Mbinu za kuhusianisha masomo na kazi uipendayo

Muktasari:

  • Mambo haya yalikuwa, mosi, unataka kufanya nini kwa siku za mbele? Pili, uwezo wako uko kwenye eneo lipi?

Katika makala yaliyopita tulijifunza mambo kadhaa yanayoweza kuwa msaada unapofikiria ukasome nini kwa masomo ya kidato cha tano.

Mambo haya yalikuwa, mosi, unataka kufanya nini kwa siku za mbele? Pili, uwezo wako uko kwenye eneo lipi?

Ingawa maswali haya yanaweza kuonekana kuwa ni mepesi, mara nyingi yanahitaji msaada wa karibu kuyajibu kwa ufasaha kulingana na mazingira uliyonayo.

Wakati mwingine kile unachokiweza sicho unachotaka kukifanya na sicho unachojitambulisha nacho.

Mathalani, unaweza kucheza mpira wa kikapu. Muda wako wa ziada unapenda kuutumia kucheza mpira wa kikapu. Lakini unapotafakari kile unachotaka kukifanya kwa siku za mbele, hujioni ukicheza mpira wa kikapu ingawa unaona fahari kuwa mchezaji wa mpira wa kikapu.

Hapa kuna mawili. Inawezekana huna uhakika na kile unachokipenda kwa dhati au pengine umeathirika na matarajio ya jamii.

Wakati mwingine unaweza kumezwa na kile unachoamini kinahitajika kiasi kwamba unapuuzia kile ulichonacho ndani yako.

Lakini pia wapo wengine wanaomezwa na mwelekeo au mtazamo wa walio wengi. Hawa ni wale wanaosoma fani fulani kwa kuwa ndiyo inayokimbiliwa na watu wengi.

Wakati nasoma, nilikuwa mchoraji maarufu. Lakini nilipokuwa nikitafakari nikasome nini baadaye fani ya uchoraji haikuwa inanijia kichwani.

Maana yake ni kwamba wakati mwingine kuna vitu unaweza kuwa unavipenda lakini visitoshe kuwa utambulisho wako. Ndio maana unahitaji kutafakari swali la nne ambalo ni:

Mahitaji ya soko la ajira

Kisaikolojia mafanikio ya mtu kazini yanategemea namna anavyoweza kuhusianisha wito alionao ndani yake na mahitaji halisi katika jamii anamoishi.

Kwa msingi huo, wanasihi wa masuala ya kazi husisitiza mtu kuanzia ndani yake kwanza atambue kwa hakika yeye ni nani kabla hajatoka nje kuona nini kinahitajika na jamii.

Faida mojawapo ya kujitambua nini unacho ndani yako, ni kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kubadilisha mazingira yako bila kutegemea mwelekeo wa hali nyingine usizo na uwezo nazo.

Chukulia mtu aliyesomea teknolojia ya mawasiliano kwa sababu hicho ndicho anachokiweza na kukipenda.

Mtu huyu hahitaji kuajiriwa kama mhandisi ili aendeshe maisha yake. Ile tu kusoma kitu kilichoanzia ndani yake, anajiweka kwenye nafasi kubwa ya kuwa mbunifu na kujiajiri kuliko mwenzake aliyesomea kitukile kile lakini kwa kutumia kigezo cha soko la ajira.

Ukifuatilia historia ya watu wengi wenye mafanikio makubwa, unaweza kuona mara nyingi wanakuwa ni wale waliosomea mambo yaliyoanzia ndani yao na wakatengeneza mfumo wa kutatua changamoto zilizopo katika jamii. Hawa ndio wajasiriamali wakubwa.

Hata hivyo, si kila mmoja anaweza kufanikiwa kwa njia hii kwa sababu mara nyingi utalazimika kujiajiri.

Ndio maana tunasema kulingana na malengo uliyonayo, ni vyema kufikiri namna unavyoweza kusoma kitu kinachohitajika kwenye jamii ili umuhimu wako uonekane kirahisi baada ya masomo yako.

Kama unalenga kujiajiri, somea fani zinazokujengea ujuzi wa moja kwa moja wa kufanya vitu kulingana na eneo lako la utaalamu.

Epuka kusoma fani zinazokupa uelewa wa jumla tu usioweza kuutumia kutatua changamoto halisi.

Pia, kama unahitaji kuajiriwa epuka kusoma vitu kwa sababu tu unavipenda, lakini baadaye visiongeze thamani yako kwenye soko la ajira. Hapa nazungumzia umuhimu wa kujua mahitaji ya soko la ajira.

Katika hicho unachotamani ukakisomee siku moja, fikiria namna kitakavyokuwezesha kuongeza ushindani wako kwenye soko la ajira.

Fikiria idadi ya watu waliosomea fani hiyo na linganisha na nafasi za kazi zilizopo.

Nikupe mfano. Inawezekana unapenda falsafa. Jiulize, watu wangapi huajiriwa moja kwa moja kama wanafalsafa? Kama unataka kusomea sayansi ya siasa, jiulize, kuna idadi gani ya watu waliosomea sayansi ya siasa na uhusiano wa kimataifa ukilinganisha na nafasi zilizopo? Je, unaweza kujiajiri kwa kusomea sayansi ya siasa?

Pamoja na hayo, unapofikiria soko la ajira, ni muhimu kuwa mwangalifu. Soko la ajira lina tabia ya kubadilika kulingana na mahitaji ya jamii.

Kinachohitajika leo, kinaweza kisihitajike kesho.

Husianisha masomo yako na kazi

Mpaka hapo nimekupa maelezo ya jumla yanayokusaidia kubaini unataka kufanya nini.

Naelewa si kazi nyepesi ndio maana tunashauri uwasiliane na mnasihi wa masuala ya kazi akusaidie kukupa taarifa zinazolingana na mazingira yako.

Baada ya kujua unataka kufanya nini hatua inayofuata ni kuhusianisha kazi uitakayo na masomo utakayochagua.

Kama kwa mfano, umeamua kwenda kwenye fani za afya, yaani udaktari, uuguzi, ufamasia, maabara, basi unahitaji kupitia njia ya Fizikia, Biolojia na Kemia (PCB) kwa kidato cha tano na sita.

Jiografia ikiambatana na masomo ya Biolojia na Kemia (CBG), uelekeo wako unakuwa kwenye misitu, hifadhi za wanyama, sayansi kilimo, masuala ya chakula na fani zinazofanana na hizo.

Ikiwa unataka kufanya kazi za uhandisi wa mitambo, ujenzi, kompyuta, umeme na teknolojia za aina mbalimbali, angalia uwezekano wa kusoma masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM).

Ukiweka Jiografia kwenye Fizikia na Hisabati (PGM) uelekeo wako unakuwa kwenye fani za ubunifu wa majengo, sayansi za miamba na urubani ingawa pia bado unakuwa na nafasi ya kufanya fani zinazohusiana na teknolojia.

Inawezekana pia umebaini uelekeo wako ni stadi za jamii. Kwa mfano, kama unalenga kuwa mwandishi wa habari, mwanasheria, mtaalamu wa maendeleo ya jamii, lugha, ni vyema ukasoma masomo ya Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Historia, Jiografia (HGL, HKL, KLF).

Lakini ukisoma somo la Uchumi katika hayo, au yale ya sayansi, yaani HGE, EGM, uelekeo wako ni kuwa mchumi, utawala wa biashara, mhasibu na fani nyingine kwenye sekta ya fedha.

Jambo la kuzingatia ni kwamba zipo fani ambazo wakati mwingine hazitegemei moja kwa moja ulisoma masomo gani kwa kidato cha tano na sita.

Mfano ni ualimu, jeshini, ofisa wa benki, usimamizi wa biashara, uchumi na stadi nyingine za maendeleo ya jamii. Itaendelea