Miaka 54 na kero zinazoongeza nyufa za Muungano

Muktasari:

  • Kwa viapo vyote, kwa fikra zangu, pamoja na tambo nyingi na kama ambavyo nimekuwa nikiandika hisia zangu mara zote, Muungano huu ni zaidi wa msukosuko na mashaka kuliko wa faida, zaidi ya kuwa umedumu na unadumu kwa sababu ya kukosa hiari ya kujitoa, na kama ipo basi imevizwa na nguvu za kisiasa na hata imani kuwa halitawezekana kiusalama.

Kwa zaidi ya nusu ya umri wangu nimekuwa, kwa hiari yangu au kwa kazi au kwa kuombwa kama nilivyoombwa sasa, nikiandika makala za Muungano, maadhimisho ya kila mwaka ifikapo Aprili 26 kusherehekea sio tu utiaji saini mkataba wa kuzikutanisha kwa ndoa ya kudumu Zanzibar na Tanganyika, lakini pia mapitio yake ya mafanikio na matatizo.

Kwa viapo vyote, kwa fikra zangu, pamoja na tambo nyingi na kama ambavyo nimekuwa nikiandika hisia zangu mara zote, Muungano huu ni zaidi wa msukosuko na mashaka kuliko wa faida, zaidi ya kuwa umedumu na unadumu kwa sababu ya kukosa hiari ya kujitoa, na kama ipo basi imevizwa na nguvu za kisiasa na hata imani kuwa halitawezekana kiusalama.

Basi kukiwa na Muungano wa aina hiyo wa kuwa pande zinazohusika zinaishi kwa shaka, zinaishi kwa kutokuaminiana na mara kadhaa upande mmoja unazidi kujisogezea mamlaka na madaraka na upande mwingine unanywea na kunyong’onyea, ukijiona mdogo zaidi kila siku na nguvu zake za udhibiti zikipungua, ifikapo hapo utakuwa ni Muungano wa mazoea.

Na kwa ukweli baada ya miaka 54 sasa Muungano huu ni wa mazoea tu. Kwamba tunaamka asubuhi Muungano upo, tunakaa mchana bado upo, jua linatua bado upo, alfajiri tunauona bado na kwa hivyo asubuhi nyingine bado upo. Upo kwa kuwa upo lakini si wa tija wala tijara, ni wa hasara si wa biashara. Upo kwa kuwa hauwezi kuvunjika

Na yote yameanzia kwa mfumo wake ambao tunajisifu ni wa aina yake. Tumekuwa tukisifu wepesi na urahisi wa Muungano huu ulivyoingiwa kama vile hiyo ilikuwa ni sifa wakati ambao huo baada ya muda sasa naanza kubaini kuwa ndio msingi wa tatizo.

Ili kuungana nchi moja na nyingine, zote zikiwa ni huru lazima zipitie mchakato. Hivi sasa ndio nabaini nchi zote ambazo hazikufanya hivyo au miungano yoyote ambayo haikufanya hivyo basi imekufa tena fofo. Msiri na Sudan au Senegal na Gambia.

Mchakato wa kuungana nchi mpaka zikafika kuingia hatua za kisiasa huchukua muda ili kujiridhisha na kusomana iwapo kweli nia ni thabiti pande zote. Huanzia mikataba na kupita hatua kama vile muungano wa masoko (custom union), hatua ya muungano wa kifedha na mwisho kuishia muungano wa kisiasa nikitaja kwa haraka mchakato huo.

Ila Tanzania ilikwenda moja kwa moja kupitia Rais Julius Nyerere na Rais Abeid Karume, wakikiuka masharti muhimu ya hatua za miungano. Na ndio maana hata baada ya kufikia hatua ya mwisho kabisa ya muungano mambo ya msingi bado yanadaiwa na kila upande, lakini zaidi kwa Zanzibar.

Mpaka leo haki za kisiasa za Zanzibar haziko wazi na zile zilioko wazi hazitolewi na Zanzibar kubaki kuzidai kila dakika. Hivi Muungano gani tulitaraji ambao kura zote za upande wa Zanzibar ziwe hazina sauti kabisa katika kapu kuu la kuchagua Rais wa Muungano? Ina maana gani kwa Zanzibar basi kupiga kura kwa Rais wa Muungano ilhali kura zake hazina thamani –uzito - mazingatio yoyote, yaani ashakum : ni kura za kujamba kwenye maji?

Hivi ni muungano gani ambapo unashindwa kutamka urais utakwenda kwa zamu kwa sababu nchi hizi mbili zina mamlaka sawa, na badala yake tunaliogopa suala hili na kwa hivyo kuamuliwa kisiasa kukidhi mahitaji ya chama ambacho kimetutawala kwa miaka yote ya Muungano? Kuwa kudai zamu ya urais iwe si sahihi?

Unakuwaje Muungano ambapo ndani yake kuna Serikali tatu ndani ya nchi, ilhali makubaliano ni Serikali mbili yaani ya Zanzibar na ya Muungano, lakini ile ya Tanganyika iwe kinyemela? Hivi mwenye chembe tu ya busara haoni kuwa kuna Serikali ya Tanganyika chini ya Waziri Mkuu ambaye hana mahusiano yoyote yale na Serikali ya Zanzibar?

Tumeona jinsi ambavyo pamoja na mamlaka za Mahakama Kuu za Zanzibar kuwa na mamlaka sawa, lakini pia tunashuhudia mamlaka za upande mmoja zikifanywa kuwa kubwa zaidi hata kuweza kuwahamisha watuhumiwa kama vile Masheikh wa Uamsho kwenda kushtakiwa upande mwingine na Mahakama Kuu za huko, kuwazuia kwa miaka mitano bila ya kesi wanayoshutumiwa nayo kuanza. Huo ni utata mwingine ambao hauna suluhu.

Kwa utata kama huu umekuwa ukionyeshwa na ambapo kuna mifano mingi ambayo imeonyeshwa na ambayo kwayo haiendani na hali (spirit) ya Muungano tunaosema tunajenga, lakini maoni hayo yanapuuzwa au yanagonga ukuta na huku upande mmoja ukifaidi keki ya Muungano na upande mwingine ukiishia kulalama.

Lakini, pia Muungano huu umekuwa na shutuma na shaka nyingi kwa Zanzibar kama vile pande hizi mbili ziliungana ili mmoja awe mdogo na mwingine awe mkubwa, mmoja awe na sauti na mmoja anyimwe au mmoja awe na tonge kubwa mwingine arambe makombo. Umekuwa kama kwamba ni Muungano wa mmoja kukosa na mwingine kupata na kuwa ni Muungano wa kugawana hasara na sio utajiri.

Tulipoungana tulijua Zanzibar ni kisiwa, ni ndogo na ina idadi ndogo ya wananchi na udogo wa soko. Kwamba kwa umbile la kisiwa bila ya shaka litakuwa na changamoto zake za kiuchumi na hakuna njia ila kujiendesha kwa njia za uchumi wa visiwa kama vile nchi za visiwa nyingine zinavyojiendeleza kwa mifano ya mafanikio makubwa.

Hakuna maana ya Muungano iwapo mpaka leo Serikali ya Muungano haijui kuwa hii ni dola moja, uchumi mmoja na soko moja ambalo linawashiriki wawili walio sawa kimamlaka na kwamba ni ukweli kuwa wanatofautiana kwa nguvu za kiuchumi. Na kwa hivyo tofauti hiyo ambayo ni changamoto ingepaswa na inapaswa igeuzwe kuwa ni fursa. Lakini wapi.

Kinachofanywa ni kutwa kuiona Zanzibar ni korofi na kuwa ni uchochoro, ni njia ya panya ya kupenyeza bidhaa zisizolipwa ushuru. Kama vile hilo linafanywa na Wazanzibari wote na kuwa hakuna wafanyabiashara wanaolipa kodi zao halali. Kuwa kama kuna wakorofi hao basi ni sawa na wale wanaopenyeza bidhaa Sirari kutoka Kenya, au Mbeya kutoka Malawi, au Tunduma kutoka Zambia au pia Kyaka kutoka Uganda. Hao ni watafutiwe njia zao na sio kuiadhibu na kuisulubu Zanzibar kama Zanzibar.

Ila pamoja na yote yanaikuta Zanzibar haiwezi kujibu mapigo ya kiuchumi kama vile nayo kuzuia bidhaa za Bara kuingia Zanzibar kama ilivyozuiwa sukari yake kwa kisingizio kuwa yenyewe haitoshelezi mahitaji ya Zanzibar. Kwa kweli hiyo ilikuwa ni kauli mbaya dhidi ya Wazanzibari, ambao kikubwa kwao ni kupiga kelele.

Kama hiyo haitoshi, Muungano huu haujali nafuu na fursa za kiuchumi za Zanzibar hivi karibuni ulizuia meli za kimataifa kusajiliwa kubeba bendera ya Tanzania na kuathiri uchumi wa Zanzibar kwa sababu biashara hiyo imeshuka toka meli 470 mpaka sasa kwenye daftari zipo 350 na kuwa mapato yafikayo dola 150,000 kwa mwezi yatakuwa yameshuka kiasi cha kutisha.

Wazanzibari wanajiuliza kama suala ni kuwa meli zinapakia silaha au mihadarati ni kwa meli za Tanzania tu? Na Tanzania itazuiaje nia mbovu ya watu wenye nayo katika biashara ya kimataifa? Lakini suala muhimu zaidi je, haki ya Zanzibar kupeperusha bendera ya Tanzania ina mipaka? Na kama ipo ni ipi?

Wakati nakamilisha makala hii nikapata mshtuko mwingine ambao unazidi kujenga hoja yangu kuwa hatujui Muungano huu tunaupeleka wapi. Huu ni mkasa wa Mzanzibari mmoja aliyetakiwa na Ubalozi wa Hispania alikokuwa anaomba viza afanye uthibitisho wa cheti chake cha ndoa iliyofanyika Zanzibar.

Ubalozi wa nchi hiyo umekataa uthibitisho huo ufanywe na taasisi ya Zanzibar ila wakatoa maelekezo lazima ufanyike na taasisi ya usajili wa vizazi na vifo ambayo ni taasisi ya Muungano yaani RITA na akafanya hivyo.

Kwa Mtanzania cheti hicho kupata ithibati mtu hutakiwa alipe Sh20,000, lakini yeye aliambiwa kwa taratibu za RITA ndoa yake kufanyika Zanzibar inachukuliwa “kuwa imefanyika nchi ya kigeni” na kutakiwa kulipa Sh100,000 kwa huduma hiyo.

Hapo ndipo tulipofika.

Yapo mengi ya kujiuliza kila Muungano ambao huku ukiongeza umri wake na nyufa zinazidi kuwa nyingi kuliko kuimarika, na Watanzania wasihadaike na utulivu wa uji wa uwele. Fursa nzuri ya kuwa na Katiba Mpya ilikuwa ni mujarab kutibu matatizo mengi, lakini tukaipiga teke.

Tusijidanganye kuwa hali itakuwa hivihivi kila siku Zanzibar ikinyang’anywa fursa za kiuchumi kila uchao, na huku fursa za kisiasa zikiwa zimechukuliwa nyingi na usawa wa Tanganyika na Zanzibar kwenye Muungano wenyewe ukiwa unakula kwa upande wa Zanzibar.

Vizazi vinazaliwa na kuongezeka na ukweli vinakuja na nguvu zaidi za kuhoji ambao vilivyopita vilikuwa na subira lakini tulivyo navyo vinazidi kukosa subira. Ni bora sasa kuondosha vikwazo vyote ili kulinda Muungano wa kesho na kesho kutwa.