Nampenda Raila lakini naguswa sana na Uhuru

Muktasari:

  • Uhuru na Raila wana historia tofauti, lakini kwa kiasi kikubwa wote wawili wamezaliwa kwenye familia za wazee ambao wamewahi kushikilia madaraka makubwa sana ya kisiasa nchini Kenya. Wote wawili wamewahi kufanya kazi kwenye chama kimoja kama viongozi na wamewahi kufanya kazi kwenye vyama tofauti kama viongozi. Wote wawili wana sifa za kupenda sana demokrasia.

Moja ya mambo ambayo hutokea sana kwenye Nyanja za siasa ni ufuasi. Wanasiasa wote wakubwa na wadogo huwa na watu wanaowaunga mkono au kuwapinga. Leo nawafanyia uchambuzi wanasiasa wawili wa Kenya, Raila Odinga na Uhuru Kenyatta. Lengo la makala hii siyo kupitia sifa zao tu, kwa kiasi kikubwa ni kuonyesha namna gani masuala ambayo Raila na Uhuru wanayafanya au kuyasimamia yana mafunzo mengi kwa wanasiasa wa Tanzania na siasa za maendeleo za Afrika Mashariki.

Uhuru na Raila wana historia tofauti, lakini kwa kiasi kikubwa wote wawili wamezaliwa kwenye familia za wazee ambao wamewahi kushikilia madaraka makubwa sana ya kisiasa nchini Kenya. Wote wawili wamewahi kufanya kazi kwenye chama kimoja kama viongozi na wamewahi kufanya kazi kwenye vyama tofauti kama viongozi. Wote wawili wana sifa za kupenda sana demokrasia.

Raila Odinga

Nampenda sana Raila kwa sababu ni mwanasiasa mwenye mafanikio makubwa sana kimsimamo. Masuala ambayo huyasimamia yakitetereshwa hufanya maamuzi ya haraka ya kutengana na msimamo mpya asiouamini. Nimewahi kuandika nikielezea alivyowahi kuhama vyama kadhaa ili kulinda msimamo wake na au mwelekeo wake kisiasa. Katika uhamaji ule kwa kweli Raila hakuwa tu anahama ili kutafuta madaraka – alikuwa anahama pamoja na madaraka lakini ni kujaribu kutaka kupigania kitu ambacho alikuwa anataka kiwe, na hasa masuala ya katiba na haki za Wakenya.

Raila, kila mara alipoona anashindwa kufikia malengo yake mahali, alikwenda mahali pengine na kuongoza mapambano ya kusaka kile anachokisimamia. Wanasiasa wengi wa Tanzania wanapohama kwenye vyama vya zamani kwenda vipya, huenda huko na kukaa kimya, na kufuata kila kilichoko huko – ndiyo, nidhamu za kivyama zinataka sana watu kuzungumza masuala ya chama kwa utaratibu maalum na kwa kiasi kikubwa kutetea chama, hilo linafahamika – lakini chama hakikatazi mwanachama au kiongozi wake kusimamia masuala mema aliyoyaamini.

Mathalani, kama ulikuwa mwanasiasa wa chama cha DP na sasa umehamia UDP, kama ulikuwa unapigania haki za watoto pale DP – kwa nini ukifika UDP unakaa kimya? Kwani haki za watoto zimepatikana? Raila anatufundisha kusimamia ajenda. Raila alipoona chini ya Kanu Kenya haiendi sawa na akajiridhisha kuwa moja ya mambo yanayoirudisha nyuma Kenya ni ukosefu wa katiba mpya na imara – aliendelea na mchakato wa kupigania Katiba mpya ya Kenya hata nje ya Kanu na alifanikiwa kuikwamisha Kanu.

Mapambano ya kudai Katiba itakayoleta uimara wa nchi na utendaji wake ni suala ambalo linamtangaza Raila na kumpa heshima kubwa sana Kenya na duniani. Mwanasiasa huyu ndiye mhimili mkubwa wa demokrasia ya Kenya na amepitia matatizo mengi sana katika kuishi maisha ya kuitafuta Kenya ambayo itaongozwa kitaasisi na amepigana na kufanya hatua zote hizi akiwa katika vyama zaidi ya kimoja, akiwa gerezani na akiwa ndani ya serikali kama kiongozi.

Raila amepata kuwa Waziri Mkuu wa Kenya baada ya machafuko ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 akifanya kazi chini ya Rais Mwai Kibaki kwenye serikali ya umoja wa kitaifa. Bila kujali kuwa alikuwa serikalini na chini ya Kibaki, Raila aliendelea kupaza sauti na kushikilia ajenda yake ya Kenya kuwa na Katiba mpya, demokrasia imara, utawala wa sheria, ulinzi wa haki za binadamau, uwazi na uwajibikaji na utawala bora. Ajenda hizi Raila hajaziacha na nina uhakika hata akifa zitasindikizana naye kaburini.

Somo kubwa analotoa Raila kwa wanasiasa wa Tanzania ni kuenzi misimamo yao hata wanapokuwa kwenye vyama vipya. David Kafulila amehamia CCM mathalani, hapaswi kabisa kuachana na ajenda yake ya kupambana na ufisadi – na awe mkali kama pilipili hata pale anapogundua kuwa chama chake kipya kimeshiriki kwenye ufisadi fulani au kimekalia kimya ufisadi fulani au chama chake cha zamani kimefanya ufisadi fulani au kimeshindwa kuibana serikali kuhusu ufisadi fulani.

Kafulila ni mfano tu lakini lengo ni kuwakumbusha wanasiasa kwamba mambo mazuri waliyowahi kuyapigania na bado yanahitajiwa na taifa letu leo, wanapaswa kuendelea kuyapigania bila kujali wako kwenye chama kipi au wamehamia wapi. Kukaa kimya au kutulizwa unapohamia kwenye chama kipya na kuacha kabisa kusimamia masuala makubwa ya kitaifa kwa sababu yoyote ile, ni usaliti mkubwa kabisa na ndiyo unafanya wanasiasa wanaohama vyama kuitwa wasaliti.

Uhuru Kenyatta

Uhuru Kenyatta amejitanabaisha kama mwanademokrasia. Baba yake, mzee Jomo Kenyatta hatajwi kama mwanademokrasia. Na demokrasia tunayoizungumzia ni ile iliyomo kwenye sheria na katiba zetu na ile ambayo dunia inatarajia kuiona kutoka kwa wanasiasa wote. Yako mambo mengi sana yanayoonyesha kuwa Uhuru siyo mchokozi, ni mtulivu na anapenda sana kuheshimu haki za watu na makubaliano yaliyopo. Uhuru ni mfano halisi wa kiongozi mwenye mamlaka na ambaye bado anaamini wako watu wana haki kushinda hata mamlaka yake.

Naposema hivi kuna watu wanaweza kujiuliza, mbona Uhuru ameyaacha majeshi yake yakawapiga na kuwaumiza waandamanaji hivi karibuni huku akichukua hatua zingine kadhaa za kudhibiti utulivu nchini mwake na zingine zimekuwa na madhara? Jibu ni rahisi sana – walau kwa Kenya, matumizi ya nguvu za polisi yanadhibitiwa kwa kiasi fulani kuliko nchi zingine na uwezekano wa hili kutendeka lazima umuendelee Rais wa nchi.

Uhuru ndiye amiri jeshi mkuu wa majeshi ya Kenya na ndiye anayapa amri. Lakini, sheria na katiba ya Kenya vimeweka utaratibu wa namna ambavyo majeshi yatatekeleza wajibu wao kiweledi na bila kutumia nguvu kubwa sana – na hilo limekuwa likifanikiwa. Hivi karibuni kuna mtoto wa miaka 7 alipigwa risasi na polisi, akauawa! Vitendo vya namna hii haviwezi kumuhusu amiri jeshi mkuu, vinahusu weledi wa polisi wanapokuwa kazini na kwa kweli kama polisi wangekuwa wanataka kuua watu wangeliwaua kwa idadi kubwa zaidi nchini humo.

Kilichofanya watu wengi wasiuawe ni uwezo mkubwa wa kidemokrasia wa Uhuru. Hata polisi wa Kenya walipojaribu kuzuia shughuli za siasa na maandamano ya vyama vya upinzani, Uhuru aliingilia kati na kusisitiza lazima polisi wawalinde waandamanaji hata kama waandamanaji hao wanampinga yeye na kuchaguliwa kwake. Siyo rahisi kwa Afrika kupata marais wenye fikra za kidemokrasia namna hii.

Nchi nyingine za Afrika Mashariki kuna matumizi mabaya sana ya madaraka na kwa kweli marais wa nchi ndiyo hutoa maagizo ya kuzuia shughuli za vyama vingine pamoja na kuwadhibiti wanasiasa wa vyama vingine. Tumekuwa na mifano mingi sana ya udhibiti huo kutoka Tanzania, Uganda, Rwanda na Burundi. Ni rahisi kusema kuwa wakuu wa nchi hizo hawaamini katika demokrasia na wao hawayaishi maisha ya Uhuru Kenyatta.

Pamoja na marais hawa wengine kutoyaishi maisha ya Uhuru Kenyatta, wanalo kubwa la kujifunza. Wao kama alivyo Uhuru wote wameendeleea kuwa wakuu wa nchi na wakiheshimiwa sana ndani na nje ya nchi zao. Uhuru Kenyatta amefanya makosa kadhaa kwenye utawala wake, lakini ameionyesha Afrika kuwa mtu anaweza kuwa na madaraka makubwa kushinda wote katika nchi yake, lakini bado akayatumia madaraka hayo kwa faida ya watu wote.

Katika bara la Afrika, siyo rahisi mtu au watu wakaandamana kupinga kuchaguliwa kwa rais wa nchi yao. Watu hao watakutwa mochwari. Kenya inatuonyesha kuwa kila mtu anaweza kupingwa. Mahakama ya Kenya hivi karibuni ilituonyesha kuwa mhimili wa serikali siyo mkuu kuliko mingine na unaweza kudhibitiwa na mahakama au bunge na ukarudishwa kwenye utaratibu. Lakini yote haya yanawezekana katika dunia ya Kenya, chini ya Uhuru Kenyatta – mwanademokrasia wa mfano katika ukanda wetu.

Raila na Uhuru ni shamba darasa

Natambua Raila na Uhuru watastaafu siasa baadaye, yako mambo mengi wameyaacha na watakumbukwa sana kwa sababu ya mambo hayo. Kama kuna jambo ambalo viongozi wengi wa Afrika husahau wawapo madarakani, ni kuandaa kesho yao. Ni kujiuliza, Je, kesho ntakuwa kama Mandela, Nyerere, Nkrumah?

Wanasiasa wote wa Afrika na hasa Tanzania, wale walioko chama kinachoongoza dola, wanaweza kuendelea kujiuliza, je, kesho ntakuwa Uhuru Kenyatta au Raila Odinga? Je ntakuwa Raila ambaye amepigania mabadiliko ya kimfumo ya Kenya bila kuchoka na kwa kutumia majukwaa tofauti bila kuogopa wala kukata tamaa? Au ntakuwa Uhuru Kenyatta ambaye pamoja na kuwa na madaraka ya mkuu wa nchi, hatujasikia hata akimtishia maisha au kumkamata na kumfunga Raila Odinga.

(Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtafiti, Mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi CUF. Simu; +255787536759 (Whatsup, Meseji na Kupiga)/ Barua Pepe; [email protected])