UCHAMBUZI: Madawati sawa, ila tumeandaa pa kuyaweka?

Muktasari:

Jambo hilo limefanya shule nyingi kukumbwa na ‘mafuriko’ ya wanafunzi. Mathalani, mwalimu wa shule moja iliyopo nje kidogo ya jiji la Dar es salaam alinukuliwa hivi karibuni akisema kuwa ingawa shule yake ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 945 tu, sasa hivi imelazimika kuchukua wanafunzi 5,876!

Kufuatia tamko la Serikali kuhusu elimu bure ambayo imefuta ada na michango katika elimumsingi, wazazi wengi ambao awali walikuwa wameshindwa kuwaandikisha watoto wao kutokana na kushindwa kumudu gharama za shule, sasa wamejitokeza kuwaandikisha watoto.

Jambo hilo limefanya shule nyingi kukumbwa na ‘mafuriko’ ya wanafunzi. Mathalani, mwalimu wa shule moja iliyopo nje kidogo ya jiji la Dar es salaam alinukuliwa hivi karibuni akisema kuwa ingawa shule yake ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 945 tu, sasa hivi imelazimika kuchukua wanafunzi 5,876!

Ni dhahiri kuwa jambo hili limesababisha shule nyingi kukumbwa na uhaba mkubwa wa madawati, walimu na madarasa pia kiasi cha kuwalazimu wanafunzi wengi kusomea nje na chini ya miti.

Hivyo, watoto wengi nchini wamekuwa wakisoma kwenye mazingira magumu sana kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa pamoja na madawati.

Hali hii si nzuri kiafya na kimasomo; ni kama vile tunarudi nyuma badala ya kusonga mbele.

Swali ambalo watu wamekuwa wakijiuliza ni je, wakati Serikali ilipokuwa ikija na sera ya elimu bure haikufikiria kwamba wazazi wengi walioshindwa kuwaandikisha watoto wao kwa kukosa ada, wangeichukulia fursa hiyo kuwaandikisha watoto wao kwa wingi?

Hilo limepita.Kwa bahati nzuri Rais John Magufuli alilibaini tatizo hili na kuiagiza mikoa yote ihakikishe ina madawati ya kutosha ifikapo Juni 30.

Kutokana na agizo hilo, mikoa mingi imejitahidi kutengeneza madawati kwa ajili ya shule zake.

Taasisi na hata baadhi ya watu binafsi wamekuwa wakijitolea kusaidia madawati

Kutokana na juhudi hizi za wananchi, kwa kiwango kikubwa sasa madawati mengi yameshatengenezwa na mengine bado yanaendelea kutengenezwa.

Hii ni kusema shule nyingi za msingi sasa zimejaa madawati.

Kwa kweli katika maeneo mengi madawati sasa yamefurika kiasi kwamba hakuna hata sehemu ya kuyaweka!

Hivyo kuna hatari dhahiri madawati mengine yakaishia kuwekwa nje kwa sababu hamna madarasa au sehemu nyingine salama za kuyaweka na hivyo kuwa katika hatari ya kuibiwa au kuharibika.

Hapa tena watu wamekuwa wakijiuliza, inawezekanaje kuamrisha kutengeneza madawati mengi kiasi hicho wakati shule hizohizo hazina vyumba vya madarasa vya kutosha kwa ajili ya kuweka madawati hayo?

Je, Serikali haikutafakari kwamba huenda shule hizo zikaja kuwa na changamoto ya vyumba vya kufundishia?

Kwa maana nyingine, baada ya tatizo la madawati kuwa limetatuliwa kwa kiasi kikubwa sasa tatizo la uhaba wa madarasa limeibuka!

Katika baadhi ya shule ukosefu huu wa vyumba vya madarasa umesababisha wanafunzi wa madarasa tofauti kusomea katika chumba kimoja; hali inayosababisha kuwa na mwingiliano katika masomo.

Hapa tena mtu unajiuliza, je, Serikali ilishindwa vipi kufikiria athari zitakazotokea wakati wa kutekeleza sera hiyo mpya?

Je, Serikali haikujua kwamba kuna uhaba wa madarasa katika shule nyingi nchini?

Hivi hakuna kiongozi aliyeweza kutegemea kuwa baada ya kutolewa kwa tamko hilo la elimu bure, wazazi wengi wangejitokeza kwa wingi kuandikisha watoto wao shule na hivyo kusababisha shule kuwa na wanafunzi wengi na madarasa machache hususani katika shule za msingi?

Kwa mfano katika shule moja ya msingi iliyopo mkoani Kigoma watoto wanalazimika kwenda kusomea msikitini kwani shule yao haina madarasa ya kutosha.

Watoto wanaoandikishwa shule ya awali wamekuwa wengi na kuvuka idadi inayotakiwa na hivyo kusababisha ugumu kwenye ufundishaji.

Katika shule nyingine hali imekuwa mbaya kiasi kwamba wanafunzi wa madarasa tofauti wanalazimika kusomea chini ya mti mmoja kwa kupeana mgongo; hali ambayo inasababisha kuingiliana kwa masomo.

Je, hali hii itamlazimu tena Rais Magufuli kutoa tamko la kampeni ya kitaifa ya ujenzi wa madarasa ili kutatua tatizo hili ili kuboresha mazingira ya kusomea?

Kwa kuwa shule nyingi nchini zinakabiliwa na uhaba huu wa vyumba vya kusomea, ingekuwa busara kama zoezi kama hili la madawati lingeletwa ili kuwahamasisha wananchi, taasisi na wadau wengine kujitolea kujenga madarasa.

Sidhani kuwa itakuwa busara kujipiga kifua kuwa mikoa yote sasa ina madawati lukuki wakati madarasa ya kusomea wanafunzi na kuhifadhia madawati hayo hayapo!

Sarah Phillip anafanya mazoezi ya vitendo katika Shirika la HakiElimu. Anapatikana kwa baruapepe: [email protected]