Maisha ya Ulaya jinsi yalivyo ‘pasua kichwa’

Muktasari:

  • Lilikuwa tukio la huzuni na la kutisha, hasa ukichukulia kuwa wahusika wote ni wageni katika nchi ya Ulaya. Msiba unapotokea ugenini hasa Ulaya unaleta simanzi kwa wanajamii wanaohusika hasa Watanzania, kwa sababu mara kadhaa wanalazimika kuchangia gharama za kusafirisha mwili, hasa familia husika inapokuwa na kipato duni.

Asubuhi ya mwisho wa mwezi Machi mwaka huu, mitandao ya kijamii ilifurika habari ya majonzi kutoka Jijini London, Uingereza ambako Mtanzania, Leyla Mtumwa (36), aliuawa kwa kuchomwa kisu na mtuhumiwa Mtanzania mwenzie Belly Kasambula (38) ambaye amekamatwa na kesi yake iko mahakamani huko London.

Lilikuwa tukio la huzuni na la kutisha, hasa ukichukulia kuwa wahusika wote ni wageni katika nchi ya Ulaya. Msiba unapotokea ugenini hasa Ulaya unaleta simanzi kwa wanajamii wanaohusika hasa Watanzania, kwa sababu mara kadhaa wanalazimika kuchangia gharama za kusafirisha mwili, hasa familia husika inapokuwa na kipato duni.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na rafiki wa marehemu kuwa: Usiku wa wa kabla ya kutokea tukio, Leyla na Kasambula walikwenda muziki na waliporejea nyumbani wenza hao walianza kugombana. Kinachoonekana hapo ni kuwa mwanaume huyo hakukubariana na kitendo cha Leyla kwenda kujirusha kama inavyofahamika kwa wengi, aliingia hasira na hatimaye kufanya kitendo cha hatari kilichopelekea kupoteza uhai wa mwenzie.

Nia yangu si kuingia kwa undani kwenye tukio hilo bali kwa hayo ni matokeo ya kile ambacho wengi wetu hatukijui kuhusu maisha ya Ulaya yalivyo, wengi tumekuwa tukikubali kuwa hali ya huko ni njema na kila aendaye ni lazima ‘atoboe’.

Wapo vijana wengi ambao wako barani Ulaya kwa sasa wanahaha kutafuta wapenzi hukohuko ughaibuni, hapa nyumbani na mahali popote ambapo wanaweza kuwapata wenza ili waweze kuishi kwa pamoja. Hivyohivyo wapo vijana wa kike ambao wangependa kupata mwanaume aliyepo Ulaya ili wakale maisha kama tulivyozoea kuita na wengine wanapendelea wanaume wa Kizungu au wanawake wa Kizungu.

INAENDELEA UK 24

INATOKA UK 23

Kwa kiasi kikubwa mitandao ya kijamii inasaidia sana kupata kile wanachohitaji, huko hakuna mahojiano ya kutizama chini, kuchezesha ulimi wala mguu ni simu yako na ujanja kidogo.

Kwa bahati mbaya huko kuna ujanja na udanganyifu hali ya juu sana, katika uwanda huu wa kidigitari, kwa mfano kijana wa kiume anaweka picha zake nyingi kwenye mitandao kama Facebook, Instagram au Twitter akijionyesha mwenye tabasamu, afya murua, mavazi ya kisasa na vilevile mazingira safi na mandhari za kuvutia ili tu kuwavuta akina dada ambao kwa bahati nzuri kwake wapo Afrika ambako mazingira ya Ulaya wanayaona kama mazingaombwe kwao au kama wanavyoiita Bling bling nyingi. Hii hata kwa wanawake pia wanatumia njia hii vilevile.

Lakini, ndani ya picha hizi kuna matatizo makubwa ambayo hakuna anayeweza kuyajua bila kusafiri na kwenda kuishi huko japo kwa muda mfupi. Maisha ya Ulaya yamejaa msongo wa mawazo ambao siyo wa kawaida na kuna wakati hasa wageni wanaingia katika majaribu mbalimbali hata ya kutaka kujinyonga. Wapo vijana ambao ninawafahamu walijiingiza katika biashara ya kuuza dawa za kulevya katika mitaa kama vile barabara ya Oxford na Mandela Court mjini Reading.

Mbali na hapo wapo wengine ambao wameamua kufunga safari kabisa za kuja Afrika kuoa, Waafrika tumezoea kuwa anayeoa ni mwanaume, la hasha hata kama dada katoka Uingereza kuja Tanzania na akarudi na mume Ulaya walioko kule wanajua kuwa aliyeolewa ni mwanaume na aliyeoa ni yule aliyemwingiza mgeni kwa wazungu.

Kwa bahati mbaya kuanzia Oktoba hadi Aprili kwa kila mwaka, maisha huwa ni magumu sana kwa sababu ni kipindi cha baridi kali na upatikanaji wa kazi huwa ni mgumu sana, wakati huohuo gharama za maisha huwa juu kwa sababu matumizi ya gesi yanapanda kwa kiasi kikubwa, njaa huwa inauma sana wakati huo, hivyo basi huo ndiyo wakati ambao unatakiwa kuwa na akiba ili kusaidia kuendesha maisha.

Kwa mgeni ambaye anapokosa kazi hapati usaidizi kutoka serikalini, hapo huwa ni mtihani tosha kwa sababu kulipia gharama za nyumba, ankara za gesi ya kuzalisha joto ndani ya nyumba, umeme, kodi za Halmashauri ya miji na kama uliingia nchini humo kama mwanafunzi na huna ndugu mwenye uwezo kutoka nyumbani wa kukusaidia, basi wenyewe wanaita utatia adabu pasipo kulazimishwa kwa sababu ada ya chuo nayo ni jinamizi jingine.

Sasa basi ili kujaribu kupambana na changamoto hizi za kimaisha wageni wengi hapa ni kwa jinsia zote, wanawake kwa wanaume wanajaribu kutafuta wenza ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha. Wapo vijana wanaoamua kuja Afrika na wapo ambao wanashawishiana hukohuko na kuamua kuishi kama mume na mke au sogea tuishi ilivyozoeleka hapa nyumbani.

Hivyo basi, mtindo huu wa maisha haujengi kile kitu kinaitwa ndoa, unaleta utaratibu wa maisha wa kusaidiana ili kukabili changamoto za kimaisha, ingawa wapo wanaofanikiwa hata kupata watoto na maisha kuendelea hadi uzeeni. Walio wengi hawapendi kuitana bibi na bwana badala yake wamechukua msemo wa kimagharibi na kupenda kutambulishwa kama mtu na mwenza wake.

Kwa mantiki hiyo, iwe kwa kijana wa kiume au wa kike kuwa na mwenza wako kwa sehemu kubwa kunasababishwa na changamoto za maisha na kwa hakika Ulaya haina huruma kwa mgeni kwa sababu hakuna kula, kulala kwa mjomba na shangazi, ni lazima utumike kuijenga nchi huku wenyeji wakila kwa ulaini kwa ujumla ni hali ya utumwa ambao hauna viboko wala mijeredi.

Sasa basi ni vizuri kujua kuwa maisha ya aina hii hayana ule mfumo wa baba au mama mwenye nyumba, wote hapo ni wahanga wa maisha na inabidi muwe wapole ili kusonga mbele. Hakuna anayeratibu nini kifanyike kinachotakiwa ni kukimbizana na paundi ya Malkia.

Kutokana na ugumu wa maisha nimewahi kushuhudia dada mmoja ambaye aliletwa na jamaa yetu kutoka hapa nyumbani kama rafiki yake, lakini alipoonja mikikimikiki ya maisha akaamua kumkimbia na kwenda zake na kuhamia jimbo la Scotland ili kutafuta hadhi ya ukimbizi (Kujiwasha), kwa sababu ukifanikiwa kupata hadhi ya ukimbizi mzigo wa kuendesha maisha yako unabebwa na Serikali, unaweza kupata nyumba, ukalipiwa umeme, maji, gesi na kupewa fedha za chakula na nauli ya mabasi na treni, matibabu na mambo mengine yenye kurahisisha maisha.

Hivyo basi kwa upande huo ukawa mshindi. Lakini kwa kuwa ni utaratibu mgumu na wa kubahatisha wengi huamua kufuata njia ya kwanza, tafuta mwenza na kuhamisha makao au kumhamisha mwenzio, hakuna anayejali kwa hilo Ulaya kila moja anajitahidi kupambana na hali yake.

Kwa upande wa wanaume hata ukifanikiwa kupata hadhi ya ukaazi au ukimbizi na kuwa na nyumba, lakini sheria za Uingereza zimempa mwanamke nguvu kubwa sana ambayo akiiitumia mtakapokorofishana utaumia sana kwa sababu utapoteza nyumba na hata kama mmepata watoto utawekewa masharti magumu sana ya kuwaona.

Ili kukabiriana na ugumu wa maisha haishangazi kumkuta kijana wa kiume wa Kitanzania akijivinjari na mke wake mwenye umri ambao ni sawa na bibi wa kumzaa mama au baba yake, hivyohivyo kwa msichana kumkuta akiwa na babu yake ukiuliza utaambiwa maisha na makaratasi.

Makaratasi ni nyaraka za kukuwezesha kuishi kama raia wa Uingereza na kupata mahitaji yote ambayo ni ya lazima kwa raia wa nchi hiyo, hasa unapokosa kazi kwa hiyo wengi huona kama wamepata aina fulani ya ushindi ingawa nina uhakika wengi hawana furaha na maisha ya aina hiyo zaidi ni kuigiza tu.

Binafsi nikiishi mjini Reading, Kusini mwa Uingereza mwaka 2005 niliwashuhudia wanaume wawili moja wa Kitanzania na mwingine Mkenya ambao walitimuliwa na wake zao kutoka majumbani mwao na kushia kuishi kwa kubahatisha kwa marafiki, ndugu na jamaa au vituo vya kusaidia watu wasio na makazi.

Mwaka huohuo nikiwa barabara ya Workingham, mjini huohuo nilishuhudia kijana wa kiume wa Kiingereza akichapwa vibao na mke wake na kuporomoshewa matusi makubwa pasipo kujibu, kwa sababu kwa kufanya hivyo kungempeleka jela kwa kipindi kisichopungua miaka miwili.

Hivyo basi, kwa wanaume wanaotarajia kuishi na wapenzi wao wa kike nchini Uingereza inawabidi kuwa makini sana, kwa sababu huko hakuna amri kwa mwanamke na lililo kubwa ni kufanya jitihada kubwa kuzijua sheria na hata utamaduni wa nchi yenyewe, siyo kwamba Uingereza hakuna mfumo dume hapana upo ila kulingana na sheria zilizopo wanaume inawabidi wakubali yaishe.

Nimewashuhudia baadhi ya watu ninaowafahamu kutoka Tanzania wakilala mahabusu za polisi za Thames Valley kwa sababu ya mzozo mdogo tu na wapenzi wao, kitu ambacho ni nadra sana kukiona barani Afrika ambako mwanaume ndiye mtawala wa mfumo mzima wa uendeshaji wa familia.

Sheria hizi za kuwapendelea wanawake zilipitishwa kipindi ambacho Margareth Thatcher alikuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo kuanzia mwaka 1979 hadi 1990. Alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke barani Ulaya. Umadhubuti wake katika kuendesha Serikali ulimfanya aitwe mwanamke wa chuma (Iron Lady)

Hivyo basi, kijana wa kiume na wa kike kabla hujaamua kusafiri kwa mtindo huu ni vizuri ukafanya utafiti wako, lakini kwa bahati mbaya Watanzania walio wengi hawataki walioko nyumbani wajue ni madhila gani wanayapitia ughaibuni.

Idd Amiri ni mwandishi wa habari aliyewahi kuishi nchini Uingereza.

[email protected], 0783 165 487