Maendeleo ya teknolojia : uzuri na tahadhari

Muktasari:

  • Taarifa hii iliyokusanywa kifanisi na Maelezo inamulika wananchi wa kawaida, Korogwe, Dodoma , Mwanza vijijini, na kudokeza kule tunakoelekea.

Muhtasari uliotolewa kushehererekea miaka miwili ya uongozi wa awamu ya tano, umesisitiza umuhimu wa viwanda. Kwa Watanzania hili ni jambo zuri sana. Rais JP Magufuli anasisitiza sana sayansi na teknolojia kwa ajili ya wananchi.

“ Serikali yetu ni kama wazazi, “ anasema Bi Bokhe Bwire, mmoja wa wahojiwa kiwanda cha chaki cha Maswa, “ ni kama wametulea, wametupa mafunzo, ...wametusaidia kupata mikopo mbalimbali, pia wametupa hifadhi....”

Taarifa hii iliyokusanywa kifanisi na Maelezo inamulika wananchi wa kawaida, Korogwe, Dodoma , Mwanza vijijini, na kudokeza kule tunakoelekea.

Ukweli teknolojia ndiyo nguzo ya jamii yeyote ile. Huku Uzunguni maendeleo hayo yalishika moto karne ya 19 ndipo Wazungu wakaanza kuzunguka kila mahali na kutaka mali ghafi kupitia makoloni. Historia ya karne 20 iilihusu vita vya mali ghafi. Hatimaye teknolojia imesambaa. Karne ya 21 imeshuhudia maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano. Chombo mahsusi kinachoongoza ni kompyuta. Takriban kila sehemu inaendeshwa na kompyuta Majuu. Na hapo usalama wa kitengo hiki umekuwa nguzo kuu ya askari doria kila pembe ya sayari yetu. Kuna mazuri na mabaya kuhusu maendeleo haya.

Kipengele tunachokijua zaidi kuhusu maendeleo haya ya kompyuta ni simu za mkononi.

Uzuri wake hausemeki.

Leo ni rahisi kuwasiliana popote pale haraka kupitia simu. Ubaya wake hata hivyo umeanza kuonekena. Mfano ni namna wananchi hasa vijana na watoto wanavyoanza kusahau kabisa mila na desturi za mawasiliano. Tuliozaliwa na kukulia kipindi ambacho vifaa hivi havikuwepo mawasilino ni jambo la kawaida. Ila walioingia miaka 20 iliyopita kuja mbele, suala la mahusiano ni tofauti.

Utafiti uliofanywa na shirika la Casumo, kuhusu matumizi ya simu karibuni umesititiza matumizi ya kifaa hiki yanasababisha ajali, hadharani. Uchunguzi ulioangalia Waingereza 2,000 ulithibitisha asilimia 20 hujishtukizia wamegongana au kuanguka kutokana na kutembea huku wakisoma au kuandika juu ya simu.

Suala jingine la kiteknolojia hii ni namna watoto wadogo wanavyotazama sana ngono na kuanza ubakaji mapema. Wanausalama wanakiri idadi ya watoto chini ya umri wa miaka 18, wanaokutwa wakitazama ngono katika simu imeongezeka maradufu kati ya 2015 na sasa. Ongezeko hili liko sambamba na utafiti mwingine ulioonesha kuwa asilimia 84 ya watoto Uzunguni hupoteza muda mwingi wakitazama (vioo) vya kompyuta badala ya kucheza au kufanya shughuli za mikono. Huu ni mfano mahsusi wa matokeo ya maendeleo ya viwanda, ambapo waanadamu tunapitiliza mstari.

Ugunduzi mwingine mpya ni wa magari yasiyokuwa na madereva. Taarifa zinazoendelea kutolewa na vyombo vya habari zinasisitiza ifikapo 2030 itakuwa kawaida kuwa na magari yanayojiendesha yenyewe.

Magari haya yatawafaidi walemavu, wazee, na wale wasio na leseni.

Na linalostua zaidi (na labda tulizungumzie zaidi makala zijazo) ni la Wazungu kuanza kubatili wanaume wanaotaka kuzaa. Miaka michache ijayo itakuwa kawaida kwa wanaume kufanyiwa upasuaji na hatimaye kuwa waja wazito. Hatua hii imezua watu wa jinsia mpya wanaoitwa “trans” na ni mada kubwa sana Uzunguni.

Wakati Waafrika tukifurahia maendeleo yetu ya msingi na viwanda, ni muhimu kuzingatia sisi hatutaki teknolojia ivuke mipaka kama ilivyowafikia wenzetu weupe.