JICHO LA MWALIMU : Mbinu za kumjenga mtoto kujiamini

Muktasari:

  • Staha huanzia utotoni na madhara yanayotokana na malezi ya mtu katika staha (kujiamini) huwa hayaishi. Hupungua tu kwa msaada wa wataalamu wa ushauri wa masuala ya saikolojia

Kujiamini (staha) ni jinsi vile mtu anavyojiona na kujichukulia yeye mwenyewe.
Ukiona mtu ni mbishi, hashauriki, yeye ndiye yeye kila kitu anajua na anafikiri huwa hakosei, hayo ni matokeo ya malezi na makuzi, mazingira na jamii aliyokulia.
Staha huanzia utotoni na madhara yanayotokana na malezi ya mtu katika staha (kujiamini) huwa hayaishi. Hupungua tu kwa msaada wa wataalamu wa ushauri wa masuala ya saikolojia.
Ni vema  watu wakafahamu mambo ambayo huchangia mtu kujiamini. Hii ni kwa sababu, kujiamini hakujitokezi ukubwani  kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya mambo yaliyofanyika utotoni.
Kwa muktadha huo, walimu na wazazi wana nafasi kubwa  ya kuwasaidia watoto na wanafunzi kujenga staha.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa makala haya, kuna makundi matatu ya staha au kujiamini: kundi la watu wenye staha ya juu, wenye staha ya chini na wenye staha ya juu iliyopitiza  Staha ya juu, malezi na tabia zake
Mtu mwenye staha ya juu (high self-esteem) hujipenda na kujikubali kwa jinsi alivyo. Hujiamini na kujithamini; na yuko tayari kuanzisha jambo jipya lenye faida. Baadhi ya tabia za watu wenye staha ya juu ni hizi zifuatazo:
Kwa asilia ni viongozi; hujithamini na kujikubali katika hali zote; hawaishi maisha ya kuigiza; huwa na furaha kwa jinsi walivyo; hufurahi wanapoona wengine nao wakifurahi; ni wabunifu na wanaothubutu kuvumbua mambo na vitu.
Hupenda kazi, hawaziogopi na wako tayari kuwajibika kutokana na matendo yao; hutambua nafasi yao katika jamii na wamekuwa wakitetea nafasi zao na huwa hawapendi kunyanyaswa wala kudhalilishwa.
Pia, hujitambua maeneo waliyo na uwezo nayo na yale wasiyo na uwezo wa kuyafanya vizuri; hujitambua wanapofanya makosa; hujitambua vipawa vyao na wanajitahidi kupunguza  upungufu wao.
Huwa hawapendi watu wanapowasifia sifia  juu ya uwezo au vipawa walivyonavyo; huwa wana mpangilio katika shughuli zao; hufanya jitihada ili kufikia ndoto zao; huuliza kama hawaelewi au kama hawafahamu jambo; hushiriki katika matukio na shughuli mbalimbali za kijamii na hutoa misaada na kuomba msaada wanapohitaji.
Malezi yanayosababisha mtu kuwa na staha ya juu
Mtu ambaye leo hii huonekana akiwa na staha za juu (anajiamini), wakati wa utoto wake alilelewa katika mazingira ya nyumbani au shuleni kama haya yafuatayo:-
Alilelewa kwa upendo; alipewa sauti, uhuru wa kutoa maoni yake; alifundishwa nidhamu, utii na kuwaheshimu wengine. Alifundishwa jinsi ya kuweka malengo, alipatiwa lishe bora nyumbani pia shuleni na chanjo zinazostahili; alipewa fursa ya kucheza na wenzake, hakufungiwa kama mtoto wa ‘geti kali’.
Pia, alipewa ulinzi. Hakudhurika na vitendo vya ukatili wa watoto; ukatili wa kimwili, kihisia, kiakili.
 Staha ya chini, malezi na tabia zake
Mtu mwenye staha ya chini (low self-esteem) kwa kwaida hajipendi, hajikubali jinsi alivyo na wala hajithamini kwa uwezo na vipawa alivyonavyo.
Wazazi na walimu hupaswa kufahamu sababu za kimalezi zinazosababisha watu kuwa na staha ya chini ili wasifanye makosa. Baadhi ya tabia za watu wenye staha ya chini ni hizi zifuatazo:
Hawana maamuzi. Mara nyingi wanaona vigumu kufanya maamuzi, hii ni kwa sababu ya kuogopa kufanya makosa. Hufanya maamuzi pale tu wanapojiridhisha kwamba kwa asilimia 100 watapata matokeo mazuri; ni waoga na wenye wasiwasi, hivyo hukwepa mazingira yanayowatia hofu; hufikiri kuwa hawawezi kufanya jambo jipya kwa kuwa hawajui kitu.
Hawathamini vipawa walivyonavyo; hujitazama na kujiona kwamba watu wengine wana uwezo na ni bora kuliko wao; huogopa kuongea na watu hasa kueleza hisia zao.  Pia, hawana uhakika wa hisia zao (hawazijui), hivyo hushindwa kujieleza wanavyojisikia; hawawezi kushindana na mtu mwingine; huwa wagumu kutambua makosa yao; hujihisi kwamba hawawezi kusimamia maisha yao wenyewe.
Pia, hufikiri wao ni wajinga. Mara nyingi wametafuta viongozi wa kufanya hata yaliyowahusu wao. Hivyo, hutegemea  watu wengine kutekeleza majukumu yao. Huogopa kuwa wa kwanza kufanya jambo; huogopa kushiriki katika matukio mbalimbali ya kijamii yanayotokea shuleni, mahali wanapoishi au eneo lao la kazi; hawaridhiki na wanafikiri hawawezi kufanya jambo vizuri na hujawa na fikra hasi za kushindwa.
Huamini kila jambo wanalofanya litakuwa na matokeo mabaya. Na ikitokea hivyo,  hutafuta wa kumtwisha lawama.

Malezi yanayosababisha watu kuwa na staha ya chini
Watu wasiojiamini, ni matokeo ya malezi na makuzi waliyoyapata kipindi cha utotoni. Tabia hii huwa mwiba kwa watu kutimiza ndoto zao.
Tafiti zinaonyesha kuwa kama mzazi au mlezi ni mwathirika wa staha ya chini, kuna uwezekano mkubwa wa baadhi ya watoto wake kurithi tabia hiyo.
Hata walimu wa jinsi hiyo pia, huwa na hatari ya kuwaambukiza baadhi ya wanafunzi wao. Baadhi ya tabia za kimalezi zinazosabisha mtu kuwa na staha ya chini (asiyejiamini) ni kama hizi zifuatazo:
Kudekezwa, kufundishwa nidhamu ya woga; kunyimwa fursa ya kucheza. Badala yake kufungiwa ndani; kunyimwa haki ya kucheza na watoto wenye umri wake; kunyang’anywa sauti, yaani hakupewa uhuru wa kutoa maoni yake, kujaliwa na ku
Pia, aliyefanyiwa ukatili wa kimwili (kipigo), kihisia (kuchekwa, kukaripiwa (sauti ya juu au ukali, kudharauliwa, kuitwa kwa majina ya kudhalilisha) na kimapenzi (kubakwa); aliyepewa upendo wenye masharti.
Aliyepoteza wapendwa wake kama vile  wazazi, mzazi mmoja, dada au kaka kwa kifo) akiwa na umri mdogo; kuishi chini ya sheria zilizo kigeugeu, kukatazwa kila anachokifanya.
Kwa kufahamu mazingira yanayoathiri staha ya mtu, ni wajibu wa walimu na jamii kusaidia ili kujenga jamii yenye staha ya juu.