MAONI YA MHARIRI: Matumizi ya Kiswahili EAC ni uamuzi mzuri uliochelewa

Muktasari:

Umoja wa Afrika (AU) kwa muda mrefu umekitambua Kiswahili kuwa ni miongoni mwa lugha rasmi zinazozungumzwa ama katika mikutano au kwa mtangamano ndani ya jumuiya hiyo. Lugha nyingine zilizoidhinishwa ni Kiarabu, Kifaransa, Kihispania, Kiingereza na Kireno.

Ni uamuzi mzuri lakini uliochelewa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwa ndiyo kwanza Bunge la nchi hizo linapitisha azimio la kuitumia lugha ya Kiswahili.

Umoja wa Afrika (AU) kwa muda mrefu umekitambua Kiswahili kuwa ni miongoni mwa lugha rasmi zinazozungumzwa ama katika mikutano au kwa mtangamano ndani ya jumuiya hiyo. Lugha nyingine zilizoidhinishwa ni Kiarabu, Kifaransa, Kihispania, Kiingereza na Kireno.

Pamoja na kuchelewa huko, hii ni hatua ambayo Watanzania tunapaswa kujivunia kwa sababu Kiswahili ni lugha yao ndiyo iliyotambulika rasmi katika majumui za Afrika. Sasa ni wakati wa kukipaisha Kiswahili kiwe ni lugha inayopendwa kuzungumzwa duniani kote na katika duru zote. Lakini wakati kikipata hadhi hiyo, wenye Kiswahili wenyewe hatukithamini. Makosa mengi yanafanywa katika uzungumzaji wa lugha hiyo na hata wakati wa kuandika.

Watanzania tulipaswa kuwa ndiyo wazungumzaji na walimu wazuri wa lugha hiii kwa sababu sisi ndiyo wenye lugha. Pamoja na kuwa Tanzania kuna makabila zaidi ya 120 na lugha kwa idadi hiyohiyo, lakini zaidi ya asilimia 90 wanazungumza Kiswahili na wengi wao hawazijui hata lugha za makabila yao, hasa vijana waliozaliwa mijini.

Ingawa Watanzania tunajinasibu kwa Kiswahili, inashangaza kuwa fursa zitokanazo na lugha hii hatuzitumii. Mathalan, zinatoka nafasi kadhaa za kufundisha Kiswahili katika vyuo vikuu vya kimataifa, Watanzania hatuziombi. Zinatoka nafasi mbalimbali za kutangaza katika idhaa za Kiswahili duniani, Watanzania tupo kimya tunazifumbia macho. Fursa hizo nyingi huchukuliwa na watu wa nchi nyingine ambao wengi wao wamejifunza Kiswahili vyuoni wakati sisi tulikizungumza mara tu tulipoacha kunyonya, tunakichukulia kama kitu cha kawaida.

Tatizo la letu ni kujibweteka kwa kudhani kuwa tunakijua Kiswahili ndiyo maana tunanyamaza kimya wakati lugha hii adhimu ikivurundwa na kubanangwa kwa kufahamu au bila kutambua.

Leo hii Watanzania hatutaki kujifunza Kiswahili kwa kudhani tu kuwa tunakijua, kumbe ukweli ni kwamba tulio wengi hatukijui na tumeruhusu kutawaliwa na matamshi yenye athari za lugha zetu mama. Mathalani, asiyeweza kutoutisha herufi L na R wala hafanyi jitihada za kujifunza kutamka vyema.

Aidha, huu sasa ni wakati wa taasisi zinazoshughulikia makuzi na matumizi ya Kiswahili nchini kama vile Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita), Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza), Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (Tuki) na nyinginezo kukaza mkanda, kukishughulikia Kiswahili kwa mapana na marefu, kuboresha kamusi na kufanya utafiti wa lahaja na maneno mapya yanayoingia katika lugha.

Tatizo linalotajwa kila mara panapohitajika kuendeleza jambo la muhimu kwamba kuna upungufu wa fedha (linalojulikana kama ukata), sasa wakati umefika wa kutafuta mbinu za kukabiliana nalo ili tukipe hadhi Kiswahili, tuhakikishe kwamba ndiyo lugha iliyotamalaki siyo tu Afrika Mashariki na Afrika nzima, bali duniani kote. Penye nia ipo njia. Tusisubiri Wakenya, Wanyarwanda, Warundi, Wakongo au wengineo wakithamini na kukikuza Kiswahili, Watanzania tunapaswa tujivunie lugha yetu.

Ni wakati wa kujifunza lugha nyingine kwa dhamira ya kuweza kukitarjumi (kukitafsiri kwa wasiojua Kiswahili). Tujifunze ukalimani wa Kiswahili, hii itatusaidia pia kupata ajira nje. Kadhalika, tuwashauri viongozi wetu watumie Kiswahili katika mikutano ya kimataifa ili wengi zaidi waisikie ladha ya lugha hiyo na watamani kuizungumza.