Matumizi ya takwimu yatapunguza migogoro na kuchochea maendeleo

Muktasari:

 

  • Takwimu zenye ubora zina sifa kadhaa ikiwamo kuwa mahsusi (specific), zinazopimika (measurable), zinazofikika (attainable), zenye uhalisia (realistic) na zenye muda maalumu (time bound).
  • Pia, takwimu zenye ubora zinatakiwa ziwe zimekusanywa na mtaalamu au wataalamu wenye sifa na vigezo vinavyotambulika kitaifa na kimataifa. Baada ya kukusanywa lazima zipitiwe ili kuondoa makosa ya kibinadamu, zichanganuliwe na zitafsiriwe katika lugha rahisi kueleweka na watu wote.

Kupanga ni kuchagua, bila takwimu zenye ubora hakuna namna unaweza kupanga. Uamuzi usiotokana na takwimu sahihi hauwi bora na wenye manufaa kwa anaoufanya au wanaonufaika nao.

Takwimu zenye ubora zina sifa kadhaa ikiwamo kuwa mahsusi (specific), zinazopimika (measurable), zinazofikika (attainable), zenye uhalisia (realistic) na zenye muda maalumu (time bound).

Pia, takwimu zenye ubora zinatakiwa ziwe zimekusanywa na mtaalamu au wataalamu wenye sifa na vigezo vinavyotambulika kitaifa na kimataifa. Baada ya kukusanywa lazima zipitiwe ili kuondoa makosa ya kibinadamu, zichanganuliwe na zitafsiriwe katika lugha rahisi kueleweka na watu wote.

Bila takwimu zenye ubora, huwezi kupanga mipango ya maendeleo yenye tija kwa taifa. Matumizi sahihi ya takwimu zenye ubora huondoa malalamiko katika jamii kuhusu mgawanyo wa rasilimali ikiwamo fedha, watumishi na vifaa.

Kwa mfano, kwa kutumia takwimu Serikali inaweza kujenga hoja ya kwa nini imeamua kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ikiwamo ujenzi wa barabara, ununuzi wa ndege na utengenezaji madawati badala ya kuzielekeza nguvu hizo kwenye huduma za afya, maji au kilimo.

Matumizi sahihi ya takwimu zenye ubora, hupunguza maswali na kutoa majawabu yenye ushahidi wa kisayansi ambayo kila mwenye hoja kinzani anatakiwa kujipanga kabla hajaongea hadharani na kupendekeza tofauti na ilivyoamriwa.

Maandalizi ya kujadili na kupitisha mpango na bajeti ya Serikali, lazima uzingatie na kuungwa mkono na takwimu zenye ubora za mwenendo wa uchumi kwa kuzingatia utendaji wa kila sekta kwa miaka iliyopita na kinachohitajika sasa.

Kwa kuzingatia vipaumbele vilivyopo, takwimu zinatakiwa zielekeze sekta ipi itengewe kiwango gani cha fedha na mahitaji mengine, siyo kwa kuzingatia matakwa ya mtu au kikundi cha watu waliopewa dhamana ya kuwasilisha mapendekezo hayo.

Takwimu zenye ubora ni kioo kinachoonyesha uhalisia wa jambo bila kupendelea. Zinabainisha ukuaji, kudumaa na kurudi nyuma katika utekelezaji wa kila sekta, idara au taasisi ya umma.

Kujua ukubwa au udogo wa tatizo na nguvu zinazohitajika kuwekezwa ili kulitatua, lazima utumie tawimu zenye ubora. Kwa mfano; kama kuna shule mbili zenye mahitaji sawa, huwezi kuwapanga walimu 10 kwenye shule moja na kuwapeleka wanne kwenye inayobaki.

Lakini, kama hakuna au mwenye dhamana ameamua kutozitumia au hajui namna ya kuzitumia takwimu zilizopo, zenye ubora unaohitajika, hili linaweza kutokea na kuleta malalamiko kutoka kwa wananchi na walimu wenyewe kwa sababu baadhi watakuwa wanafanya kazi kubwa kuliko wengine.

Kuwa na takwimu zenye ubora inawezekana. Inahitaji utashi wa kisiasa na kuwekeza kwenye rasilimali ikiwamo watu, fedha na vifaa ili zitumike kwa namna ambayo italeta manufaa kwa wananchi wa kila wilaya au mkoa nchini.

Pia, lazima pawepo na uelewa sawa kuanzia mifumo ya ukusanyaji takwimu hadi usambazaji kati ya watakwimu waliopo katika taasisi mbalimbali za umma, binafsi na watumiaji hasa watunga sera au wanaopanga mikakati ya idara.

Baada ya Chama cha Watakwimu (Stata) kushindwa kuwaunganisha wanachama wake ni vyema kikaanzishwa chombo ambacho kitakuwa kinasimamia taaluma na weledi wa watakwimu nchini kama ilivyo Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), au Bodi ya Wafamasia.

Sasa hivi watakwimu wamegawanyika katika makundi makuu matatu, kuna watakwimu wa NBS, wa Serikali za Mitaa (Tamisemi) na sekta binafsi. Hawa wote wanahitaji chombo cha kuwaunganisha ili wawe na misingi ya pamoja juu ya takwimu.

Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 inazitambua zaidi zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), taasisi na idara za Serikali, taasisi binafsi au mtu binafsi ili mradi zikidhi vigezo vilivyowekwa.

Mipango bila kutumia takwimu zenye ubora ni kupoteza rasilimali ikiwamo muda, fedha au nguvu kazi. Tuwekeze kwenye takwimu na tafiti kwa ajili ya mipango itakayokuwa na tija wakati wote kwa wananchi wanaozitumia.

Hili likifanywa kwa umakini unaohitajika siyo tu litachochea maendeleo ya nchi, bali litapunguza malalamiko ya wananchi juu ya masuala mbalimbali.

Vilevile, migogoro ya kijamii mfano baina ya wakulima na wafugaji iliyopo kwenye mikoa tofauti nchini.

Sio hao peke yao, halmashauri au mamlaka zilizopo nazo zitaondokana na vikwazo vinavyokwamisha utekelezaji wa miradi au mgawanyo wa rasilimali kutokana na sababu ambazo zingetatuliwa kwa takwimu sahihi.

Takwimu hizi ni muhimu pia kuondoa manung’uniko ya watumishi wa umma waliopo kwenye ofisi tofauti ambao wanaamini kuna mambo hayaendi kama yalivyotarajiwa.