Maisha ya kisiasa ya Rais Mteule, George Weah

Muktasari:

  • Lakini, Watanzania wanamkumbuka zaidi Weah alipokuja nchini mwaka 1997 akiwa na Timu ya Taifa ya nchi yake kucheza na Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Jina la George Weah si geni masikioni mwa watu. Wengi wanamfahamu kwa umahiri aliokuwa nao katika kucheza soka tangu miaka ya 1990 alipokuwa anachezea klabu mbalimbali katika nchi za Ulaya.

Lakini, Watanzania wanamkumbuka zaidi Weah alipokuja nchini mwaka 1997 akiwa na Timu ya Taifa ya nchi yake kucheza na Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Mbali na mchezo huo uliofanyika Februari 22, 1997 na kumalizika kwa sare ya 1-1, pia kulitokea hofu kwa klabu ya Simba kwamba pengine angeondoka na mchezaji wake raia wa Liberia, William Fahnbulleh. Hata hivyo, Weah alifanya mazungumzo na aliyekuwa mfadhili mkuu wa Simba, Azim Dewji na Fahnbulleh alibaki kuendelea kuichezea klabu hiyo.

Weah alipokuja Tanzania alikuwa akitokea timu ya AC Milan ya Italia alikokuwa akichezea soka la wa kulipwa. Pia, Weah anayeapishwa rasmi kesho, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pekee kutoka Afrika aliyeshinda tuzo ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) ya mchezaji bora wa dunia mwaka 1995. Pia, mwaka huo alipata tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Ulaya.

Alipata umaarufu alipokuwa katika klabu za Monaco FC (1987-1992), Paris St Germain (1992 - 1995), AC Milan (1995 - 1999), Chelsea (1999 - 2000), Manchester City (2001) na Olympic Marseille (2001 - 2002). Pamoja na mafanikio yake yote makubwa kwenye soka,

INAENDELEA UK 26

INATOKA UK 25

Weah alionyesha kupenda siasa hasa katika nchi yake ambayo kwa muda mrefu ilikuwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha vifo vya watu wengi.

Weah ambaye alizaliwa mwaka 1966, alikuwa akitoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa vita nchini humo. Hata hivyo, baadaye alitangaza rasmi kugombea urais mwaka 2005 ikiwa ni miaka mitatu tangu astaafu soka.

Alianzisha chama cha CDC (Congress for Democratic Change) na kugombea kupitia chama hicho dhidi ya Rais wa nchi hiyo, Ellen Johnson Sirleaf, msomi wa Chuo Kikuu cha Havard cha Marekani.

Katika uchaguzi huo, Weah alikabiliana na upinzani mkali hoja kubwa ikiwa ni kwamba hana elimu na uzoefu wa kutosha kuongoza nchi. Pia, alituhumiwa kwamba alibadilisha uraia wake, madai ambayo aliyakana na kusafishwa na Mahakama ya nchi hiyo.

Hata hivyo, Weah alishindwa katika uchaguzi huo na Sirleaf ambaye alikuwa na uzoefu wa muda mrefu, alishinda uchaguzi huo na kuwa Rais. Aliweka rekodi ya pekee kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke katika nchi hiyo na Afrika kwa ujumla.

Hata hivyo, Weah hakukata tamaa baada ya kushindwa. Aliendelea kufanya siasa na mwaka 2009 alirejea kutoka Marekani na kwenda kumfanyia kampeni mgombea wa nafasi ya useneta wa jimbo la Montserrado na akashinda.

Baadhi ya wachambuzi walisema hatua hiyo ya Weah ni maandalizi ya kugombea urais tena katika uchaguzi wa mwaka 2011.

Hata hivyo, chama cha CDC kilimchagua Weah kuwa mgombea mwenza wa urais wakati mgombea urais akiwa ni Winston Tubman.

Mwaka 2014, Weah aligombea nafasi ya useneta katika jimbo la Monteserrado na kufanikiwa kushinda kwa kishindo dhidi ya Robert Sirleaf ambaye ni mtoto wa Rais wa Liberia. Alishinda kwa asilimia 78 ya kura zote na kuwa mwanamichezo wa kwanza kuchaguliwa katika Bunge la Seneti la nchi hiyo.

Mwishoni mwa mwaka jana, Weah ameandika historia nyingine baada ya kushinda uchaguzi wa urais dhidi ya Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Joseph Boakai ambaye ameshika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 12 akiwa pamoja na Rais Ellen Sirleaf.

Weah ambaye ametangazwa rasmi kuwa mshindi wa kiti cha urais huko Liberia Desemba 28, 2017 kwa sasa anasubiri kuapishwa hapo kesho baada ya kuibuka kidedea katika majimbo 12 kati ya 15 nchini humo na kupata wastani wa asilimia 61.5 ya kura zote zilizopigwa katika duru ya pili ya uchaguzi huo.

Mara baada ya kutangazwa mshindi, Weah aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter; “Nawashukuru sana wananchi wa Liberia kwa kunichagua, tutakuwa pamoja katika mageuzi makubwa ya nchi hii.”

Kazi iliyo mbele yake

Weah baada ya kuapishwa hapo kesho, ana kazi kubwa ya kujenga uchumi wa Taifa hilo ambalo limedumu kwenye mapigano ya muda mrefu, jambo ambalo lilisababisha kusimama kwa shughuli za kiuchumi.

Uchumi wa Taifa hilo unategemea zaidi kilimo na biashara huku shughuli za utalii zikiathiriwa na sababu mbalimbali ikiwamo mlipuko wa ugonjwa wa ebola na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Katika kampeni zake, aliahidi kujenga uchumi wa nchi hiyo ili kuwasaidia vijana katika Taifa hilo ambao wengi wao hawana ajira.

Taifa hilo lenye idadi ya watu milioni nne (kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2016), lilikuwa na hali mbaya kiuchumi mwaka 2014/15 baada ya kuzuka kwa virusi vya ebola ambavyo viliziathiri pia nchi jirani za Sierra Leone na Guinea.

Tathmini ya Benki ya Dunia (WB) ya hali ya uchumi wa Liberia inaonyesha kwamba ugonjwa wa ebola ulisababisha kuporomoka kwa bei ya bidhaa nchini humo na uchumi wake ulitarajiwa kuimarika zaidi kutoka asilimia -1.6 mwaka 2016 mpaka 2.6 mwaka jana.

WB inafafanua kwamba kushuka kwa shughuli za kiuchumi zilisababisha matokeo mengi hasi ikiwamo kushuka kwa mapato ya Serikali, mfumuko wa bei na kuongezeka kwa umaskini miongoni mwa wananchi wa Liberia.

Tathmini hiyo inabainisha pia kwamba mfumuko wa bei wa Liberia uliongezeka kwa wastani wa asilimia 12.4 katika nusu ya pili ya mwaka jana ikilinganishwa na wastani wa asilimia 7.3 kwa mwaka 2016. Benki ya Dunia inabainisha kwamba mfumuko huo umetokana na kuporomoka kwa thamani ya Dola ya Liberia dhidi ya Dola ya Marekani, kupungua kwa fedha za kigeni nchini humo na uzalishaji mdogo wa bidhaa.

Matokeo yake, gharama za maisha zimepanda na wananchi wanashindwa kupata mahitaji na huduma muhimu kwa sababu wengi wao katika maeneo ya mijini na vijijini hawana ajira zinazowaingizia kipato.

Rais mteule, Weah ana kazi ya kuhakikisha maelfu ya vijana nchini humo wanapata ajira na uchumi wa Taifa hilo unaimarika tena na maisha ya wananchi ambao wamempigia kura yanakuwa bora.

Utendaji wake utapimwa kwa kuinua uchumi wa nchi hiyo na kuboresha maisha ya wananchi wake ambao wana imani naye. Alipata kura nyingi kutoka kwa vijana wengi kutokana na umaarufu wake na kundi hilo ndilo linalokabiliana na changamoto ya ajira.

Kiongozi huyo ana wajibu wa kujenga mazingira mazuri ya kazi ili kuwafanya vijana wa Taifa hilo waache kukimbilia nchi za Ulaya kutafuta ajira na maisha mazuri. Changamoto ya ajira itakuwa ni hatua muhimu ya awali itakayomwezesha kujenga uchumi wake.

Utawala wa Sirleaf umefanya kazi kwa sehemu yake lakini bado changamoto ni nyingi. Sasa ni wakati wa Weah kuja na fikra mpya, mbinu mpya na maarifa mapya ya kufufua uchumi wa Liberia ili uwe na ushindani.

0763891422