Mtaji wa kuanza kwa kuku wa kisasa

Muktasari:

  • Tulianza kwa kuangalia ni namna gani mtu anaweza kufuga kuku kibiashara na si kuishi na kuku.
  • Tukachambua ujenzi wa mabanda bora ya ufugaji wa kuku wa asili na kuku wa kisasa (broilers), baadaye tukaangalia koo za kuku zinazoweza kuhimili mazingira ya Kitanzania.

Katika mfululizo wa makala haya ya ufugaji wa kuku kibiashara, nimefanikiwa kuchambua mambo manne hadi kufikia sasa.

Tulianza kwa kuangalia ni namna gani mtu anaweza kufuga kuku kibiashara na si kuishi na kuku.

Tukachambua ujenzi wa mabanda bora ya ufugaji wa kuku wa asili na kuku wa kisasa (broilers), baadaye tukaangalia koo za kuku zinazoweza kuhimili mazingira ya Kitanzania.

Jambo la nne ambalo tunalihitimisha wiki hii ni kiasi gani cha mtaji mtu anaweza kuanza nacho katika kufuga kuku kibiashara na hatimaye kutimiza malengo yake.

Eneo hili tulilijadili kwa undani wiki mbili zilizopita tukiangalia mtaji wa kuanzia kwa kuku wa asili.

Wiki iliyopita ilikuwa nikamilishe mada hii kwa kujadili gharama ya mtaji wa kuanzia katika kufuga kuku wa kisasa.

Hata hivyo, nililazimika kuacha kujadili kiasi cha mtaji ambacho mtu anaweza kuanza nacho katika kufuga kuku wa kisasa (Broilers) kama nilivyoahidi baada ya kukamilisha mtaji wa ufugaji wa kuku wa kienyeji, kwa sababu nilipokea idadi kubwa ya maombi ya wasomaji wa safu hii waliokuwa wakitaka kujuzwa kwa undani faida, hasara na umuhimu wa mashine za kutotolesha vifaranga.

Baada ya kufanikiwa kutekeleza kile walichokihitaji wengi, wiki hii nitajadili kiasi cha mtaji anachopaswa kuwa nacho mtu aliye na utayari wa kufuga kuku wa kisasa kibiashara.

Kwa bahati mbaya, kuna tofauti kubwa kati ya ufugaji wa kuku wa kisasa na wale wa asili, ambao wengi wetu tumezoea kuwaita kuku wa kienyeji.

Tofauti ipo zaidi kwenye matunzo. Wanatofautiana mahitaji hasa siku za mwanzoni.

Hali hii inawafanya kuku wa kisasa kumlazimisha mfugaji kuwa na mtaji mkubwa kidogo tofauti na kuku wa asili.

Hata hivyo, tofauti hii haiondoa faida kubwa na ya muda mfupi inayopatikana kutoka kwenye kuku hawa wa kisasa.

Kupata faida kubwa ndani ya muda mfupi si jambo jepesi, lakini linawezekana kwa sababu wapo waliofanikiwa. Jambo la kuzingatia ni kuthubutu, kuvumilia na kubeba dhamira ya kweli ya kufuga kuku kibiashara.

Kama ilivyo kwenye biashara nyingine, hata huku kwenye ufugaji wa kuku wa kisasa nako kunakabiliwa na changamoto ya magonjwa pamoja na soko la uhakika.

Hata hivyo, kupitia safu hii tunaweza kupeana njia za kupita ili kupata soko la uhakika.

Jambo muhimu ni kuhakikisha unafuga kuku wako kwa kuzingatia mahitaji yao muhimu ili kuhakikisha wanakuwa na uzito utakaoweza kukuingiza pamoja na kukuimarisha sokoni.

Hili suala la soko na namna ya kufanikisha ufugaji wa kuku wenye hadhi sokoni ni mada inayojitegemea na tutaiongelea kwa kina mbele ya safari. Kwa leo tuendelee na kiasi cha mtaji kinachoweza kukuingiza kwenye ulimwengu wa wafaidika wa kuku wa kisasa.

Kwenye mtaji wa ufugaji wa kuku wa kienyeji hakutofautiani sana na mtaji wa kuku wa kisasa kote unaweza kuanza na mtaji wa Sh500,000 hadi Sh 1.5 milioni.

Tofauti pekee iliyopo ni kwamba kwenye ufugaji wa kuku wa kisasa huwezi kuanza na kuku wachache, lakini pia ni lazima uanze na vifaranga wawe wa kuku wa nyama au wa mayai.

Hesabu ya mtaji ninayoinyambulisha hapa inajumuisha chakula cha kuanzia, hata hivyo inaweza kuongezeka au kupungua kulingana na mfumo wa huduma kwa kuku hao.

Ili uanze ufugaji wa kibiashara wa kuku wa kisasa ni lazima ununue vifaranga, ambavyo kwa kawaida mfugaji analazimika kuanza na vifaranga 100. Ulazima huu unatokana na matakwa ya wauza vifaranga, kwani hawawezi kuuza kifaranga kimoja au wawili.

Kwa wastani kifaranga kimoja kinauzwa kati ya Sh2,000 mpaka 2,500, hivyo ili ufanikishe kununua vifaranga 100 ni lazima mfugaji awe na kiasi cha Sh250,000 hesabu hiyo ni kwa makadirio ya juu.

Faida ya kuku wa kisasa hasa wa nyama hupatikana kwa muda mfupi, lakini si endelevu kama ilivyo kwa kuku wa mayai ambao wana uwezo wa kutaga kwa mwaka mmoja hadi miwili.

Baada ya kukamilisha mtaji ambacho mtu anaweza kuanza nacho katika ufugaji wa kibiashara wiki ijayo tutajadili namna ya kutunza vifaranga, lishe na dawa za kuku ambao tayari wako bandani.

Hata hivyo nasisitiza, kinachohitajika hapa ili kufikia malengo ni uvumilivu na utayari kwani haya mambo hayaji kwa miujiza. Kamwe usitegemee kuishi na kuku ukafikiria kufikia kiwango hiki cha ufugaji. Utasubiri sana.

Itaendelea, 0789063838-Barua pepe [email protected]