Ma-RC, DC wanatambua kwamba ‘maendeleo hayana vyama’?

Muktasari:

Rais John Magufuli amewazoeza Watanzania jambo moja miongoni mwa mengi. Amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba “maendeleo hayana chama”. Hivyo ndivyo ilivyo na ndivyo kila mmoja anapaswa kuamini ukweli huo.

Jambo lolote linaporudiwa mara nyingi, hasa na kiongozi mkubwa wa kitaifa, huaminika katika jamii kuwa jambo hilo ndio ukweli wenyewe.

Rais John Magufuli amewazoeza Watanzania jambo moja miongoni mwa mengi. Amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba “maendeleo hayana chama”. Hivyo ndivyo ilivyo na ndivyo kila mmoja anapaswa kuamini ukweli huo.

Kauli hiyo Rais Magufuli aliirejea hivi karibuni alipokuwa akizindua barabara ya Uyovu- Bwanga, akisema Serikali imefanya maendeleo kwa ujenzi wa barabara, kitu ambacho anachokihitaji kwenye Serikali yake.

Huku akieleza kuna watu hawafurahii maendeleo na ndiyo maana wamekuwa wakijitahidi kufanya chokochoko, Rais alihoji: “Nani afurahi nchi hii inavyokaa kwa amani, nyinyi pale mmekaa yupo wa ACT-Wazalendo na wa Chadema yupo pale amekaa sawasawa, kila mtu na kila mahali wote tunajiona ndugu kwa sababu maendeleo hayana chama.”

Anaongeza: “Tunajenga hospitali ile, huyu wa ACT atashindwa kwenda pale? Barabara hii, wa Chadema si ndiyo wanawahi kwenda kuandamana mle. Hayo ndio maendeleo ninayotaka ya nchi yangu, hayo ndiyo maendeleo ya Watanzania,” alisema Rais Magufuli.

Pamoja na wananchi, viongozi wa ngazi mbalimbali, wakiwamo wateule wake, wanatazamiwa kuwa ndio waumini wakuu wa msemo huu maarufu.

Hata hivyo, baadhi ya wateule wa Rais, hasa wakuu wa mikoa na wilaya, wanaonekana ama hawajaielewa kauli hii au wameamua kutenda kinyume nayo; yaani kwao inaonekana maendeleo yana vyama.

Si jambo la ajabu kuona au kusikia baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wakitoa kauli au kufanya matendo ambayo ni tofauti na maana ya kauli hii ya “maendeleo hayana vyama”. Wanaona maendeleo hayawezi kupatikana endapo watu wa vyama tofauti vya siasa watawekwa katika kapu moja.

Hawa, ama wametangaza wazi kutoshirikiana na wapinzani au wanafanya vitendo vinavyoonyesha kuwatenga viongozi wa vyama vya upinzani.

Kwa mfano, hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti aliwataka madiwani wa Chadema mkoani humo kuhamia CCM ili aweze ashirikiane nao.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara kata ya Haydom wilayani Mbulu Februari 11, 2018, Mnyeti alisema yupo tayari kupokea simu ya diwani wa CCM hata akipigiwa usiku wa manane ili kumpa msaada lakini si diwani kutoka vyama vya upinzani.

kwamba diwani wa Chadema ni ngumu kufanikisha maendeleo ya wananchi kwa kuwa hakuna atakayemsikiliza akiwasilisha hoja zake katika vikao vya halmashauri husika.

“Hata hapa Haydom najua ni ngome ya Chadema..., sasa ondokeni huko mje huku tutekeleze ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 kwa kuleta maendeleo,” alinukuliwa akisema Mnyeti.

Kauli hiyo ilitokana na swali na mkazi wa kata ya Hayderer, John Tluway kuhusu kutofika kwa mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga katika kata yao inayoongozwa na diwani wa Chadema.

Akijibu swali hilo, Mnyeti anasema: “Mkuu wa wilaya ninakupongeza kwa kutofika kwenye kata hiyo kwani ningepata taarifa umefika mara ya kwanza, mara ya pili na mara ya tatu ningekuwa na shaka na wewe, lakini hongera sana kwa kutokwenda,” alinukuliwa akisema Mnyeti.

Katika kusisitiza uamuzi wake huo, Mnyeti akahoji, “Kwanza niwatambue Chadema kama nani? Mimi si NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) wala Msajili wa Vyama vya Siasa. Pili nishirikiane nao katika kutekeleza ilani ipi? Nimesoma ilani yote ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 sijaona mahali pametajwa Chadema, sasa nalazimika vipi kushirikiana nao?”

Awali alipokaribishwa katika mkoa huo mwishoni mwa mwaka jana, Mnyeti aliweka wazi adhma yake ya kutofanya kazi na wapinzani.

“Chama kinachotawala ni CCM, kama kuna mtu ana itikadi yake aifiche isionekane milele amina mpaka watakapotawala wao. Kwa hiyo tunategemea wote wanatekeleza ilani ya chama, tukikubaini unatekeleza ilani ya chama chako lazima tutakushughulikia.”

Jimbo la Babati Mjini lina mbunge wa upinzani (Chadema) na kwa upande wa madiwani katika kata nane CCM ilipata tatu.

Mbali na Mnyeti, mfano mwingine ni wa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ambaye amekaririwa akikiri kuwafukuza kwenye ofisi za umma wabunge wa Chadema, Halima Mdee (Kawe) na Saed Kubenea (Ubungo) akisema hakuna sheria inayomlazimisha kuwapa ofisi kwenye jengo la ofisi yake.

Hapi ameongeza kuwa wabunge hao wanapaswa kuwa na ofisi kwenye majimbo yao na siyo kwenye ofisi yake iliyopo katika jimbo la Kinondoni.

“Nimewaondoa ili waende wakakae na wananchi wao huko majimboni. Wanafanya nini kwenye ofisi yangu? Tunataka wabunge wawe karibu na wananchi wao ili wawatumikie,” alisema Hapi akisisitiza hiyo ilikuwa hisani tu.

“Isitoshe, hakuna sheria inayotulazimisha kuwapa ofisi, ‘it is just a privilege’” aliongeza Hapi.

Mwishoni mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala aliomba radhi uongozi wa CCM Taifa baada ya mgombea wa chama hicho kushindwa ubunge katika kata ya Ibighi iliyokuwa miongoni mwa kata 43 zilizofanya uchaguzi wa marudio na chama hicho kushinda katika maeneo mengine yote.

Makalla alisema CCM kushindwa kupata ushindi katika kata hiyo kumeutia doa mkoa wa Mbeya na wapaswa kujitafakari upya.

Wakuu hao wa wilaya ya mikoa ambao ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama kwenye maeneo yao, ni miongoni mwa wengine wengi wanaojitokeza kwenye kampeni za vyama vya siasa na ama kuwanadi wagombea wa chama kimojawapo au kuvikandamiza vyama vingine kinyume na majukumu hayo.

Wakizungumzia majukumu ya wakuu wa mikoa na wilaya, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema pamoja na wakuu hao kuwa makada wa chama kinachotawala, hawatakiwi kufanya kazi kwa kubagua vyama bali kujikita katika majukumu yao yaliyoainishwa kikatiba.

Maoni ya wasomi

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda anasema katika sheria ya tawala za mikoa ya mwaka 1997, hakuna kifungu kinachowataka wakuu wa mikoa au wilaya kufanya au kubagua wananchi kwa itikadi za siasa.

“Sheria haijaelekeza popote wakuu wa mikoa na wilaya kufanya shughuli za chama. Wanaofanya hivyo wanafanya kwa utashi wao wenyewe,” anasema Dk Mbunda.

“Ni kweli maendeleo hayana vyama, lakini tunaona viongozi wanaowasumbua wapinzani wanapandishwa vyeo, hii ni tofauti,” anaongeza.

Akijadili kuhusu sheria hiyo, Mhadhiri wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Jesse James anasema licha ya Sheria ya tawala za mikoa ya mwaka 1997 kutokuwa na kifungu cha kuwaruhusu wakuu wa mikoa na wilaya kufanya shughuli za vyama vya siasa, tatizo lake ni kuwa haitoi adhabu kwa anayekiuka.

“Ni makosa kabisa kwa mkuu wa mkoa au wilaya kufanya shughuli za vyama vya siasa, sheria haiwapi mamlaka hayo. Ndiyo maana tumeona wakati wa kampeni kuna wakuu wa wilaya walioshiriki kwenye kampeni walitakiwa kuripotiwa kwenye kamati ya Maadili ya Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC),” anasema Dk James.

Anasema licha ya kuwa wakuu hao ni makada wa CCM, hawapaswi kuonyesha mapenzi yao kwa vyama fulani vya siasa wala kuonyesha ubaguzi kwa vyama vingine.

Hata hivyo, Dk James anasema, “Sheria haisemi hatua watakazochukuliwa hata wakikiuka, labda ukitaka kuwashtaki utumie sheria ndogo na ukusanye ushahidi wa kutosha na mwisho wake mahakama itaishia tu kueleza kosa lake.”

“Kuna watu wanauliza mbona hamshtaki? Ni lazima ujue mfumo wa mahakama zetu, kesi kama hiyo inaweza kuchukua miaka mitatu minne, sasa ina faida gani? Mfumo wa mahakama wenyewe haushawishi watu kushtaki,” anaongeza.

Katiba na majukumu yao

Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 61 (1-5) inawatambua wakuu wa mikoa na kueleza kwa ujumla majukumu yao ambao kwa maoni ya wachambuzi ndiyo yangekuwa mpaka wa utendaji wa kazi kwa kuwa maendeleo hayana vyama.

Inasema, (1) Kutakuwa na Mkuu wa mkoa kwa kila mkoa katika Jamhuri ya Muungano ambaye, bila ya kuathiri ibara ndogo ya (3), atakuwa kiongozi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

(2) Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Bara watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.

(3) Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Zanzibar watateuliwa na Rais wa Zanzibar baada ya kushauriana na Rais.

(4) Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (5), kila Mkuu wa Mkoa, atakuwa na wajibu wa kusimamia utekelezaji wa kazi na shughuli zote za Serikali ya Jamhuri ya Muungano katika mkoa aliokabidhiwa; na kwa ajili hiyo, atatekeleza kazi na shughuli zote zilizotajwa na sheria, au kwa mujibu wa sheria kama hizi au shughuli za Mkuu wa Mkoa na atakuwa na madaraka yote yatakayotajwa na sheria yoyote iliyotungwa na Bunge.

(5) Pamoja na wajibu na madaraka yake yaliyotajwa kwenye masharti yaliyotangulia ya ibara hii, Mkuu wa Mkoa kwa mkoa wowote katika Tanzania Zanzibar atatekeleza kazi za shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar atakazokabidhiwa na Rais wa Zanzibar, na kwa mujibu wa Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar 1984 au sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

Sheria inayowaongoza

Mbali na Katiba, pia Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997, inaeleza mamlaka na majukumu ya wakuu wa mikoa.

Miongoni mwa majukumu hayo ni kuhakikisha ulinzi wa sheria na utulivu katika mkoa, kuongoza na kusimamia operesheni za maafa na kufariji, kama mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Mkuu wa mkoa atawajibika kufanya jitihada za kuhakikisha kutimizwa kwa sera za Serikali juu ya mkoa husika.

Kwa kushirikiana na Katibu tawala, RC atahakikisha na kufanya yale yote yatakayosaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa mkoa na kuhakikisha serikali za mitaa zinatimiza wajibu wake na kupata hati safi.