Muktadha wa mawasiliano na athari zake

Muktasari:

  • Uandishi ulio rasmi hauna budi kuzingatia taratibu zote za uandishi na muundo maalumu wa andiko linaloshughulikiwa.

Uandishi ni taaluma kama zilivyo taaluma nyingine. Kazi rasmi zina namna yake ya kuandikwa.

Uandishi ulio rasmi hauna budi kuzingatia taratibu zote za uandishi na muundo maalumu wa andiko linaloshughulikiwa.

Kwa upande mwingine, uandishi au mawasiliano yasiyo rasmi yana namna zake za kufanyika pia. Marafiki huweza kuwasiliana kwa namna waonayo inafaa bila kuzingatia urasmi huo.

Lengo la makala haya ni kutaka kuweka bayana kuhusu umuhimu wa uandishi na mawasiliano rasmi, kwa namna ya pekee katika lugha yetu adhimu ya Kiswahili. Siku za hivi karibuni kumekuwa na tatizo kubwa, hususan miongoni mwa vijana kuhusu namna ya kuwasiliana. Wengi wanashindwa kutofautisha aina za mawasiliano wanayoyafanya ikiwa ni rasmi au sivyo.

Mathalani, wapo baadhi ya watu wanapoandika barua za kuomba kazi sehemu mbalimbali, hutumia lugha isiyo rasmi katika muktadha huo rasmi. Katika semina moja iliyohusiana na masuala ya uandishi, mtoa mada alitoa mfano huu:

“...watu siku hizi hawajui kuandika. Nikiwa nakaimu ofisi niliwahi kupokea barua ya mtu akiomba kazi iliyoanza hivi, ‘Mkurugenzi mpenzi sana endapo utanipa kazi hii nita...’” Maneno yaliyotumiwa ni ya Kiswahili fasaha lakini hayakutumika katika muktadha mwafaka.

Msamiati ‘mpenzi’ hauendani na barua za kikazi na pengine unaibua dhana tofauti kabisa katika maombi ya aina hiyo.

Siku za hivi karibuni kumezuka mtindo mwingine wa uandishi wa kuchanganya herufi na tarakimu. Wapo baadhi ya watu ambao hata wanapowasiliana na wazazi wao, wakubwa wao wa kazi na watu wengine waliowazidi umri, hutumia namna hiyo ya mawasiliano ambayo hadi sasa si rasmi.

Kwa mfano, mfanyakazi anaweza kumwandikia mkubwa wake wa kazi ujumbe huu: “Nipo Muhi2, nimelazwa 10a naomba ruhusa” yaani Muhi2 akimaanisha hospitali ya ‘Muhimbili’ na 10a akimaanisha ‘tena’.

Kama ilivyokwishasemwa awali, uandishi huo si rasmi na si wengi wanaoufahamu na kuupenda. Aidha, kwa kuwa uandishi wa namna hiyo hautambuliki katika mazingira rasmi, haufai hata kutunzwa katika kumbukumbu za kiofisi.

Kwa hivyo, aombaye ruhusa kwa msimamizi wake wa kazi anayejua umuhimu wa mawasiliano katika sehemu za kazi kwa namna hiyo, huenda hatajibiwa au kuhitajika atumie lugha rasmi na fasaha ili aweze kueleweka na kusaidiwa.

Kila wakati, mtumiaji wa lugha anapaswa kuangalia mtu anayewasiliana naye. Ikiwa ni rafiki wa kundi rika, mawasiliano huweza kufanyika kwa namna marafiki hao waonavyo inafaa.

Kwa sababu hiyo, mtu afanyaye mawasiliano awe makini mara zote, ajiulize anawasiliana na nani na kwa nini. Kwa kuzingatia hilo ataweza kuwasiliana kwa namna mwafaka. Vijana wanapaswa kuwa makini na suala hili kwa kuwa ndio wahusika wakubwa. Ikiwa mawasiliano unayoyafanya yanahusiana na masuala rasmi ya kazi na mengineyo, tumia msamiati rasmi na fasaha wa Kiswahili. Kabla ya kutuma barua au ujumbe rasmi, ni vyema kumwomba mtu mwingine unayemwamini asome na kutoa marekebisho ikibidi.

Kutofanya hivyo ni kujikosesha fursa au haki ambayo mmoja anastahili kupata kwani ujumbe usio rasmi aghalabu hupuuzwa katika sehemu rasmi.

Ni muhimu kufanya maandalizi kabla ya kufanya mawasiliano rasmi. Msamiati mwafaka utumike, katika muundo unaotambulika wa mawasiliano yanayoshughulikiwa.