MAONI: NCCR-Mageuzi inavyojikokota nyuma ya kivuli cha Ukawa

Muktasari:

Chama hiki kilikuwa na nguvu kubwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 kwani aliyekuwa mgombea wake wa urais, Augustine Mrema alipata asilimia 28 ya kura zote za urais. Ulikuwa mwanzo mzuri.

NCCR-Mageuzi ni chama chenye historia ya aina yake katika ulingo wa siasa nchini, pengine kuliko vyama vyote vya upinzani tangu kuanza kwa mfumo wa uchaguzi unaovihusisha vyama vingi vya siasa.

Chama hiki kilikuwa na nguvu kubwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 kwani aliyekuwa mgombea wake wa urais, Augustine Mrema alipata asilimia 28 ya kura zote za urais. Ulikuwa mwanzo mzuri.

Baada ya uchaguzi huo chama hicho kimekuwa kikiporomoka kwa kasi ya kutisha. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 kilipata wabunge 19, ila katika uchaguzi kama huo miaka mitano baadaye kiliambulia mbunge mmoja tu, Kifu Gullamhussein, ambaye alikuwa mbunge kwa takribani miaka miwili tu.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2005, NCCR kiliweka mgombea urais, Dk Sengondo Mvungi (marehemu), lakini licha ya kushindwa pia hakikuweza kupata mbunge hata mmoja. Uchaguzi wa mwaka 2010, walau kiliibuka na kupata wabunge wanne.

Tatizo ni kwamba wabunge hao wote walikuwa katika mkoa wa Kigoma na mbaya zaidi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, mmoja alihamia ACT-Wazalendo na watatu kushindwa katika uchaguzi huo.

Katika Uchaguzi huo chama hicho kiliambulia mbunge mmoja tu, James Mbatia ambaye wananchi wa jimbo la Vunjo walimchagua kuwa mwakilishi wao bungeni.

Naelewa kuwa vyama vingi vya upinzani vinakabiliwa na ukata, lakini ukata huu ndiyo ukifanye chama kishindwe hata kufanya mikutano mikubwa walau miwili tu kwa mwaka?

Licha ya kuwa Rais John Magufuli amepiga marufuku mikutano ya hadhara mpaka mwaka 2020, lakini NCCR kimekuwa kimya hata kukemea tamko hilo (kama kweli si sahihi), kama ilivyo kwa washirika wake, Chadema na CUF, ambao kwa pamoja wameunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Chama hakiwezi kujijengea jina kwa kukazania kutoa taarifa na kuzungumzia hoja mbalimbali za kitaifa katika mikutano na waandishi wa habari.

NCCR wako wapi? Mbona katika harakati za kufanya mikutano ya hadhara au maandamano kinaonekana CCM, CUF na Chadema tu?

Juzi tumemsikia mwenyekiti wa NCCR, Mbatia akiunga mkono Operesheni Ukuta ya Chadema, hata hivyo amechelewa kuchukua uamuzi huo.

Tuliziona operesheni Sangara ya Chadema na ile operesheni Zinduka ya CUF kwa ajili ya kujenga vyama hivyo na kutangaza sera, ila NCCR hawakuonekana.

Kwanini chama hiki kina mtandao mpana Kigoma na siyo Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Dodoma pamoja na mikoa mingine?

Chama hiki tangu mwaka 2005, licha ya kufanyika kwa chaguzi ndogo zaidi ya tano, hakijawahi kusimamisha mgombea kwa madai kuwa kitamuunga mkono yeyote wa upinzani kama watakubaliana na chama husika.

Pamoja na kumbukumbu hiyo na mengine ya hivi karibuni, sidhani kama huo ndiyo msimamo wa chama kinachotaka kuchukua dola.

Pamoja na kuwa nyuma ya Ukawa, chama kinapaswa kuwa na mikakati yake ya kujiimarisha.

Mathalani Chadema kimeibuka na mkakati wake wa Ukuta na kufanya maandamano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi mwaka huu, kupinga kile wanachokiita ‘utawala usiozingatia Katiba na sheria za nchi’.

Chama cha siasa lazima kisikike, lazima kiwe na harakati za kujipanua na kujijenga kuanzia ngazi ya shina na kwa wanaojua maana ya kujijenga, hawakushangazwa na mkakati wa Chadema kuanza kujiimarisha vijijini, baada ya kutawala mjini.

Katika uchaguzi wa mwaka jana, CUF kimefanya vyema Tanzania Bara kwa kupata wabunge 10. Hayo ni matunda na kujenga chama na kutokubali kufanya siasa za matamko.

Askari kawaida husonga mbele na hata mkulima wa kweli hata siku moja huwezi kumwona akichagua jembe. Wagombea kugawana kura ni jambo la kawaida kwa kuwa unaposhindana kuna kushindwa na kushinda.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alipobaini kuwa wananchi wameanza kupoteza imani na chama hicho tawala, alifanya ziara karibu nchi nzima.

Ndani ya miaka mitatu tangu aliporejea tena CCM kama Katibu Mkuu, Kinana alifanikiwa kukirejesha CCM katika ramani walau sasa chama hicho kinaanza kuzungumzwa kwa mazuri yanayochangiwa na kasi na mwenyekiti wake, Rais John Magufuli.

Chama kukaa nyuma ya hoja ya chama kingine ni kujimaliza, chama kukubali kumezwa na muungano na vyama vingine kwa ajili ya kudai jambo fulani ni kujimaliza.

Fidelis Butahe ni mwandishi wa gazeti hili anapatikana kwa baruapepe: [email protected] na simu namba 0754 597315