BIASHARA LEO : Mipango itachangia mafanikio ya wajasiriamali wadogo na kati

Muktasari:

  • Biashara yenye malengo mazuri hupita njia sahihi bila vikwazo vingi na kuwa na matokeo makubwa.
  • Yapo maeneo ambayo ni vyema wajasiriamali wakayaangalia ili kuzifanya biashara zao ziendelee kuwa hai na zifanye kazi nzuri mara kwa mara.

Moja kati ya kundi linalohitaji kuweka mipango ya utendaji sawa ili kufanikiwa kwa kiwango kinachohitajika, ni wajasiriamali wadogo na kati. Hii ni muhimu kutokana na ukweli kwamba mzunguko wa biashara umeyumba, hivyo ili kuendelea kubaki sokoni kwa mafanikio.

Biashara yenye malengo mazuri hupita njia sahihi bila vikwazo vingi na kuwa na matokeo makubwa.

Yapo maeneo ambayo ni vyema wajasiriamali wakayaangalia ili kuzifanya biashara zao ziendelee kuwa hai na zifanye kazi nzuri mara kwa mara.

Kuwekeza kwenye bidhaa zenye mzunguko wa haraka ni miongoni mwa mambo hayo muhimu. Katika kipindi hiki, siyo kila bidhaa iliyopo sokoni inapata walaji au watumiaji wengi kwa sababu wateja wanafanya ununuzi kutokana na umuhimu wa bidhaa na huduma husika.

Kikubwa kwa wajasiriamali ni kuwekeza nguvu kwenye bidhaa ambazo zinatoka haraka na watu wanazihitaji zaidi kwa mfano; chakula na nyingine zinazokamilisha mahitaji makubwa ya binadamu. Bidhaa nyingine zitakuwa zinatoka lakini mzunguko wake utakuwa mdogo.

Kufanya kazi kwa ubia au ushirikiano na wadau wengine ni suala jingine ambalo linaweza kuchangia mafanikio ya wajasiriamali wadogo na wa kati. Kuna ulazima wa kubadilisha mifumo ya umiliki, ili kuisogeza biashara karibu na wateja na kuipa nguvu ya mtaji na utendaji.

Kwa biashara zinazofaa kufanya ushirikiano wa umiliki na masoko, ni vizuri njia za bora za kufanya kazi na watu wenye nafasi ya kufanikisha biashara wakawa nafasi husika.

Umuhimu wa ushirikiano wa biashara siyo kwenye mtaji pekee bali mahitaji mengine, ikiwamo kuwa na mdau ambaye atakuwa na nguvu ya kuwekeza kwenye eneo unalohitaji na mkanufaika kwa pamoja.

Kitu kingine muhimu kwa wajasiriamali ni kutengeneza msingi wa soko la uhakika kwa bidhaa zao. Kuna umuhimu kwa mjasiriamali kuhakikisha anatengeneza kundi la wateja ambao watakuwa na imani na bidhaa, au huduma zake ili kujiwekea uhakika wa kuuza wakati wote.

Ukiwa na uhakika wa wateja, kikubwa unachotakiwa kukifanya ni kuendelea kuboresha na kuongeza thamani kwenye bidhaa na huduma zako ili kuzifanya ziendane na mahitaji ya wateja ulionao.

Ni muhimu kutengeneza kundi hili la uhakika kwa sababu sasa hivi ushindani ni mkubwa, hivyo ni vizuri kutafuta soko hata nje ya eneo lako unalofanyia biashara.

Umakini kwenye masuala ya fedha na biashara ni sehemu nyingine inayohitaji uangalizi wa kina kwa faida ya biashara husika. Sekta ya fedha ndiyo mhimili mkuu kwenye biashara zote, wajasiriamali wanatakiwa kuendelea kuboresha utaalamu wao wa fedha kwenye maeneo yote kuanzia uhusiano na taasisi za fedha na wataalamu wa ushauri.

Tuboreshe utunzaji wa kumbukumbu za fedha, tujitengenezee uwezo wa kuandaa mipango ya biashara kwa muda mfupi na mrefu ili kuwa na dira makini.

Jingine muhimu ni kufuata sheria na taratibu zilizopo. Moja ya changamoto za wengi kuzingatia kinachoagizwa na Serikali. Wakati wote mjasiriamali unatakiwa kufuata taratibu zinazohusu biashara yako, kuanzia kuirasimisha, ulipaji kodi na kufuata sheria na taratibu zinazoongoza unayofanya.

Kwa kufanya hivyo, tutakuwa na uhusiano mwema wa biashara na Serikali, taasisi za fedha, wawekezaji wenye mitaji na wadau wengine wa maendeleo. Biashara inayotengenezwa kwa malengo mazuri yanayotokana na utulivu wa mawazo na tafiti ndogo inakuwa na msingi mzuri wa kufika mbali, kwa sababu itakuwa inafahamu njia sahihi.