UCHAMBUZI: Matumizi bora ya likizo kwa wanafunzi

Muktasari:

Likizo hii yafaa itumiwe vizuri na wanafunzi kujiandaa na mwaka mpya wa masomo ifikapo mwakani.

Huu ni mwezi wa Novemba na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanakaribia kufunga shule na kuanza likizo ndefu ya mwisho wa mwaka.

Likizo hii yafaa itumiwe vizuri na wanafunzi kujiandaa na mwaka mpya wa masomo ifikapo mwakani.

Wako wazazi wanaopendelea kuwapa watoto kazi za kufanya kama vile kulima, kuhudumia mifugo, kufanya shughuli ndogo ndogo na hata biashara ili kuongeza kipato katika familia.

Kuna baadhi ya watoto wanaotumia muda wao kuangalia kanda za video au vipindi katika runinga. Wakati mwingine vipindi hivi ni vya burudani kama vichekesho, mchezo wa mpira wa miguu na kadhalika.

Kuna wakati watoto wanaangalia picha mbalimbali baadhi zikiwa za mapenzi na ngono, jambo ambalo linawakwaza na kuwavuruga kimaadili.

Ukiwa ni mzazi makini nakushauri uwe unasimamia na kufuatilia kile ambacho watoto wanaangalia kwenye video au runinga. Wasiachiwe kuangalia kila wanachotaka kuona.

Shughuli nyingine ambazo wazazi wanapenda watoto wao wafanye wakati wa likizo ni kuwatembelea ndugu na jamaa wanaoishia sehemu mbalimbali za nchi. Hii ni jambo zuri lakini kuwe na ukomo na udhibiti wa aina fulani, kwani wako baadhi ya ndugu au jamaa hawako makini kufuatilia nyendo za watoto wao.

Ni dhahiri kuwa kipindi cha mapumziko kiwe na mpangilio utakaowafaa wanafunzi kuendelea kumaliza mafunzo yao kwa ukamilifu.

Si busara kumfanya mwanafunzi aliyekaa darasani kwa kipindi kirefu wakati wa mafunzo endelee tena na mfumo huohuo wa kusoma kwa mtindo wa twisheni. Wanatakiwa wapumzike na wabadilishe mtindo wa maisha.

Baada ya shughuli hizo za kitaaluma, inashauriwa kuwapangia watoto muda wa kujisomea kwa mfumo tofauti, Je, unafahamu kuwa kutembelea asasi au taasisi za kitaaluma ni njia mojawapo ya kuwaongezea watoto wako maarifa?

Asasi mojawapo inayofaa kutembelewa ni maktaba. Maktaba zimejengwa karibu kila mkoa. Kwa wale wanaoishi mijini wajaribu mtindo huu. Wale wanaoishi jijini Dar es Salaam au vitongoji vinavyozunguka jiji hili, kuna Maktaba Kuu ya Taifa.

Hapa kuna sehemu ya vitabu vya kujisomea kwa watoto, sehemu ya kufanyia mazoezi ya darasani, sehemu ya kuangalia katuni, kanda za video zenye mada za kitaaluma.

Watoto wakiwa na mazoea ya kutembelea maktaba watajenga tabia ya kujisomea wenyewe mapema na hii itawafanya wawe na utamaduni wa kupenda kusoma.

Hatua hii pia itajenga mwelekeo wa watu kupenda kusoma na itaondoa udhaifu uliopo kwa baadhi ya wasomi wengi wasiopenda kusoma baada ya kuhitimu masomo yao.

Mzazi mwenye busara anashauriwa kuwapa watoto wake nafasi ya kujisomea kwa mfumo maalumu wa twisheni. Kwa mfano wazazi wachague walimu wa kuwafundisha watoto wenye udhaifu katika mada ambazo wanadhani watoto wao wanatakiwa kufuata.

Mfano wa twisheni hizi unaweza kuwa katika kukazia taaluma ya kujifunza lugha, sayansi au hisabati. Hakikisha kuwa kama mzazi makini unapaswa kutembelea sehemu anakosoma mwanao ili ujue mazingira ya darasa, vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Vilevile chunguza uwezo wa kitaaluma wa walimu wanaofundisha kwani wako walimu wanaojidai kufundisha lakini hawana taaluma ya ualimu.

Kwa mfano, vijana wengi waliofeli mitihani yao ya kidato cha nne au cha sita hujitokeza kufundisha kwa minajili ya kujipatia kipato, licha ya ukweli kuwa hawana sifa za ualimu.