MAONI YA MHARIRI: Matokeo haya ni aibu kwa Sekondari ya Azania

Muktasari:

Sura ya kwanza ni kile kinachoonekana kama shule za Serikali hasa zile za vipaji maalumu kurudi kwenye makali yake ya ufaulu.

Julai 15, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), lilitoa matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha sita, yaliyoteka hisia za watu wengi kwa sura kuu mbili.

Sura ya kwanza ni kile kinachoonekana kama shule za Serikali hasa zile za vipaji maalumu kurudi kwenye makali yake ya ufaulu.

Katika matokeo hayo, shule za wanafunzi wa vipaji maalumu nne na moja ya kawaida, zilitajwa kuwa katika orodha ya shule bora 10 kitaifa.

Ni matokeo yaliyoleta ahueni kwani kwa miaka kadhaa shule hizo zilishindwa kufurukuta dhidi ya shule binafsi.

Kingine kilichoteka hisia za wengi ni kuanguka kwa shule kongwe ya Azania. Kwa mara ya kwanza shule hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam imeingia katika orodha ya shule 10 zilizofanya vibaya kwenye mtihani wa kidato cha sita.

Katika matokeo hayo, wahitimu 29 walipata daraja sifuri, huku 11 wakipata daraja la kwanza. Waliopata daraja la pili ni wanafunzi 33, la tatu 115, na la nne wanafunzi 36.

Matokeo ya Azania yamewaacha midomo wazi watu wengi, si kwa sababu ya umaarufu unaotokana na ukongwe wake, lakini kutokana na ukweli kuwa shule hiyo iko mjini kunapopatikana kila aina ya rasilimali inayohitajika kwa ajili ya utoaji wa taaluma bora.

Nasi tumo kwenye kundi hilo la watu wanaomini kuwa kwa vigezo vyovyote vile shule hiyo haikupaswa kufanya vibaya kwa kiwango cha kuwa katika orodha ya shule zilizoshika mkia.

Tunajiuliza ikiwa shule iliyo ndani ya jiji kuu la nchi na yenye hadhi kihistoria inaachwa kuwa na matokeo mabaya kama haya, hali ikoje kwa shule za pembezoni mwa nchi?

Aidha, uzoefu unaonyesha siku zote matokeo yanapokuwa mabaya katika shule hizi, wa mwanzo kutupiwa mzigo wa lawama ni walimu.

Kwa mfano tunakumbuka mwaka 2014 kiongozi mmoja wa juu serikalini alipohoji shule kama Iyunga iliyopo mkoani Mbeya kufanya vibaya katika mtihani wa kidato cha sita huku ikiwa na walimu wasiopungua 70.

Alichoshindwa kuelewa ni kuwa kuwapo kwa walimu ni jambo moja, lakini kuna vitu vingi vya kuzingatia katika utoaji wa taaluma bora shuleni.

Ni kwa sababu hii hata uongozi wa Azania ulipozungumza na gazeti hili wiki iliyopita ulishangazwa na matokeo licha ya kuwa walimu ni walewale waliokuwapo miaka ya nyuma shule ilipokuwa ikifanya vizuri.

Rai yetu ni kuwa wakati Serikali ikijitahidi kuajiri walimu wengi na kuwapangia vituo, ihakikishe pia kunakuwapo mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia ili isiwe sababu ya walimu kukata tamaa kama inavyojidhihirisha katika shule nyingi ambazo zina walimu wa kutosha, lakini ufaulu wake si wa kuridhisha.

Kero kama uhaba wa nyumba za kuishi, miundombinu duni kama vyoo, maslahi na kuthaminiwa hazina budi kuwa kipaumbele katika harakati za kurudisha heshima ya shule za Serikali.

Kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoanza na kasi ya kurudisha heshima katika utendaji serikalini, kasi hiyo ijidhihirishe kwenye vyombo vyake mbalimbali zikiwamo taasisi za elimu.

Ufaulu wa shule za vipaji maalumu katika matokeo ya mwaka huu, utumike kama chachu ya kuisukuma Serikali kubadili hali ya mambo katika shule zake ili hatimaye ziwe kimbilio na tumaini la walio wengi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.