Mtizamo wa kiuchumi kuhusu diplomasia, maendeleo ya uchumi

Muktasari:

  • Kwa mantiki hii, utendaji wao utapimwa kwa namna wanavyotekeleza dhana hii katika vituo vyao vya kazi. Ipo mitizamo mbalimbali kuhusu diplomasia ya uchumi.

        Kati ya mambo yanayotiliwa mkazo na Serikali katika uhusiano wa kimataifa ni kuimarisha diplomasia ya uchumi ambayo wawakilishi wa Tanzania nje ya nchi wanategemewa kuihamasisha.

Kwa mantiki hii, utendaji wao utapimwa kwa namna wanavyotekeleza dhana hii katika vituo vyao vya kazi. Ipo mitizamo mbalimbali kuhusu diplomasia ya uchumi.

Mabalozi wa Tanzania nchi za nje, kama ilivyo kwa nchi nyingine, hufanya shughuli nyingi za kuliwakilisha Taifa kwenye masuala ya kisiasa, kijamii, kijeshi, kibiashara na kiuchumi.

Diplomasia ya uchumi ni dhana pana. Kwa lugha rahisi inaweza kumaanisha uwakilishi wa nchi nje ya nchi unaojikita katika mambo ya kiuchumi ambayo ni pamoja na yahusuyo uwekezaji na biashara.

Kila moja kati ya haya ni jambo muhimu sana kwa nchi yoyote inayojihusisha kiuchumi kimataifa. Kuna mambo ya msingi ambayo lazima yaeleweke vizuri na yazingatiwe ili diplomasia ya uchumi ifanikiwe.

Kuvutia uwekezaji

Kati ya mambo ya msingi katika diplomasia ya uchumi ni kuvutia uwekezaji kutoka nchi mbalimbali duniani. Ili kuvutia uwekezaji kwa kiwango kinachotegemewa, yapo mambo kadhaa ya msingi ya kuzingatia. Haya ni pamoja na kujua namna ya kuvutia uwekezaji na wawekezaji wenyewe.

Kuvutia uwekezaji na wawekezaji kunahitaji ujuzi maalumu. Pamoja na mambo mengine ni lazima kujua fursa na miradi ya uwekezaji iliyopo katika nchi kwa upana wake.

Hizi ni fursa na miradi katika sekta mbalimbali za uchumi kama vile kilimo, viwanda, madini, utalii na huduma mbalimbali. Fursa na miradi hii inaweza kuwa katika maeneo kadhaa kijiografia kama vile mikoa na wilaya.

Pamoja na kujua fursa za uwekezaji katika muktadha wa diplomasia ya uchumi, ni lazima pia kujua malengo makuu, sera na mipango ya nchi kwa ujumla na katika muktadha wa uwekezaji.

Vilevile ni lazima kujua taratibu zinazotakiwa kufuatwa na mwekezaji kwa ujumla wake na katika sekta na mradi mmoja mmoja kimahususi.

Pia, ni muhimu kubainisha vivutio vya uwekezaji vinavyotolewa na nchi na namna wawekezaji kutoka ndnai na nje wanavyoweza kuvipata. Katika muktadha huu ni muhimu pia kujua wawekezaji wanataka nini kabla ya kuwekeza katika nchi wanayoichagua.

Ingawa juhudi kubwa huelekezwa katika kuvutia uwekezaji, ni vizuri pia kutia nguvu za kutosha kubakiza wawekezaji baada ya kuwavutia. Ni lazima wanaotekeleza diplomasia ya uchumi kujua yote haya na zaidi namna ya kuyatekeleza inavyotakiwa.

Biashara

Pamoja na kuiwakilisha nchi katika shughuli za uchumi, diplomasia ya uchumi inahusu biashara pia. Yapo mambo mbalimbali yahusuyo diplomasia ya uchumi katika tasnia ya biashara. Kati ya mambo haya ni pamoja na kuwezesha wafanyabiashara wa Tanzania kufanya biashara na nchi za nje kwa urahisi.

Mambo haya ni pamoja na kununua na kuuza bidhaa na huduma kati ya nchi husika. Diplomasia ya uchumi katika eneo hili, pamoja na mambo mengine, inapaswa kuwezesha wafanyabiashara kupata masoko ya huduma na bidhaa wanazozalisha na kuuza katika masoko ya nje.

Katika jambo hili wanapaswa kuonyesha ukubwa wa soko la bidhaa na huduma husika na taratibu za kuingia katika masoko hayo.

Pamoja na kuwezesha uuzaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi, diplomasia ya uchumi inapaswa kuwezesha ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka kutoka huko kuja Tanzania. Hii ni pamoja na kubaidi bidhaa na huduma hizi, bei zake na taratibu za kuzinunua ili kuziuza au kuzitumia Tanzania.

Pamoja na hili, diplomasia ya uchumi inapaswa kulenga kuwezesha wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki katika mikutano, makongamano na maonyesho ya biashara ndani ya nchi walizopo.

Vilevile wanapaswa kuwawezesha wafanyabiashara kutoka katika nchi walizopo kuhudhuria katika mikutano, makongamano na maonyesho ya biashara kama vile Sabasaba na Nanenane ndani ya Tanzania. Taarifa za maonyesho haya na taratibu za msingi kuzifuata zinapaswa kuwekwa wazi kwa kutangazwa kwenye mataifa ya nje ili kuongeza ushiriki.

Utalii

Katika diplomasia ya uchumi, kuvutia watalii wa nje kuja nchini ni miongoni mwa vipaumbele. Kama ilivyo kwa uwekezaji na biashara, wanadiplomasia wetu wanapaswa kuwa wawezeshaji wa kuleta watalii nchini.

Kwa mantiki iliyotumika katika uwekezaji na biashara, lazima wajue mambo yote muhimu kuhusu sekta na mazingira ya utalii nchini ikiwa ni pamoja na vivutio vilivyopo. Ni lazima kutangaza na kujibu maswali ya wanaotaka kuja kutalii Tanzania na kuwapa taarifa za namna ya kufika na za kila kivutio wanachotaka kukitembelea na kuwajulisha wasivyovijua.

Ujuzi

Kusudi diplomasia ya uchumi ifanyike kwa ufasaha, ufanisi na jinsi inavyotakiwa, ujuzi wa wanadiplomasia ni muhimu sana. Hii ni kuanzia kwa balozi mwenyewe na timu yake yote.

Kimsingi, diplomasia ya uchumi ni juu ya uchumi kuliko uhusiano wa kijamii na kisiasa. Kwa mantiki hii ni lazima wanadilomasia wafahamu vizuri na kuwa na weledi kuhusu uchumi.

Hata kama uchumi si kitu ambacho baadhi ya wanadiplomasia wanakifahamu vizuri, ni ujuzi wa lazima katika kazi ya diplomasia ya uchumi. Uzuri ni kuwa kila mara kuna nafasi ya kujifunza kile tusichofahamu kama nchi na zaidi mtu mmoja mmoja wakiwamo wanadiplomasia.