MAONI YA MHARIRI: Majimbo haya yakachukue madawati yao

Muktasari:

Jumla ya madawati 9,666 yametengenezwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutekeleza ahadi ya Rais John Magufuli kumaliza tatizo la madawati kwa shule za msingi nchini. Dk Mwinyi alitaja majimbo yaliyoshindwa kuchukua madawati hayo kuwa ni Kilindi, Pangani, Makambako, Ludewa, Wanging’ombe, Makete, Tunduru Kaskazini, Songwe, Ileje, Kyela, Rungwe, Busokelo, Kwela, Nkasi Kaskazini, Nkasi Kusini, Iringa Mjini, Mbeya Mjini na Mbeya Vijijini.

Ukurasa wa sita wa gazeti hili toleo la jana kulikuwa na habari iliyosomeka ‘Majimbo 18 ‘yasusa’ madawati ya Magufuli’. Ni taarifa ya kusikitisha ambayo ilitolewa kwenye vyombo vya habari na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi akiwakumbusha wahusika na kuwapa siku saba wawe wameyachukua madawati yao.

Jumla ya madawati 9,666 yametengenezwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutekeleza ahadi ya Rais John Magufuli kumaliza tatizo la madawati kwa shule za msingi nchini. Dk Mwinyi alitaja majimbo yaliyoshindwa kuchukua madawati hayo kuwa ni Kilindi, Pangani, Makambako, Ludewa, Wanging’ombe, Makete, Tunduru Kaskazini, Songwe, Ileje, Kyela, Rungwe, Busokelo, Kwela, Nkasi Kaskazini, Nkasi Kusini, Iringa Mjini, Mbeya Mjini na Mbeya Vijijini.

Dk Mwinyi amekuwa waziri tangu awamu ya tatu ya uongozi wa nchi, alitumikia awamu ya nne na sasa anaitumikia Awamu ya Tano, tangu awamu zote hizo hakuna mwenye shaka na utendaji wake wa kazi. Pia, si waziri mwenye kufanya kazi kwa kujikweza, hivyo kwa taarifa hii ni dhahiri amechoshwa na utendaji wa mwendo wa jongoo wa viongozi wa majimbo hayo.

Tunaamini hadi Dk Mwinyi ameamua kulisema hadharani ni wazi amekereka na namna wahusika wa madawati hayo wasivyo na nia njema ya kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kuboresha elimu nchini kwa kuhakikisha watoto wote wanakaa kwenye madawati na kutoa elimu bure.

Siku za nyuma tulisikia baadhi ya maeneo wamekataa kupokea madawati kwakuwa yalitengenezwa chini ya kiwango au kwa mbao zisizo bora, hao tunawapongeza kwakuwa wanatambua wajibu wao na umuhimu wa sera ya Serikali ya kutoa elimu bure na watoto kusoma kwenye mazingira bora.

Tunajua majimbo yote yaliyotajwa yana wabunge na madiwani waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, lakini kuna viongozi wa halmashauri, viongozi wa wilaya na viongozi wa mkoa, wote hawa tunashindwa kuelewa kama hawana taarifa za madawati yaliyotengenezwa na JKT.

Hata wale waliotoa sababu za kushindwa kuchukua madawati hayo baada ya kuulizwa na gazeti hili, tunajiuliza walishindwaje kumaliza kasoro hizo kwenye vikao vyao na kupata ufumbuzi wa haraka badala ya kusubiri kutoa kasoro hizo kwenye vyombo vya habari, tena walipotakiwa kueleza sababu za kutoyachukua.

Majimbo yaliyotajwa kuna yaliyo chini ya chama tawala na mengine ya upinzani, hivi vyama vyenye wabunge na madiwani kwenye majimbo hayo 18 hawana taarifa kuhusu madawati yaliyotengenezwa na JKT. Je, wanataka tuamini kwamba kuna maeneo viongozi hawapeani taarifa.

Ni imani yetu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwatumikia wananchi kwa dhati hasa wale wa kipato cha chini, lakini kinachoonekana kuna baadhi ya watendaji serikalini na hata kwenye vyama vya siasa hawako tayari kwenda na kasi ya Rais Magufuli.

Tunapenda kumtia moyo Rais Magufuli kwamba aendelee kupambana na wale wanaotaka kukwamisha juhudi zake za kuwatumikia Watanzania, pia tunaomba Serikali iwashughulikie wale ambao wanakuwa wazito kuonyesha moyo wa kujitolea katika kutekeleza majukumu yao.

Tunachosema hatukubaliani na viongozi au watendaji wenye tabia ya kujitetea kuliko moyo wa kujitolea, hawa tunaamini hawafai kuendelea kuwamo kwenye safari ya Rais Magufuli ya kuwaletea Watanzania maendeleo.