Mtizamo wa kiuchumi bajeti ya miundombinu Afrika Mashariki

Muktasari:

Kuna mambo mengi ya kimjadala kuhusiana na bajeti hii itakayotumika miongoni mwa wanachama wa jumuiya ambao ni Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Sudan ya Kusini.

Kwenye mmkutano wao uliofanyika juma la mwisho la mwezi uliopita, wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walikuwa na mkutano wao huko Uganda katika walipitisha Sh175.5 trilioni kutekeleza takriban miradi 200 ya miundombinu ndani ya miaka 10.

Kuna mambo mengi ya kimjadala kuhusiana na bajeti hii itakayotumika miongoni mwa wanachama wa jumuiya ambao ni Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi na Sudan ya Kusini.

Kwa ujumla bajeti hiyo ni kubwa. Ikilinganishwa na bajeti ya Tanzania kwa mwaka huu wa fedha ya Sh31.7 trilioni, ni mara tano na nusu ya kiasi hiki kilichotengwa na jumuiya kwa ajili ya miundombinu tu.

Fedha hizi za miundombinu ni sawa na bajeti ya Tanzania kwa miaka mitano na nusu. Hata hivyo, hii ni bajeti itakayotumika kwa miaka 10 ijayo kwa wastani wa Sh17.6i trilioni kila mwaka miongoni mwa nchi sita wanachama.

Kama kila nchi ingechanga sawa, Sh2.9 trilioni kwa mwaka, basi ingekuwa ni Sh29.3 trilioni kwa kipindi hicho cha miaka 10. Hii ni sawa na asilimia 9.2 ya bajeti yote ya Tanzania kwa mwaka 2017/18. Kwa mtizamo huu, hii si bajeti kubwa sana.

Miradi

Miradi inayolengwa na wakuu wa jumuiya hii ni zaidi ya 200 katika kipindi hicho, wastani wa miradi 20 kwa mwaka. Kiuchumi, kiasi hicho kinaweza kuonekana kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.

Hata hivyo miradi 20 kwa mwaka kwa nchi sita ni wastani wa miradi mitatu kwa kila moja. Hii si mingi kama mambo mengine yote yakikaa sawa. Miradi ya kipaumbele ni pamoja na reli ya kiwango cha kimataifa (SGR), ufuaji umeme kwa kutumia maji, gesi na mafuta na miundombinu mingine ya kikanda.

Bajeti kwenye miundombinu ni uwekezaji wa kupanua uwezo wa nchi kuzalisha za aina tofauti kwa matumizi ya ndani au uuzaji nje ya mipaka yake. Ukifanywa na ikatumika vizuri, ni fursa ya kusisimua na kukuza uchumi wa nchi husika.

Fursa

Kama ilivyo kwa bajeti nyingine yeyote, hii ya miundombinu ya EAC ni fursa kwa makundi mbalimbali ambayo ni pamoja na biashara mbalimbali zitakazohitajika katika kuitekeleza.

Hawa ni pamoja na kampuni za kusanifu, kujenga, kusimamia na kuendesha miradi hii. Wengi watakuwa ni wakandarasi. Pia ni fursa kwa wenye kampuni zinayozalisha na zinazouza malighafi zitakazohitajika kama vile saruji, nondo, mchanga, kokoto au nyaya za viwango tofauti.

Pia kuna fursa kwa watoa huduma mbalimbali kama za fedha, bima, vyakula, malazi, utafiti na ushauri elekezi. Kwa Serikali Kuu na za mitaa pamoja na mambo mengine hii ni fursa ya kupata mapato mbalimbali ya kikodi na yasiyo ya kikodi moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Wazawa

Kati ya mambo makuu ya kimjadala katika utekelezaji wa miradi mikubwa katika nchi nyingi hasa za Afrika kama Tanzania ni ushiriki wa wazawa. Nchi itapata faida nyingi sana na za haraka kama wazawa watapewa nafasi kubwa kwenye utekelezaji wake.

Hii itasaidia kuzalisha ajira nyingi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika nchi husika. Pia fedha zitokanazo na malipo ya kazi hizi zitatumika nchini hivyo kuchangia kusisimua uchumi.

Uwezo wa wazawa

Kati ya masuala ya kimjadala katika ushiriki wa wazawa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ni uwezo wa kampuni zao. Kampuni nyingi hasa za ukandarasi zinaweza kushindwa kushiriki katika miradi hii.

Hii ni kwa sababu ya kushindwa kushindana na kampuni kubwa za nje mfano zitokazo China, India au Ulaya. Zinaweza kushindwa kiutaalamu au kifedha au vyote. Hata hivyo mazingira rafiki na wezeshi ya kisera, kisheria na kiudhibiti yakiwekwa na kutekelzwa katika nchi hizi, kampuni za ndani zinaweza kushiriki kwa njia yenye tija na maana zaidi katika miradi hii.

Haitoshi kampuni hizi kuwa watazamaji au kupewa kazi ndogondogo na kampuni kubwa za nje zinazopata kandarasi kubwa. Lazima kampuni za ndani zijijengee na kujengewa uwezo wa kiushindani katika utekelezaji wa miradi mikubwa ndani ya jumuiya.

Vyanzo vya Fedha

Kati ya maswali makuu yanayoibuka katika utekelezaji wa miradi hii mikubwa ndani ya jumuiya ni pamoja na vyanzo vya fedha za kuigharamia. Kulingana na msimamo wao, wakuu hao wa nchi walisema fedha hizo zitatoka ndani na nje ya nchi ikiwamo za kukopa.

Kiutaalamu fedha za ndani zitatokana na kodi na zisizo za kodi. Fedha za nje zinaweza kuwa za mikopo hata michango ya wafadhili. Fedha kutokana na mikopo zitaongeza ukubwa wa deni la taifa katika nchi hizi. Hata hivyo kukopa na kutumia vizuri mfano kwenye miundombinu ni uwekezaji mzuri.

Chanzo cha fedha kwa miradi kama hii kwingineko duniani huwa ni ubia kati ya Serikali na sekta binafsi. Sekta binafsi katika miradi kama hii hutoa fedha na utaalamu wakati Serikali huweza kuchangia kiasi fulani cha fedha.

Wawili hawa kuweza kuunda kampuni inayojitegemea kutekeleza miradi hii na itakapoanza kutumika au kuzalisha fedha, sekta binafsi hulipwa gharama zake kwa kadiri ya makubaliano. Changamoto katika upande huu wa dunia ni kutokuwa na sekta binafsi yenye misuli ya kutosha kifedha kutekeleza miradi hii.