Mabingwa wa Afrika ndani ya Tanzania

Muktasari:

Hazina hiyo ndiyo iliyoipa ubingwa wa Afrika ikiwa ni mafanikio ya pili kwa Afrika Kusini kwani ni miaka 21 tangu Orlando Pirates kutwaa ubingwa huo mwaka 1995.

Licha ya kufungwa bao 1-0 na Zamalek ya Misri mjini Cairo katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana, Mamelodi Sundowns ilikuwa na hazina ya mabao 3-1 ya mchezo wa kwanza uliofanyika Pretoria, Afrika Kusini.

Hazina hiyo ndiyo iliyoipa ubingwa wa Afrika ikiwa ni mafanikio ya pili kwa Afrika Kusini kwani ni miaka 21 tangu Orlando Pirates kutwaa ubingwa huo mwaka 1995.

Inaelezwa kuwa mchezo huo wa fainali ulikuwa wa ushindani huku mabenchi ya timu zote presha ikiwa juu, Zamalek wakitaka kurudisha washinde, Mamelodi wakitaka kuongeza. Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Borg El Arab, Cairo.

 

Mamelodi ilikoanzia

Mamelodi Sundowns ilitokana na watu wa Marabastad, katika eneo lililokuwa na utamaduni mchanganyiko Kaskazini Magharibi mwa Pretoria.

Klabu hiyo ilianzishwa mwaka 1960 na kundi la vijana, kabla ya kuwa timu ya soka mwaka 1970. Kwa sasa klabu hiyo inamilikiwa na bilionea wa madini, Patrice Motsepe.

Tangu kufahamika kuwa klabu ya Ligi Kuu Afrika Kusini, PSL mwaka 1996 Sundowns imetwaa ubingwa mara saba.

Mbali na ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika 2016 na pia ni klabu bora Afrika.

Pia imetwaa ubingwa wa Nedbank Cup mara nne, na ndiyo klabu pekee Afrika Kusini kucheza Kombe la Dunia la FIFA ngazi ya klabu.

 

Watua Tanzania

Mamelodi ilitua nchini wiki iliyopita na kucheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Azam FC. Ilikuwa icheze na African Lyon kabla ya mchezo kufutwa na awali ilipangiwa kucheza na Simba na Yanga lakini baadaye zilichomoa.

Ilikubali kucheza na Azam, na ilitoka nayo suluhu. Azam itaiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho lakini ikipangwa kuanzia raundi ya kwanza ya kombe hilo ikisubiri mshindi kati ya Orapa United ya Botswana na Mbabane Swallows ya Swaziland.

Mamelodi imetumia mechi hiyo kama sehemu ya maandalizi ya mchezo maalumu wa ufunguzi wa msimu wa mashindano ya klabu Afrika (Super Cup) dhidi ya TP Mazembe utakaofanyika Februari 18 mwaka huu kwenye uwanja wa Loftus Versfeld jijini Pretoria, Afrika Kusini.

Mbali na kujiandaa na mchezo dhidi ya Mazembe, pia mechi hizo zilikuwa maalumu kwa ajili ya kupiga vita mauaji ya tembo nchini.

 

Msafara wao kiboko

Msafara wa Mamelodi uliowasili nchini, Januari 30 ukiwa na watu 41, wachezaji wakiwa 23, maofisa wa benchi la ufundi 13 na maofisa wengine wa timu watano.

Miongoni mwa watu maarufu waliokuwemo kwenye msafara huo ni kocha wao, Pitso Mosimane ambaye aliiongoza timu hiyo kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita. Mosimane ndiye kocha bora wa Afrika mwaka 2016.

Pia yupo nahodha na kiungo wao Hlompho Kekana na mshambuliaji Teko Modise ingawa hawakuambatana na mastaa wawili wa timu hiyo, kipa Joseph Onyango na kiungo Khama Billiat.

Hata hivyo wachezaji hao waliungana na timu hiyo siku moja baadaye baada ya majukumu ya Fainali za Afrika nchini Gabon wakiziwakilisha nchi zao za Uganda na Zimbabwe.

Ni msafara ambao uliacha gumzo kwa watu mbalimbali waliokuwepo uwanjani hapo, kutokana kuja na mizigo mingi. Kulikuwa na mabegi makubwa ya vifaa kama jezi, mipira, sare za mazoezi na viatu.

Pia walitua na katoni nyingi za maji, juisi maalumu za kuongeza nguvu kwa wachezaji ambazo walizitumia kwa muda wote waliokuwa nchini huku pia wakija na makasha ya dawa na mahitaji yao mengine.

 

Nidhamu ya hali juu

Kama kuna mambo ambayo timu na wachezaji wetu wanaweza kujifunza kwenye ujio wa Mamelodi, basi ni nidhamu.

Ndani ya muda mfupi waliokaa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, JNIA, nyota wa timu hiyo waligoma kuzungumza na vyombo vya habari kwa maelezo kuwa wanaopaswa kufanya hivyo ni kocha mkuu na nahodha wao.

Nidhamu hiyo waliionyesha hata wakati wa kupanda basi waliloandaliwa kwani hawakulikimbilia kupanda hadi pale Mosimane ambaye alichelewa kutoka kwenye ukaguzi, kuwaruhusu wachezaji hao kuingia kwenye basi hilo.

 

Wanaishi kwa ratiba

Ratiba ya timu hiyo ambayo ilifikia hoteli ya Bahari Beach iko hivi.

Muda wa kuamka ni saa tatu asubuhi, kila mchezaji anatakiwa awe amevaa sare ya timu ambayo ni kofia, fulana na track suit.

Saa 3.30 asubuhi ndio muda wa timu nzima kupata kifungua kinywa kisha wachezaji huenda kupumzika hadi saa 7.00 mchana ambao ni muda wa chakula cha mchana.

Wachezaji hurudi tena kupumzika hadi jioni na safari za kwenda uwanjani kwa ajili ya mazoezi huanza na mazoezi hufanyika saa 1.00 usiku hadi saa 2.30 kisha hurejea hotelini kwa ajili ya kula, kutazama TV kisha inapofika saa 4.30 kila mchezaji anapaswa kulala.

Ratiba ya kula huandaliwa na mtaalamu wao wa virutubisho aitwaye Ursula Botha ambaye yeye hakusafiri na timu.

Timu hiyo imeweka sheria ya kupiga faini wachezaji wake iwapo wanavaa mavazi tofauti na yale waliyopangiwa na pia ni kosa kwa mchezaji kuvaa kaptura na badala yake kila mmoja kwenye msafara ni lazima avae suruali nje ya uwanja.

 

Mosimane atoa neno

Kabla ya kuondoka uwanjani hapo, kocha mkuu wa Mamelodi Sundowns, Pitso Mosimane anasema kuwa ilikuwa rahisi kwao kuja Tanzania wakiamini watapata kile wanachokihitaji.

“Tumekuja Tanzania tukiamini kuwa hapa kuna timu nzuri ambazo zitatupa nafasi ya kupima kiwango chetu ukizingatia kuwa tulikuwa na wiki moja tu ya mazoezi baada ya kupumzika kwa takribani wiki nne.

Tunaziheshimu timu za hapa na tunaamini zitatupa ushindani mkubwa kwani soka la Tanzania limeimarika kwa kiasi kikubwa na ndio maana tumekuja na kikosi kizima isipokuwa Onyango na Billiat.

 

Kauli ya nahodha

Nahodha wa Mamelodi, Hlompho Kekana alikiri kuwa mechi ya Azam imesaidia kuwaimarisha licha ya kuwa walitaraji kucheza na Simba na Yanga ambazo zote zilichomoa.

“Hatuzifahamu timu za Tanzania lakini tunaamini ni timu nzuri ambazo zimetusaidia kutuimarisha kuelekea mechi yetu dhidi ya Mazembe na ligi ya ndani.

Tunafurahi kuona tumepata mapokezi mazuri na ninaamini mashabiki waliojitokeza uwanjani, na wameona soka safi ya kuvutia,” anasema Kekana.

Naye mratibu wa ujio wa Mamelodi, Rahim Zamunda alisema kuwa ujio wao ni fursa muhimu kwa soka na sekta ya utalii nchini.