Mchango wa takwimu na Tehama kwa maendeleo endelevu

Muktasari:

Ili kujua tunapotoka, tulipo na tunapotaka kwenda ni lazima tutumie takwimu ili zituelekeze njia bora ya kuwekeza muda, gharama,wataalamu na rasilimali nyingine.

Tunahitaji takwimu bora ili kuweza kupanga vyema matumizi ya rasirimali fedha, maliasili na watu. Hakuna mtu, kaya, jamii au taasisi yoyote inayoweza kupanga mipango ya maendeleo bila kuwa na takwimu sahihi.

Ili kujua tunapotoka, tulipo na tunapotaka kwenda ni lazima tutumie takwimu ili zituelekeze njia bora ya kuwekeza muda, gharama,wataalamu na rasilimali nyingine.

Kwa kuhakikisha mchango wa takwimu na Tekonolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) unaonekana katika malengo ya maendeleo endelevu, ni muhimu kwa Serikali kutambua na kuzirasimisha takwimu zisizo rasmi (non-official statistics) ambazo kwa kiasi kikubwa zinakusanywa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na ngazi za vitongoji.

Takwimu zinazokusanywa katika ngazi za chini ni muhimu sana katika kuwezesha upangaji wa shughuli za maendeleo kuanzia ngazi ya chini ambako kimsingi ndiko kuliko na wananchi wengi.

Kwa sheria ya takwimu ya mwaka 2015, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ndiyo imepewa jukumu la kimsingi la kukusanya, kuchakata na kuzitangaza takwimu rasmi ambazo kwa kiasi kikubwa haziakisi hali halisi iliyopo ngazi za chini kwa wakati.

Kila mmoja kwa kujua au kwa kutokujua amekuwa kwa namna moja au nyingine akifanya matumizi ya takwimu katika shughuli mbalimbali za kila siku.

Kwa mfano, kaya ikiwa na watu watatu, mahitaji ya chakula yatakuwa tofauti na kaya yenye watu watano kama sababu nyingine hazitatumika.

Uamuzi wowote unaofanywa na serikali katika sekta mbalimbali, lazima utokane na takwimu.

Kiwangao cha utekelezaji wa uamuzi unaozingatiwa na usiozingatia takwimu hutofautiana kwa kiwango kikubwa.

Uwapo wa takwimu bora unachangiwa na mifumo bora ya ukusanyaji, uhifadhi, uchakataji na utoaji wa ripoti.

Serikali chini ya taasisi zake mbalimbali imekuwa na mifumo ya Tehama ambayo lengo lake kuu ni kurahisisha kutoa taarifa pamoja na takwimu kwa jamii.

Ipo mifumo inayo ratibu masuala ya watumishi, mipango na bajeti, mapato na matumizi, takwimu za elimu na afya kwa kutaja michache. Kuna uhusiano wa karibu kati ya upatikanaji wa takwimu bora na mifumo ya Tehama.

Ni kazi nzuri inayoendelea kufanywa na serikali ya kuhakikisha inakuwa na mifumo inayodhibiti rasilimali za nchi zikiwamo fedha, maliasili na watumishi.

Upo uhitaji mkubwa wa kuhakikisha mifumo iliyopo sasa inaungwanishwa na kuwa na mfumo mmoja imara ambao utakuwa unatoa takwimu zilizopo katika mifumo iliyopo.

Mfumo huo mpya hautaondoa haki ya kuendelea kwa mifumo iliyopo. Wenyewe utakuwa kama “kapu” la kukusanya na kutoa takwimu zilizopo katika mifumo mingine.

Pia, utasaidia wananchi kujua baadhi ya takwimu ambazo wanaweza kuzitumia katika kupanga shughuli zao za maendeleo.

Kwa tafsiri ya kawaida ni kuwa, kiongozi yeyote wa Serikali kutegemea na kanuni na taratibu zitakazopendekezwa, awe na uwezo wa kuona na kulinganisha takwimu za sekta mbalimbali kama za maji, kilimo, elimu, na afya kupitia mfumo mmoja.

Kwa mfano, kiongozi akifungua mfumo ninaouzungumzia aweze kuona taarifa za mapato na matumizi bila kuondoka kwenye uso wa mfumo, aweze kuona matumizi ya mapato ya serikali kwenye vituo vya kutolea huduma zikiwamo afya na shule ili kulinganisha mapato na matumizi ya fedha za Serikali.

Kwa vyovyote vile hakuna namna maendeleo ya kasi na haraka yanaweza kupatikana bila kuimarisha mifumo ya Tehama na takwimu.

Wakati sasa umefika wa Serikali kuweka mikakati ya kuanzisha kitengo cha kuratibu shughuli zote zinazohusu takwimu zisizo rasmi za kila siku ili NBS ibaki na kazi moja ya takwimu rasmi zinazotokana na sensa, utafiti na upimaji (survey).

Mwandishi ni Mtakwimu na Ofisa Mipango