UCHAMBUZI: Mwaka 2017 Serikali imalize uhaba wa dawa nchini

Muktasari:

Mifuko hiyo inapunguza kero nyingi wanazopata watu wanapougua ghafla bila la kuwa na fedha. Lakini kampeni inaonekana kukwama kutokana na sababu nyingi hasa uhaba wa dawa kwenye vituo vya matibabu.

Kwa miaka zaidi ya 20 sasa Serikali imekuwa ikihamasisha Watanzania kujiunga kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) au Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Mifuko hiyo inapunguza kero nyingi wanazopata watu wanapougua ghafla bila la kuwa na fedha. Lakini kampeni inaonekana kukwama kutokana na sababu nyingi hasa uhaba wa dawa kwenye vituo vya matibabu.

Watanzania wengi wanasita kujiunga kwenye mifuko hiyo kwa sababu hospitali,vituo vya afya na zahanati za umma mara nyingi hazina dawa. Hawana uhakika tatizo hili litaisha lini. Ni wakati muafaka kwa wahusika kuboresha mazingira ili wagonjwa wasiambiwe wakanunue kwenye maduka binafsi.

Kero hii ni ya siku nyingi ingawa inaendelea kudumu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya hususan za umma. Imeripotiwa hivi karibuni kwamba Hospitali ya Rufaa Bombo iliyoko mkoani Tanga haina dawa za usingizi kwa wanaofanyiwa upasuaji.

Ukiacha ya Mombo, ni kawaida kwa hospitali za rufaa, wilaya hata vituo vya afya kukosa dawa za aina mbalimbali na vitendea kazi vingine. Tatizo hili linasababisha Watanzania wengi wakose imani kwa huduma zinazopatikana kwenye vituo hivyo vya huduma. Serikali inapaswa kulimaliza tatizo hili kwa sababu fedha zipo hasa zinazochangwa za wanachama wa mifuko hii.

Watanzania wanatambua umuhimu wa kuchangia gharama za matibabu ingawa kuna changamoto hiyo. Wananchi wengi wangependa waendelee kutibiwa kwenye hospitali za umma lakini wanayumbishwa na uhaba wa dawa.

Nadhani wakati umefika, Serikali ijipange na kumaliza uhaba wa dawa kwenye vituo vyake vyote vya huduma kwa mwaka huu wa 2017. Serikali ya awamu ya tano ifanye uamuzi mgumu wa kutoa fedha za kutosha kununua dawa zitakazosambazwa kwenye vituo vyote. Kwa upande mwingine Serikali itambue, hospitali za umma kukosa dawa kunachangia, kwa asilimia kubwa, Watanzania wengi kutojiunga kwenye mifuko hii.

Wengi hawaoni sababu za kujiunga wakati vituo vya matibabu vinakosa dawa. Kwa mfano, CHF mkoani Mbeya iliyoanza kufanya kazi tangu mwaka 2004 lakini hadi sasa ni asilimia 30 ya kaya 404,540 ndizo zilizojiunga.

Zaidi ya theluthi mbili ya kaya za mkoa huo hazijajiunga kutokana na kutilia shaka upatikanaji wa dawa. Mkoa unazo halmashauri saba; Mbarali, Chunya, Kyela, Mbeya wilaya na jiji, Rungwe, na Busokelo zikiwa zimejaa wananchi wenye changamoto lukuki za uchumi na afya.

Watu wengi katika halmashauri hizo wanahangaika wanapougua. Matokeo yake, asilimia kubwa, wanapenda kununua dawa kwa hisia badala ya kwenda kituo cha afya ambako hakuna dawa, wakati mwingine na vifaatiba pia.

Wachache, wenye uwezo kifedha, wanaenda hospitali za umma na kulipia kumwona daktari lakini wanaambiwa wakanunue dawa kwenye maduka binafsi. Bila changamoto hizi, wagonjwa wengi wangefurahi kumwona daktari na kupata dawa katika kituo kimoja kuliko kuendelea kuzitafuta madukani.

Hivyo, wakati umefika kwa Serikali kujipanga mwaka 2017 kumaliza ukosefu wa dawa kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati zote za umma zilizopo nchini na kurahisisha uhamasishaji wa wananchi kujiunga na mifuko ya afya hivyo kujihakikishia mapato.

Jamii yanye afya itakuwa na nguvukazi ya uhakika kuhudumia uchumi wa viwanda ambao Serikali imejidhatiti kuujenga nchini kabla ya mwaka 2025 na kuifanya Tanzania kuwa ya uchumi wa kati.