UCHAMBUZI: Muziki wa taarabu umedumazwa na wasanii wenyewe

Muktasari:

Yalikuwa ni mabadiliko ya muda mrefu, yalianzia kwa kibao kama ‘Asu’ lakini miaka michache baadaye yakazaa bendi kama Jahazi na nyingine nyingi ambazo kwa pamoja zilijinasibu kwamba zinafanya muziki uitwao ‘Morden Taarab’ au Taradansi.

Mabadiliko hasi katika burudani yalianza pale Abdul Misambano na vijana wenzake walipoanza kuuondosha taratibu muziki wa taarabu ya utulivu iliyofanywa na kina marehemu Issa Matona na kuleta ya kuchezacheza.

Yalikuwa ni mabadiliko ya muda mrefu, yalianzia kwa kibao kama ‘Asu’ lakini miaka michache baadaye yakazaa bendi kama Jahazi na nyingine nyingi ambazo kwa pamoja zilijinasibu kwamba zinafanya muziki uitwao ‘Morden Taarab’ au Taradansi.

Tangu pale mambo yakawa tofauti, wasanii wa taarabu wakaanza kupata fedha iliyowapa nguvu ya kujivunia wanachokifanya ingawa siyo kwa kiasi kikubwa.

Pengine yale ndiyo yalikuwa mabadiliko ya pekee ya maana kwa muziki wa taarabu tangu kuumbwa kwa dunia. Bila shaka baada ya pale, hakuna mabadiliko ya kimaendeleo yaliyowahi kufanywa katika aina hii ya muziki kama ilivyo kwa Bongo Fleva.

Kimsingi bendi na wasanii wanaofanya taarabu kwa sasa ni kama hawaelewi wanachofanya. Hawaelewi wamesimama upande gani, wanafanya aina gani ya muziki; dansi, singeli au muziki wa pwani.

Hawaelewi wanafanya muziki kwa ajili ya mashabiki wa enzi gani, enzi za Baba wa Taifa au Magufuli. Hii inawapa ugumu hata kujua jinsi gani wanaweza kuboresha muziki wao.

Inashangaza mpaka leo wenye taarabu yao wameshindwa kuufanya muziki huu kuwa wa kusikilizwa na kila mtu. Taarab imekuwa ni ya kusikilizwa na aina fulani ya watu ambao kwa mtazamo wa kawaida wanaonekana ni wanawake hasa wale wa mjini.

Wameshindwa kuiga mfano wa Bongo Fleva ambao wakati muziki huo unaanza ulikuwa ukionekana ni wa wavuta bangi, lakini leo hii wasanii wake waitwa Ikulu kuburudisha zinapofanyika hafla mbalimbali.

Tumeshuhudia mwanamuziki Diamond Platnumz akikabidhiwa bendera ya Taifa alipoteuliwa kutumbuiza katika hafla ya ufunguzi wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon). Ni haki yao kwa sababu waliamua kuboresha kazi yao.

Lakini inashangaza hadi leo wanaofanya taarabu wameshindwa kutengeneza nyimbo za muda mfupi ili muziki wao usikike katika vipindi mbalimbali vya redio na televisheni. Taarabu inaishia kupigwa kwenye vipindi maalumu kwa sababu vingine vinahitaji burudani fupi isiyotafuna muda.

Hadi leo nyimbo za taarab zina video za kizamani ilhali wenyewe zinaitwa ‘modern’ kwa maana ya muziki wa kisasa.

Kigezo pekee kinachozifanya ziitwe video ni kwa sababu picha zake zimerekodiwa kwa kamera yenye kunasa mijongeo na mawimbi ya sauti.

Ni video zinazoonyesha wanawake wa bendi husika wamevaa magauni bila mpangilio maalumu unaopendeza, wanachezacheza tu alimradi, kana kwamba wanakwenda kumtunza mwenzao kwenye ‘kitchen Party’.

Inashangaza; wakati Bongo Fleva wanahangika huku na kule duniani kutafuta maeneo ya utofauti ya kupigia picha za video zao, taarabu wenyewe bado kila video yao wanayotoa lazima kuwe na kipande cha ufukwe (beach) tena fukwe zilezile kila siku ambazo hata hazijatengenezwa vyovyote kuendana na umuhimu wa upigaji picha za video.

Haina ubishi kwamba taarabu ni moja ya lulu za kiburudani tulizobarikiwa Watanzania, ni miongoni mwa muziki mkongwe na wa kwanza kuingia nchini.

Bila shaka ili kuilinda na kuitunza lulu hii, wanaofanya taarab wanastahili kuangalia jinsi ya kuboresha muziki wao na ili kufanikiwa katika hilo, ni lazima wawe na mada tofauti katika miziki yao au hata kama ni zilezile waziimbe kwa ubunifu kidogo.

Waangalie jinsi wanavyoweza kuufanya nyimbo zao ziwe fupi ili zisiwe tabu kutumiwa kwenye vipindi mbalimbali vya redio na televisheni vinavyopambana na muda.

Pia, wawe na msimamo, si kila kukicha wanaitohoa taarabu ya aina nyingine ya muziki. Miluzi mingi humpoteza mbwa.

Soko na si kuangalia wengine wamekuja na nini.