KONA YA MAKENGEZA : Mwenye kupinga mipango atapanguliwa na mapanga

Muktasari:

  • Sasa kwa kuwa nilikuwa nimetafuta gesti ya bei nafuu (unajua sisi waandishi hatuna chetu dunia hii … au maandishi yetu hayapendwi hivyo hakuna anayenunua).
  • Kwa hiyo, yule aliyepiga buti akashtuka mguu umepasua mlango badala ya kuufungua hivyo akabaki anarukaruka na mguu mmoja huku akijaribu kutoa mguu kwenye mlango.

Juzi mchana nilikuwa nimekaa kwenye gesti niliyokuwa nimepanga kwa muda (maana Makengeza hapendi kukaa mji huu daima dumu). Nilipokuwa naandika makala yangu niliposikia mlango ukipigwa buti kwa nguvu.

Sasa kwa kuwa nilikuwa nimetafuta gesti ya bei nafuu (unajua sisi waandishi hatuna chetu dunia hii … au maandishi yetu hayapendwi hivyo hakuna anayenunua).

Kwa hiyo, yule aliyepiga buti akashtuka mguu umepasua mlango badala ya kuufungua hivyo akabaki anarukaruka na mguu mmoja huku akijaribu kutoa mguu kwenye mlango.

Nilishtuka lakini ilibidi nijizuie nisicheke maana alivyokuwa anarukaruka, huku akijaribu kujinasua ubabe wake wote ule ulionekana feki. Ndiyo shida ya ubabe, lakini kabla sijasema neno akaingia bosi wake.

“Hmm, mwingine tena. Kazi yake ni kukaa tu, mchana kutwa. Wakati sisi tunahangaika kujenga taifa, yeye kazi yake kulala na kula starehe. Yuko wapi mwanamke?”

‘‘Hakuna mwanamke. Kazi yangu ni uandishi na mimi najaribu kuandika makala yangu kwa ajili ya kesho. Sasa naomba mniache niendelee na kazi yangu.’’

‘‘Mwongo mkubwa. Nani atafanya kazi kwenye gesti? Au tuseme gesti kuna kazi moja tu. Yupo wapi mwanamke?’’

Wakati huu yule mwenzie hatimaye alikuwa amefanikiwa kutoa buti kwenye mlango na alikuwa anazungukazunguka, mara aangalie kwenye kabati, mara chini ya kitanda, mara nyuma ya mlango. Licha ya hali ya hatari mbele yangu, nilishindwa kujizuia kucheka.

‘‘Unacheka nini mzururaji mkubwa? Nyinyi ambao mnakuja kwetu Bongo kufaidi jasho letu watu wa jiji hili tukufu. Pumbafu.’’

Akanipiga kofi kisha nikapelekwa mzobemzobe hadi gari la polisi licha ya jitihada zangu zote za kujieleza.

Kisha nikapandishwa humo na teke la nguvu. Kufika kituo cha polisi, nikapelekwa kwa kamanda wao. Baada ya mabishano ya muda mfupi, akatambua kwamba kweli mimi mwandishi, kweli nilikuwa nimekaa gesti kuandika makala yangu huku nikisubiri mkutano wa kesho yake.

Nilitaka kulalamika kwamba misako ya namna hii inawasumbua wasio na hatia. Kwa nini wasiwafuate wale wanaoshukiwa tu.

‘‘Wote mlioko gesti mnashukiwa nukta! Na sisi ni sisi. Ndiyo maana tunaweza kufanya tupendalo.’’

Katika hali hiyo utasema nini kwa hiyo nikanyamaza nikitafakari kwa nini polisi katika nchi nyingine wanapenda kujiita watoa huduma siyo jeshi. Lakini wakati natafakari hivyo nikashtuka jamaa aliamua kunipa ushauri.

‘‘We bwana mdogo nasoma makala zako. Ufyatu mtupu. Hatari tupu.’’

Nikacheka.

‘‘Usicheke. Makengeza ya nini katika dunia ya leo?’’

‘‘Sasa afande, hujui wanasema kwamba kalamu ina nguvu kuliko panga au jambia?’’

‘‘Upumbavu. Wanajidanganya. Kama huniamini, jaribu kuandika baada ya kukatwa mkono na panga. Tena siku hizi ni enzi za risasi na mabomu. Unaweza kutunguliwa bila hata kumwona mwenye panga. Eti kalamu. Wapi na wapi?’’

‘‘Lakini umoja na nguvu ya wananchi hujengwa na mawazo yanayotokana na kalamu.’’

‘‘Labda katika enzi zingine lakini siyo sasa. Iwapo wenye mapanga hawataki kusoma, kalamu itapata nguvu wapi? Na huu ni wakati wa mapanga. Tuna mipango yetu na wenye kupinga wataonja mapanga tu. Iwapo sisi ni wateule wa Mungu wenye mawazo sahihi, wewe ni nani kutumia kalamu kupinga? Ibilisi!’’

‘‘Sijasema kwamba ni lazima sisi wenye kalamu tuwe na mawazo mazuri zaidi kuliko wenye mapanga. Aliyepanga kupangua kwa panga anaweza kuwa na mawazo mazuri zaidi hata kama anaamua kutumia upanga kuwamaliza wengine asiokubaliana nao. Lakini kupangua kwa panga ina hatari.’’

‘‘Mmmh! Hata kama mawazo yako ni mazuri namna gani, kalamu haina nguvu isiposimama juu ya panga. Mwenye panga akishapanga kutumia panga, hana haja hata kumwangalia mwenye kalamu hivyo tutakata kalamu yako vipandevipande.’’

‘‘Sawa afande, lakini mwenye kalamu anaweza pia kujaribu kuwashawishi mashabiki wa wenye mapanga waone kwamba labda mawazo yake yana maana pia.’’

‘‘Ndiyo maana hatuwapendi. Kwani mwandishi ni mteule wa Mungu? Mwandishi amechaguliwa na watu? Unakaa tu katika gesti yako ya hovyohovyo na kuwachochea watu dhidi ya waliowachagua badala ya kutumia kalamu yako kuwasifia wateule.’’

‘‘Lakini inawezekana mawazo yangu yanafanana na yale ya wengine waliochaguliwa tofauti ya wateule wa upande mmoja.’’

Kamanda akakunja uso.

‘‘Uchochezi mtupu. Wewe ngoja tu. Wewe na kalamu yako na wao na kelele zao, hivi karibuni tutawatangaza kwamba siyo raia wa nchi yetu ya Bongo. Wananchi walikosea kwa kuwachagua, ndiyo maana itabidi waadhibiwe kwa makosa yao.

‘‘Lakini afande siwachochei. Uchambuzi, uyakinifu ni msingi wa maendeleo. Na huu unapatikana kwa kuhimiza na kufurahia mawazo mbadala. Hujui hadithi ya vipofu na tembo. Kila mtu aliona sehemu nyingine na picha kamili inapatikana ukiunganisha maoni ya wote. Ungetegemea mawazo ya kipofu mmoja tu, tembo asingeeleweka.

Kamanda akacheka.

‘‘Ha ha ha ha. Umepitwa na wakati Bwana. Hakuna haja ya maoni yao maana wameshalaliwa na tembo tayari. Wataona nini wakati tayari ni chapati?’’

‘‘Duh!’’

‘‘Naam. Ujue kwamba watu wetu wengi wakishaona mapanga, wamefurahia mmeremeto wa panga. Ngoma za vita zikianza kupigwa, miguu ya watu inashindwa kutulia na wanajikuta wameamka na kuanza kucheza ngoma tena kwa mwendokasi kuliko mpiga ngoma mwenyewe. Sasa umeona wapi anayecheza ngoma anasoma vimakala vyako huku anacheza.’’

‘‘Sikatai. Huko nyuma watu waliomba kutawaliwa na mapanga badala ya mipango na sasa bado wanafurahi mmeremeto wa panga na hata ukali wake, maana kila mtu anafikiria ukali wa panga ni kwa ajili ya wengine siyo kwa ajili yao.’’

‘‘Sawasawa. Sisi tunajua tuko sahihi na haturudi nyuma. Huoni kwamba nia yetu ni njema katika kunoa mapanga?’’

‘‘Unaweza kuwa na nia safi bado unoe katika mipango siyo mapanga tu.’’

‘Unaona. Maneno tu, maneno tu. Huu si wakati wa maneno. Ni wakati wa vitendo. Mungu yuko nasi ndiyo maana ni dhahiri kwamba anayepinga mapanga yetu ni adui, msaliti, haini, gaidi, muuaji, mbakaji na amelaaniwa na Mungu. Hatutaki mawazo mbadala. Tunataka kusonga mbele na atakayetuzuia, hata akiwa amechaguliwa na wananchi kwa makosa naye atapambana na panga letu.

‘‘Lakini mbona haikuwa hivyo huko nyuma. Kulikuwa na hali ya ubaba, siyo ubabe.’’

‘‘Maneno tena.’’

‘‘Siyo maneno. Kwa nini mlishinda safari hii? Unafikiri Mungu akadondosha karatasi za kura. Mlishinda kwa sababu wenzako walizunguka nchi nzima, bila hata panga mkononi. Wakafanya kazi na wananchi, wakawasikiliza hadi watu wakaona kwamba bado mnastahili kuchaguliwa. Ubaba huleta ushindi wa kudumu siyo ubabe.’’

‘‘Enzi zile zimepita. Ubabe tu utamaliza kila kitu.’’

‘‘Sawa afande, lakini ujue kwamba kutawala kwa ubabe hakuna usalama maana watu watanyamaza kweli, lakini huwezi kujua wanafikiria nini. Ndiyo maana itabidi kutumia panga zaidi na zaidi.’ Ghafla yule kamanda akaamka na panga.

‘Na nikunyamazishe na wewe. Akaanza kunifukuza hadi nikaanguka na kujikuta niko sakafuni pembeni mwa kitanda. Ndoto gani hii jamani!