaji wa maana ambao wanatajwa.

Majaribio

Simba imemleta winga Mzambia Jonas Sakuhawa ambaye yupo katika majaribio kwenye kikosi cha Joseph Omog ambacho hakijaonja ubingwa wa Ligi Kuu kwa miaka mitano.

Sakuhawa alizaliwa Julai 22, 1983 Kafue Zambia anacheza kama mshambuliaji wa kati au pembeni na amecheza timu kubwa Afrika na hata Ulaya pia.

Alianzia klabu ya Zesco United 2006-09, baadaye alikwenda Lorient ya Ufaransa ambako alicheza mechi 14 kati ya 2009-10 bila kufunga na mwisho wa msimu huo alikwenda kwa mkopo Le Havre pia ya Ufaransa.

Alijiunga na Al-Merreikh ya Sudan msimu wa 2011-12, kabla ya kutimkia zake TP Mazembe msimu wa 2013-14 na mwaka 2015 alirudi kwao Zambia na kujiunga na Zesco na sasa ametua Simba kwa majaribio.

Mkali wa mabao

Akiwa kikosi cha Al-Merreikh alicheza mechi 33 na kufunga magoli 22 na alipokuwa TP Mazembe alicheza mechi 29 na kufunga magoli 14. Kwa ujumla amecheza mechi 62 na kufunga magoli 36.

Sakuhawa ana wastani wa kufunga goli kila baada ya mechi mbili ambazo amecheza kwahiyo kama atakuwa na uwezo kama huo anaweza kuisaidia Simba yenye shida ya wafungaji.

Anavyocheza

Tangu atue Simba takriban wiki moja iliyopita, Sakuhawa amefanya mazoezi chini ya kocha msaidizi Mrundi Masoud Djuma aliyeshika nafasi ya Omog ambaye hayupo.

Muda wote aliokuwepo hapa nchini, Sakuhawa amefanya mazoezi vizuri na Simba kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini na alikuwa anaonyesha ana kitu cha ziada.

Sakuhawa amefanya mazoezi na Simba siku tano lakini ameonyesha utulivu, umakini uzoefu na amekuwa akifunga mara kwa mara katika mazoezi ya kufunga ambayo anapewa na Djuma.

Kiwanja chamzingua

Sakuhawa anasema amekuja moja ya timu kubwa barani Afrika kwa kuwa alikuwa akiisikia Simba. Lakini amekutana na changamoto ya uwanja ambao wanatumia kufanyia mazoezi. “Uwanja si mzuri hasa eneo la kucheza kama huko ambako nimetoka, lakini nitajitahidi kuonyesha kile ambacho ninacho katika siku zote ambazo nitakuwa nafanya majaribio hapa na kocha naimani anaweza kuona uwezo wangu licha ya changamoto hiyo,” anasema.

“Kama nikipata nafasi ya kucheza katika kiwanja ambacho kinaeneo zuri la kuchezea ninaimani nitaonyesha zaidi uwezo niliokuwa nao,” aliongezea Sakuhawa ambaye yuko katika wiki ya mwisho ya majaribio yake.

Liuzio awashtua Simba

Straika wa Simba Juma Liuzio, ambaye amekuwa na nafasi finyu ya kucheza mara kwa mara katika kikosi hicho msimu huu, alisema Sakuhawa ni mchezaji mzuri ambaye alishawahi kucheza naye Zesco United.

Liuzio anasema Sakuhawa ni mzoefu na alikuwa akicheza vizuri katika kikosi cha Zesco ambacho kilikuwa chini ya kocha George Lwandamina ambaye kwa sasa anainoa Yanga.

“Sakuhawa alikuwepo wakati Zesco inafika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutolewa na Mamelod Sundowns, kwa hiyo si mchezaji wa kumbeza ingawa sijamuona siku nyingi tangu mimi nilipoondoka Zambia,” anasema Liuzio.