MAONI YA MHARIRI: Matamko yanayoathiri elimu yapitiwe upya

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa

Muktasari:

Wakiwa bungeni au kwenye mikutano ya hadhara viongozi wetu husema elimu yetu iko juu na hutoa orodha ya Watanzania walioko kwenye mashirika ya kimataifa. Lakini wakishuka kwenye majukwaa huanza kufumua mfumo wa elimu kwa lengo la kubadilisha mfumo wa awamu iliyopita.

Swali gumu ambalo limekuwa likiwatesa viongozi wetu ni kutoa majibu kuhusu mfumo na mwelekeo wa elimu nchini. Majibu yao hutofautiana na vitendo vyao.

Wakiwa bungeni au kwenye mikutano ya hadhara viongozi wetu husema elimu yetu iko juu na hutoa orodha ya Watanzania walioko kwenye mashirika ya kimataifa. Lakini wakishuka kwenye majukwaa huanza kufumua mfumo wa elimu kwa lengo la kubadilisha mfumo wa awamu iliyopita.

Mabadiliko mengine hufanywa kwa maagizo tu na waziri bila wadau wa elimu kuitwa na kukaa katika meza ya majadiliano ili kupitia changamoto zilizopo kuzipatia ufumbuzi au majibu. Matokeo yake ni kwamba mabadiliko mapya hupingwa kuanzia yanapotangazwa kwa sababu huwa hayana tija.

Hali hiyo imempa hofu Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye ameonya kuwa maagizo na amri za viongozi zinazotolewa bila ya kuwa na majadiliano, zitaitumbukiza shimoni elimu ya Tanzania. Mkapa, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, amesema idadi ya wanachuo wanaodahiliwa vyuo vikuu nchini, lazima iendane na ubora wa miundombinu pamoja na bajeti ya Serikali badala ya kujaza wanafunzi wakati hakuna fedha za kutosha na hivyo kuwa mzigo.

“Amini nawaambia, maagizo peke yake hayaondoi matatizo tuliyonayo ndani ya elimu, bali niwaombe wadau pamoja na wizara husika kuwa wakae meza ya mazungumzo ili wazijadili changamoto hizo,” alisema Mkapa wakati wa mahafali ya saba ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Mkapa ameshauri kuwa njia bora ya kuboresha elimu nchini ni kwa wadau kukutana katika meza ya mazungumzo ili wajadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kueleza nini kinatakiwa.

Pia, alisema kama maagizo yataendelea bila ya kuwepo na majadiliano elimu ya Tanzania itakuwa imewekwa rehani na kwamba katika kipindi cha miaka michache nchi haitakuwa kwenye ubora wa elimu kama ambavyo wengi wanadhania.

Tunampongeza Mkapa kwa kuiona dosari hiyo na kwa kutoa ushauri maana ni kweli katika miaka ya hivi karibuni yametolewa matamko yanayotia shaka kama kuna nia njema na mfumo wa elimu.

Mfano, wakati katika awamu yake aliwapa fursa wadau ya kujadili na kupitia upya mfumo wa elimu ambao walifikia uamuzi wa kufanyia mabadiliko masomo ya sayansi na biashara, awamu iliyofuata ilitoa tamko tu kurejesha mfumo wa zamani.

Halafu baadhi ya shule za sekondari na vyuo vya kati ambavyo vilikuwa vikitoa elimu ngazi ya cheti na diploma vilibadilishwa kuwa vyuo vikuu bila kuwepo mbadala.

Pia, katika miaka ya hivi karibuni viongozi wenye dhamana na elimu wamekuwa wakihaha kubadili mfumo wa ukokotoaji na upangaji matokeo; mara yaliongezwa madaraja ya ufaulu, mara mfumo wa upangaji kwa divisheni uliondolewa ukaingizwa mfumo wa GPA kwa shule za sekondari. Matamko mengine yaliathiri ubora na umuhimu wa mitihani ya darasa la IV na kidato cha II.

Kwa matamko tu mfumo wa kuwapata wanafunzi wa elimu ya juu wanaostahili kupewa mikopo ulifutwa; kigezo cha masomo ya sayansi na elimu kikaondolewa, kikaingizwa kigezo cha uyatima na umasikini.

Wanafunzi waliokuwa wakisoma kozi maalum ya ualimu wa sayansi wakaondolewa na vyuo binafsi vya elimu ya juu vimelalamikia kutopangiwa wanafunzi. Viongozi wetu wajiulize wanajenga au wanabomoa?