Masuala ya mjadala bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango

Muktasari:

Kati ya bajeti zinazojadiliwa ni ile ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Katika bajeti za wizara mbalimbali yapo mambo makuu ya kumjadala yanayotegemewa hasa yanayowagusa wadau wa bajeti kwa ujumla. Ni mambo ambayo wabunge wanategemewa kuyaibua na kujadili kupata muafaka kwa lengo la kuboresha mapendekezo ya bajeti ya waziri muhusika.

Kati ya bajeti zinazojadiliwa ni ile ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Mjadala wa bajeti unapokuwa bungeni huwa ni hatua baada ya maandalizi kadhaa. Kati ya maandalizi haya ni ukomo wa bajeti unaotolewa na Wizara ya Fedha. Ukomo huu huzingatia mambo kadhaa ikiwamo hali ya uchumi na mipango mipana ya nchi hasa ya mwaka wa fedha husika, utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha unaokwisha.

Ukomo huu ni muhimu kwa sababu mahitaji ni mengi kuliko uwezo wa kuyatimiza hivyo ni lazima kuweka kiwango cha juu cha fedha zinazowekwa katika wizara, idara na wakala mbalimbali.

Katika hali ya kuwa na mahitaji mengi kuliko uwezo, wapo ambao hawatakubaliana na ukomo wa bajeti katika sehemu zao. Mijadala katika hili huwa ni katika mambo kama vile uwezekano wa kuongeza kiasi cha fedha kilchotengwa katika sekta mbalimbali.

Bajeti

Kila wizara, idara na wakala wa serikali hupendekeza bajeti ambayo husomwa na waziri mwenye dhamana. Bajeti inayosomwa huwa ni jumla ya taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo.

Mapendekezo katika ngazi za awali huweza kuwa makubwa lakini hupunguzwa. Mjadala katika jambo hili huhusisha pamoja na mambo mengine, uhalisia wa bajeti inayopendekezwa kulingana na hali halisi uwandani. Mijadala huweza kuhusu utayari wa Wizara ya Fedha kuongeza kiasi cha fedha katika bajeti inayopendekezwa na wizara yoyote. Kama wabunge wakipinga kuwa bajeti ni kidogo sana kuliko mahitaji huweza kumtaka waziri wa husika kuiongeza.

Bajeti inapofika bungeni inakuwa imepitia Wizara ya Fedha kutii ukomo, marekebisho makubwa hayana budi kuihusisha wizara hiyo pia.

Bajeti inayopitishwa

Suala jingine la kimjadala katika bajeti za kisekta ni bajeti inayopitishwa ikilinganishwa na inayopendekezwa. Mara nyingi bajeti zikifikia ngazi ya kujadiliwa bungeni zinapitishwa kama zilivyoombwa.

Kuna uwezekano kuwa kabla ya ngazi hii bajeti zinazopitishwa ni kidogo kuliko zinazokuwa zimeombwa. Katika hali ya mambo kwenda kama yanavyotakiwa, bajeti inapaswa kuwa shirikishi ikiibuliwa kutoka ngazi za chini hadi Taifa. Hii hupaswa kufanywa kwa kutumia mbinu shirikishi za fursa na vikwazo vya maendeleo.

Matamanio ya wadau kutoka ngazi ya chini kama kijiji kwenda kata na halmashauri huwa ni mengi na makubwa. Lakini kwa sababu fedha za bajeti ni chache kuliko mahitaji bajeti inayopendekezwa kutoka ngazi moja kwenda nyingine huweza kuwa ndogo kuliko inayopitishwa.

Masuala ya mjadala ni pamoja na kwa nini mapendekezo kadha wa kadha yamekataliwa kwa mwaka wa fedha husika miaka iliyopita. Katika muktadha wa bajeti shirikishi, mijadala huweza kuhusu uhusiano kati ya bajeti pendekezwa na ile inayopitishwa. Suala kubwa ni pamoja na kujua kiasi cha bajeti inayopitishwa inaakisi matamanio na vionjo halisi vya wadau uwandani hasa ngazi ya vijiji. Kwa bajeti inayopitishwa kuakisi ile inayokuwa imependekezwa kwa sio rahisi.

Kwanza ni kwa sababu ya uhaba wa fedha na pili ni kwa bajeti kuweka ukomo na vipaumbele katika mazingira ambayo vipaumbele vinatakiwa kuibuliwa kwa mbinu za kutambua fursa na changamoto kutoka chini hadi juu na sio kinyume chake.\

Utoaji wa fedha

Pengine eneo la mjadala mkubwa kabisa katika bajeti ni hili linalohusu fedha zinazotoka kati ya zile zinazokuwa zimeidhinishwa na bunge. Kwa sababu mbalimbali na hasa ukosefu wa fedha na uwezo wa kufyonza fedha zinatotoka, kiasi cha fedha kinachotoka huweza kuwa kidogo kuliko kinachoidhinishwa.

Utafiti unaonyesha kuwa hii ni kweli zaidi kwa bajeti za maendeleo kuliko matumizi ya kawaida. Kumekuwapo nakisi kwa maana ya pengo kati ya kinachoidhinishwa na bunge na kile kinachotoka kutekeleza shughuli za maendeleo.

Pamoja na mambo mengine, hii ni kwa sababu ya kutopatikana fedha za kutosha hasa kutoka kwa wahisani na mikopo kama inavyokuwa imetarajiwa katika bajeti. Matokeo yake ni kutotekelezwa kwa bajeti kama ilivyopangwa.

Ni bahati nzuri kwamba kwa ujumla bajeti ya shughuli za kawaida hutoka kwa kiasi kikubwa kama inavyopangwa hivyo mijadala na ugomvi katika suala hili huwa ni katika bajeti ya maendeleo.

Katika mjadala wa fedha za bajeti zinazotoka, pia lipo suala la fedha kutoka kwa wakati na kwa kiasi kilichokubaliwa. Masuala ya mjadala katika hili hujikita katika fedha kutoka kidogo kuliko inayoidhinishwa na kutoka zikiwa zimechelewa.

Zinapotoka kidogo kuliko ilivyopangwa hufanya bajeti isitekelezeke vizuri. Inapotoka ikiwa imechelewa huweza kusababisha matatizo ya utawala bora kwa maana ya kutumia fedha ziishe kabla ya mwaka wa fedha badala ya kutumia kwa namna zilivyopangwa.

Matumizi

Namna fedha zinazotoka zinavyotumika huwa ni mjadala mkubwa katika kila bajeti ya wizara. Hii ni muhimu sana katika muktadha mpana wa nidhamu katika matumizi ya umma.

Fedha za bajeti zikipangwa na kutoka zote halafu zikatumiwa vibaya malengo ya bajeti hayatatimia. Mjadala katika suala hili huhusu ubadhirifu wa fedha za umma.

Jambo ambalo pengine halijadiliwi sawa ni kushidwa kwa baadhi ya taasisi kutumia fedha zinazopewa. Matokeo yake ni fedha hizi kurudi hazina waakati malengo ya kuzitumia hayajatekelezwa. Japokuwa inaweza kuwa sio shida kubwa sana, bado ni eneo la mjadala wa kina pia.