Mikopo itolewe kwa Wabunifu wa Tehama kutatua kero zilizopo

Muktasari:

  • Tangu kuanza kwa matumizi ya simu za mkononi miaka ya 1990 kisha huduma ya intaneti, biashara zimeendelea kushamiri duniani. Pamoja na kurahisisha huduma, mawasiliano yameongeza ushirikishwaji wa jamii katika masuala mbalimbali.

Uchumi endelevu unachangiwa na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ambayo husaidia, kwa kiwango kikubwa, kufungua fursa na kuunganisha huduma haraka.

Tangu kuanza kwa matumizi ya simu za mkononi miaka ya 1990 kisha huduma ya intaneti, biashara zimeendelea kushamiri duniani. Pamoja na kurahisisha huduma, mawasiliano yameongeza ushirikishwaji wa jamii katika masuala mbalimbali.

Tangu miaka hiyo, matumizi ya simu za mkononi na huduma za mitandao yamezidi kuongezeka kwa kasi. Takwimu Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) zinaonyesha mwaka 2000 kulikuwa na watumiaji 110,518 wa simu ambao mpaka mwishoni mwa mwaka jana walifika zaidi ya milioni 40.

Mkurugenzi wa ITU, Brahima Sanou anasema Tehama ni nyenzo muhimu ya kufanikisha utekelezaji wa Maendeleo Endelevu (SDGs) yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

“Takwimu zinaonyesha zaidi ya theluthi mbili ya watu duniani wanaishi kwenye maeneo ambayo yana mkongo wa mawasiliano. Pamoja na fursa hiyo, nusu yao hawatumii intaneti,” anasema Sanou.

Anawataka wadau kuhamasisha matumizi ya intaneti ili kuharakisha maendeleo ya wananchi na ukamilishaji wa SDG.

Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi (Costech), Dk Hassan Mshinda anasema zipo jitihada za kuhakikisha vijana, bila kujali kiwango chao cha uvumbuzi, wanatumia vyema fursa za ubunifu wa Tehama kutatua kero mbalimbali zilizopo nchini.

Anasema program ya Buni iliyopo kwenye ofisi za Costech inatoa nafasi kwa kila kijana mwenye wazo. “Vijana wanapewa nafasi ya kuanda miradi yao hapa kabla hawajaipeleka sokoni,” anasema Dk Mshinda.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, asilimia 0.12 ya Watanzania walikuwa wanatumia intaneti mwaka 2000 ambao mpaka mwishoni mwa mwaka 2016 wamefika asilimia 13.

Mwanzilishi wa Buni, Jumanne Mtambalike anasema kuwapo kwa mkongo wa taifa kumepunguza gharama za intaneti jambolinalowafanya wananchi wengi kutumia mitandao ya kijamii.

Hata hivyo anasema: “Wachache wanatumia intaneti kwa ubunifu na uendelezaji wa biashara. Watanzania wengi hawajui faida za mkongo wa taifa hivyo kutokuutumia.”

Wabunifu wachache waliopo nchini, anasema wanakabiliwa na ukosefu wa mitaji na taasisi za fedha nchini hazitoi mikopo kwenye eneo hilo hivyo kuongeza ugumu wa kukua kwa sekt ahiyo.

“Benki hazijaona fursa iliyopo huku. Lakini ndiyo sekta inayotoa mamilionea wa dunia,” anasema Mtambalike na kuitaka serikali kupunguza masharti kwenye miradi ya wabunifu hao.

Ripoti ya Shirikisho la Kampuni za Simu Duniani (GSMA) mwaka 2016 inaonyesha kuna watumiaji milioni 420 wa simu za mkononi Afrika idadi inayokadiriwa kufikia milioni 535 mwaka 2020.

Mkurugenzi Mkuu wa GSMA, Mats Granryd anasema ifikapo mwaka 2020 ongezeko la umiliki wa simu utakuwa asilimia 6.1 hivyo kuwafikia zaidi ya asilimia 50 Afrika.

“Kasi ya 3G itaendelea kuwa teknolojia inayotawala kwa siku zijazo lakini uunganishaji wa intaneti ya 4G unakua kwa kasi,” anasema mkurugenzi huyo. Zaidi ya watu milioni 19.86 nchini wanatumia intaneti.

Nchi zinazoongoza kwa ongezeko la matumizi ya simu za mkononi ni Tanzania, Congo (DRC), Ethiopia na Nigeria. Matumizi hayo nchini yamechangiwa na uhitaji wa huduma za fedha.

Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ya nusu mwaka 2016/17 inaonyesha sekta hiyo ilichangia asilimia 9.5 kwenye Pato la Taifa (GDP) huku ikitoa zaidi ya ajira milioni 3.7.

Mwaka 2016 zaidi ya miamala 43 kwa siku ilifanyika na kuchangia mapato ya kampuni kwa zaidi ya Dola bilioni moja za Marekani. Taarifa ya robo mwaka ya kwanza 2017 ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) inaonyesha zaidi ya watu milioni 19.2 walipata huduma za fedha kwa simu za mkononi.

Mkurugenzi wa biashara wa Vodacom yenye wateja zaidi ya milioni 12, Sitoyo Lopokoiyit hiyo inatokana na kuwapo kwa sera rafiki katika uwekezaji na uvumbuzi wa teknolojia.

“Huduma za M-Pesa zimekua kwa asilimia 20 mwaka huu. Tunazidi kuboresha huduma pamoja na kupunguza gharama kwa zaidi ya asilimia nane, hii ni safari kubwa na inahitaji ushirikiano kati ya wadau wa sekta hii,” anasema.

Aidha, teknolojia ya mawasiliano imezidi kuimarisha taasisi za fedha hasa benki za biasahara kwa kuziunganisha na simu za mkononi ili kurahisisha huduma.

Mkurugenzi wa GSMA, kusini mwa Afrika, Akinwale Goodluck anasema baadhi ya kodi zinaminya ukuaji wa sekta ya mawasiliano huku kikiwa na changamoto ya masoko, sheria na sera za mataifa mbalimbali.

“Kuwa na uwiano wa tozo na ada elekezi kutasaidia kuinua sekta ya mawasiliano, kukua kwa uchumi na kustahimili uwekezaji,” anaeleza mkurugenzi huyo.

Pamoja na hayo, anawataka watoa huduma kuwa wabunifu kwa kuangalia vyanzo vipya vya mapato na kuongeza ufanisi wa huduma zao.

Serikali

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan anasema ushirikiano unahitajika kukabiliana na changamoto zilizopokwenye sekta ya mawasiliano ili kuongeza mchango wake kwenye maendeleo ya wananchi kwenye sekta mbalimbali.

Anasema hali si nzuri maeneo ya vijijini ambako huduma za mawasiliano hazijafika kwa kiwango kikubwa kutokana na miundombinu mibovu.

Endapo kila mdau atatekeleza wajibu wake, anasema: “Kupitia mawasiliano tunaweza kufungua fursa nyingi za kiuchumi zilizopo katika nchi yetu.”

Mwaka 2009 serikali ilianza kujenga mkongo wa taifa wa mawasiliano na tayari zaidi ya Sh30 bilioni zimetumika na kuwawezesha zaidi ya asilimia 83 ya Watanzania kuwasiliana kwa simu za mkononi. Awamu tatu kati ya tano za mkongo huo zimekamilika.

Kwa mara ya pili mfululizo, mkutano wa nne wa GSMA umefanyika nchini mwaka huu na kutoa fursa kwa wadau ambao pamoja na mambo mengine, wamekubaliana kuimarisha huduma na kuongeza kasi ya usambazaji huduma vijijini. Ulifanyika mwaka jana pia.