Namna ushirikiano wa wabunge ulivyotoa somo kwa wananchi

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (katikati) akiwaeleza jambo Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga (kushoto) na Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilango walipokuwa wakielekea kuhudhuria kikao cha Bunge, mjini Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman

Muktasari:

Katika Bunge la 11, kuna jumla ya wabunge 391 wakiwamo wa majimbo 263, viti maalumu 113, wa kuteuliwa na Rais wanane huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiongoza kwa idadi kubwa ya wabunge.

Ni nadra wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuungana pasipo kujali itikadi za vyama vyao, lakini katika mkutano wa 10 yapo mambo matatu yaliyowaunganisha.

Katika Bunge la 11, kuna jumla ya wabunge 391 wakiwamo wa majimbo 263, viti maalumu 113, wa kuteuliwa na Rais wanane huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiongoza kwa idadi kubwa ya wabunge.

Kitakwimu, CCM ina wabunge 274 na upinzani ambao unajumuisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Chama cha Wananchi (CUF), ACT- Wazalendo na NCCR-Mageuzi, vikiwa na wabunge 116 wakiwamo wa viti maalumu.

Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa vyama vinne vyenye wabunge ndani ya Bunge, lakini katika mkutano wa 10, wabunge hao waliondoa tofauti zao na kuungana katika masuala matatu makubwa.

Masuala hayo ni pamoja na wakati wa mjadala juu ya uhalali wa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, kuamuru kuwekwa mahabusu kwa viongozi wa kisiasa na watumishi wa umma.

Suala lingine lililowaunganisha wabunge ni wakati wa kujadili na kupitisha maazimio dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti kwa kudhalilisha hadi ya Bunge.

Jambo lingine ambalo lilionekana ni jipya kwa kiasi fulani katika mkutano wa 10, ni hatua ya wabunge kugawana muda wa dakika 10 anaopewa mbunge, ambapo waliachiana pasipo kujali vyama vyao.

Kazi ya mbunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba yetu, ni kumuuliza waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake.

Nyingine ni kujadili utekelezaji wa kila wizara wakati wa mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti, kujadili na kuidhinisha mpango wa muda mrefu na mfupi na kutunga sheria mbalimbali.

Hata hivyo, bahati mbaya katika baadhi ya mijadala wabunge wamekuwa wakigawanyika katika misingi ya kiitikadi badala ya kutimiza wajibu wao wa kikatiba wa kuisimamia na kuishauri Serikali.

Mijadala ndani ya chombo hicho wakati mwingine inatawaliwa na ubishani uliojaa kejeli, vijembe na wakati mwingine kuwa nje ya hoja, ilimradi tu kila upande ukitaka kuonyesha ndio wenye haki.

Katika mambo hayo matatu niliyoyaeleza hapo awali, wabunge walishikamana na kuzungumza kwa sauti moja na hii ndiyo ambayo wananchi wengi wangetamani Bunge liwe hivyo wakati wote.

Ilikuwa ni kama wabunge waliziacha itikadi zao walipoingia ndani ya ukumbi wa Bunge, walijadili na kufikia hitimisho wakitanguliza mbele utaifa, uzalendo na masilahi ya wale wanaowawakilisha.

Mjadala ya Makonda na Mnyeti

Awali akiwasilisha hoja yake bungeni, Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alisema vitendo vilivyofanywa na wateule hao wa Rais vinakiuka Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.

Mbunge huyo alifafanua kuwa Makonda wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alisema wabunge huwa wanakwenda bungeni kusinzia, kauli ambayo inakiuka haki za Bunge.

Kwa mujibu wa Waitara, Mnyeti baada ya Bunge kujadili hoja ya wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa, kuwasweka rumande viongozi wa siasa, mkuu huyo wa wilaya aliwaita wabunge wapuuzi.

“Baada ya Bunge kupitia azimio ilionekana video clip kwenye mtandao wa Facebook wa Mnyeti akisema: “Huu ni upuuzi mtupu, wabunge hawa hawajielewi na washauri mfanye kazi zenu.”

“Haya mambo ndiyo ambayo yamejirudia wakati nikiangalia Clouds Tv ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akisema sisi humu bungeni tunasinzia maana yake tunalala humu,”alisema.

“Mheshimiwa mwenyekiti ukisoma Katiba ibara ya 63(2) inasema hili Bunge ndiyo chombo kikuu kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali. Lakini sisi ndiyo tunawapitishia bajeti,”alisisitiza.

“Bunge linaingia katika majaribu makubwa ya kudharauliwa, kusiginwa haki zake ., inawezekanaje kamati ya Bunge inajadili lakini DC anasema hawa ni wapuuzi na RC anasema hawa wanasinzia”.

Mbunge huyo alisema Makonda alienda mbali na kuwapigia simu baadhi ya wabunge akiwaambia hawamtishi wala hawambabaishi akisema hiyo inakiuka sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge.

“Kwenye taarifa hii hatukumtaja mtu yeyote lakini yeye (Mnyeti) kwa kujishuku na kujihisi akaenda hadharani kwenye mitandao ya kijamii na akasema sisi ni wapuuzi,” alisema Waitara.

Mbunge wa Ulyanhusu (CCM), John Kadutu alipendekeza wateule wa Rais wawe wanachujwa bungeni baada ya kuteuliwa kama inavyofanyika Marekani ili wabunge wawachuje.

Pia, alishauri Bunge kubadili lugha ya “Bunge linaishauri Serikali” na badala yake litumie kauli kali zaidi ya “Bunge linaazimia” hatua zichukuliwe dhidi ya mtu anayechezea hadhi ya mhimili huo.

“Hatuwezi kukubali Mkuu wa Mkoa haheshimu Bunge. Mkuu wa Wilaya haheshimu Bunge. Mimi sijawahi kuona. Wapo watu wanafikiri wapo juu yetu, hapana mwenyekiti.

“Ifike mahali hawa watu tuwawajibishe. Ifike mahali Bunge liwe linaazimia watu watumbuliwe huko. Bunge lifike mahali sasa tuazimie, likisema Bunge linaishauri serikali hii ni lugha nyepesi.

“Lazima lugha ibadilike na iwe Bunge linaazimia huyu atolewe kazini. Hatuwezi kujenga Serikali ya watu wenye kiburi. Haiwezekani watu wafanye kiburi kwa Bunge.

“Mimi napendekeza lazima lugha ya Bunge ibadilike wakati mwingine tusiwe na lugha nyepesi ya kusema Bunge linashauri. Unapotaka kulitoa pepo mheshimiwa pepo halibembelezwi,” alisisitiza.

Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya (Chadema) alisema Makonda alipita tu Umoja wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), lakini hakupikwa kuwa kiongozi mzuri wa kisiasa anayeweka akiba ya maneno.

“Hivi karibuni vijana wanaoaminiwa nasikitika sana wanatumia madaraka yao vibaya. Wengine wanaenda mbali zaidi na kusema tupo karibu na bwana mkubwa tutaendelea kuwachafua.

“Hivi tunavyoongea, wakati tunajadili mjadala wa kamati ya Ukimwi, RC Makonda alinipigia simu na kunitisha kwamba yeye yuko karibu na bwana mkubwa atatushughulikia sisi wabunge,” alisema.

“Alisema ataanza na Msukuma (Joseph), ataenda kwa Halima Mdee, kwa Esther Bulaya, Sugu (Joseph Mbilinyi) na Mchungaji Peter Msigwa na akampigia pia Ester Matiko,” aliongeza kusema Bulaya.

“Amesema mnashangaa (wabunge) nini yeye kwenda Marekani na alimpigia simu hata Esther Matiko na kumwambia ameshakaa Ufaransa sana hakuna wa kumtisha”.

“Makonda alipita tu UVCCM hakutengenezwa kuwa kiongozi mzuri. Haiwezekani umepewa mamlaka halafu unafika kwenye mkutano wa hadhara unampigia simu kiongozi wa nchi unamweka hadharani”.

“Unaweka loud speaker (sauti) ni dharau kubwa sana. Hatutakubali Bunge lidhalilike, lakini hatutakubali kama kiongozi mkuu naye akadhalilika kwa kuwekwa loud speaker kwenye mikutano”.

Mbunge wa Ubungo, Saidi Kubenea (Chadema) alisema wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kwa sasa wamegeuka kuwa polisi na hapo hapo mahakimu ambapo uamuru watu kukamatwa.

“Bunge hili limejengwa kwa nguvu kubwa sana na kuwa na hadhi ya juu. Ni lazima heshima ya Bunge ilindwe kwa gharama yoyote,” alisema na kufichua namna anavyowagonganisha wabunge na rais.

“RC Dar anawapigia simu wabunge akiwataja mawaziri kuwa ndiyo wanaowatuma wabunge wamtukane yeye. Mmoja wa Mawaziri ni Nape Nnauye,” alisema na kuongeza: “Huyu mkuu wa mkoa anagombanisha Serikali na Bunge. Anajenga fitina kati ya Rais na Waziri Nape. Anajenga fitina kati ya wananchi na wafanyabiashara na anajenga fitina kati ya wabunge na wananchi”.

“Kwa heshima kabisa nakubaliana na hoja hii. Naunga mkono waletwe kwenye kamati ya kinga, haki na madaraka ya Bunge ili washughulikiwe bila kuangalia sura ya mtu,” alisisitiza Kubenea.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM), aliunga mkono hoja ya Kubenea kuwa mkuu huyo wa mkoa ndiye anayewachonganisha wafanyabiashara na Rais.

“Tension iliyopo Dar es Salaam si ya kawaida. Haiwezekani RC anafanya kazi za intelijensia, RPC (Kamanda wa Polisi) au RSO (Mkuu wa Usalama wa Taifa) atafanya kazi gani?” alihoji Msukuma na kuongeza:

“Halafu baadaye anakuwa na kiburi cha kusimama na kulijibu Bunge. Serikali ni ya wananchi na wabunge waliopo humu wameletwa na wanachi kwanini tutukanwe.”

Mbunge huyo alienda mbali na kupendekeza Kamati ya Uongozi ya Bunge ikutane kwa dharura na kutoa tamko kali huku akihoji “Makonda ni nani katika hii nchi? Kama Jairo alitoka Makonda ni nani?”

David Jairo alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na aliwahi kuazimiwa kuwajibishwa na Bunge na baadaye Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alimuondoa katika wadhifa huo.

Baada ya kukamilika kwa majadiliano hayo, Chenge aliwauliza wabunge wanaoafiki waseme ndiyo na ndipo sauti zilisikika “ndiyoooo” alipouliza wanaosema “Siyo” Bunge zima likawa kimya.

Hoja ya Ma-Rc, DC ilivyowaunganisha

Hoja ya wakuu wa mikoa na wilaya kuwasweka na kuwatolea maneno makali kwa watendaji ilizua mjadala bungeni huku wabunge bila kujali tofauti zao za kiitikadi waliungana pamoja.

Mbunge wa Kinondoni, Mohamed Mtulia (CUF) alisema watendaji wa Serikali wanashindwa kuelewa kauli za Rais jambo ambalo linawafanya watekeleze maagizo yake tofauti na dhamira yake.

Alitoa mfano wa kauli ya kutaka vyombo vya usafiri vitakavyopita katika barabara za mwendo kasi Jijini kung’olea matairi, akisema Rais alimaanisha wachukuliwe hatua za kisheria ili kuepuka madhara.