Ni wakati wa wapinzani kutafakari upya mbinu zao

Muktasari:

Kwanza, ni ukweli kwamba wanachama wa vyama vya siasa Tanzania ni wachache, ukilinganisha na idadi ya wananchi wote walio na umri wa kupiga kura. Huenda wanachama halisi, achilia mbali mamluki wanaonunuliwa kadi ili wawapigie kura wagombea fulani kipindi cha uchaguzi wa ndani ya vyama, hawafiki hata asilimia 10 ya wapigakura wote.

Ili vyama vya siasa vya upinzani viendelee kuishi katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, vinapaswa kufikiria upya mikakati yao. Kabla ya kupanga mbinu yafaa wazingatie mambo kadhaa muhimu.

Kwanza, ni ukweli kwamba wanachama wa vyama vya siasa Tanzania ni wachache, ukilinganisha na idadi ya wananchi wote walio na umri wa kupiga kura. Huenda wanachama halisi, achilia mbali mamluki wanaonunuliwa kadi ili wawapigie kura wagombea fulani kipindi cha uchaguzi wa ndani ya vyama, hawafiki hata asilimia 10 ya wapigakura wote.

Pili, katika idadi ya wanachama wa vyama vya siasa, sehemu kubwa ni wale wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho licha ya kushuka umaarufu wake hususan katika awamu iliyopita, kimejijenga vyema na kujivunia mtandao mpana mijini na vijijini. Hii maana yake ni kuwa idadi ya wanachama wa vyama vya upinzani ni ndogo ukilinganisha na wale wa CCM na idadi ya wananchi waliopo.

Vilevile, hamasa ya kisiasa miongoni mwa wananchi siyo kubwa kiasi cha kuwategemea kufanya kila wanachoagizwa na viongozi wao, hususan agizo hilo likigusa mambo ya uasi na mapambano dhidi ya dola.

Nataja mambo haya yote kuonyesha ugumu wa kazi inayoukabili upinzani katika mapambano yao dhidi ya siasa zisizo rafiki kwa demokrasia za Rais Magufuli.

‘Jeshi’ lao ni dogo mno kufanya mapambano ya moja kwa moja dhidi ya dola hususan katika kipindi hiki ambacho imani ya wananchi wengi kwa CCM na Serikali ipo juu.

Ni kupoteza nafasi ya gazeti kuanza kuelezea mafanikio makubwa ya

Rais Magufuli tangu aingie madarakani takriban miezi tisa iliyopita hususan katika ongezeko la makusanyo ya kodi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma. Sijaona hata kiongozi mmoja wa upinzani ambaye hajamsifia mkuu huyo wa nchi kwa kazi kubwa aliyoifanya.

Kwa hatua alizozichukua, siyo ajabu kuwa Rais Magufuli anakubalika zaidi miongoni mwa walalahoi kwa sababu hatua nyingi alizozichukua ni kwa ajili ya kuwatetea wao.

Anakusanya kodi ili aboreshe huduma za wananchi, anadhibiti matumizi ili fedha inayookolewa iende katika huduma za wananchi, kama mwenyewe anavyopenda kusema.

Ziarani Mwanza

Hata hivi karibuni katika ziara zake mikoani alichukua hatua kadhaa za kuwafaidisha wananchi wa hali ya chini moja kwa moja, ikiwamo pale alipowatetea wamachinga kule Mwanza wasiondolewe katikati ya jiji hilo na pale anapokemea kila siku dhidi ya kutoza ushuru wakulima au wafanyabiashara wadogo waliobeba magunia machache ya chakula.

Wananchi wengi wa daraja la chini wanampenda Rais Magufuli na kumwona kama mtetezi wao, upendo huo unaongezeka zaidi kila mkuu huyo wa kaya anapozungumza katika hotuba zake kwa kuwaelezea wapinzani kama maadui wa maendeleo wanaohujumu harakati za Serikali za kuwaondolea kero wananchi.

Naweza kusema kwa uhakika kabisa kuwa tangu Magufuli aapishwe wapinzani wamekuwa wakipoteza wafuasi. Waliokuwa wakiitilia shaka CCM sasa wanaanza kuipenda.

Kwa sasa wapinzani wanaweza kuwa na matumaini na kupata uungwaji mkono kutoka kwa daraja la watu wa kati na baadhi ya wasomi. Matumaini ya kuungwa mkono na wananchi wa daraja hili yanatokana na kwanza uelewa wao mkubwa wa demokrasia, utakaowafanya wajue kuwa tunakoelekea siyo kuzuri.

Pia, tusisahau kuwa daraja hili la watu ndiyo waathirika wakubwa wa hatua za Rais Magufuli za kudhibiti matumizi ya Serikali. Ni hawa ndiyo waliokuwa wakisafiri kwenda nchi za nje kikazi na ni hawa ambao walikuwa wakikutana kwa ajili ya semina katika hoteli za kifahari kujadili namna ya kufanikisha sherehe mbalimbali za kitaifa zilizokuwa zikigharimu mamilioni ya fedha za umma.

Maandamano ya upinzani yatashindwa

Kwa mtazamo huu wa siasa za Tanzania kwa sasa, yeyote anayefikiri sawa atajua kuwa Serikali hii siyo ya kupambana nayo ‘kichwa kichwa’ kwa ukaidi na uasi, kwa kulazimisha mikutano iliyopigwa marufuku na kuandamana. Mkakati huo utashindwa kwa sababu kadhaa.

Kwanza, hautapata uungwaji mkono wa kutosha kwa sababu wanachama wao ni wachache na hata hao walionao huenda wanaoelewa na kuamini katika kinachopiganiwa ni wachache.

Pili, Rais Magufuli na Serikali yake wanakubalika katika mahakama ya umma ambayo siku zote ndiyo inayotoa hukumu katika siasa. Hapo ndipo unaona mgongano wa kanuni za kidemokrasia.

Vipi demokrasia, kanuni ya wengi wape inapotumika kuingiza udikteta? Ni udikteta, sawa lakini wengi wanaunga mkono.

Wangapi miongoni mwa Watanzania watakwambia ukosefu wa demokrasia ni shida yao kuu? Ukiacha uminyaji wa demokrasia, hatua nyingi anazochukua Rais Magufuli ndizo zinajibu shida zao: Umasikini, maradhi na ujinga.

Kama ambavyo ni wazi kuwa siyo haki kwa baadhi ya watu kuwekwa ndani bila kesi zao kusikilizwa, lakini madhali wananchi wanaunga mkono Serikali yao kwa hatua hiyo na hivyo kuhalalisha kitendo hicho; kwa uamuzi wa Septemba Mosi, kutumia maandamano yaliyopewa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) yanayoratibiwa na Chadema unaweza kuwa siyo jambo la busara. Watanzania hawapo tayari kwa siasa za aina hiyo.

Kenya wamefanikiwa

Mambo hayo yalifanikiwa Kenya ambako chini ya mwavuli wa muungano wa vyama vya siasa wa CORD waliichachafya Serikali ya nchi hiyo hadi ikakubali kufanya majadiliano juu ya Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya nchi hiyo (IEBC), ambayo wajumbe waliokuwapo sasa wameng’oka na wapya wanategemewa kuteuliwa hivi karibuni.

Kama imeshindikana Zanzibar ambako kuna hamasa kubwa zaidi ya kisiasa, ni wazi kuwa njia hiyo ya maandamano haitawezekana Bara. Ni wazo baya kwa wapinzani kuendelea kugomea Bunge kwa sababu mgomo huo hauna athari kwa CCM zaidi ya kuipa mwanya wa kupitisha mipango yao kiurahisi zaidi. Wanasema, ‘nyinyi suseni sisi twala”.

Ndiyo maana binafsi naamini kuwa huu ni muda mwafaka kwa wapinzani kufikiria upya mikakati yao ya kupambana kwa ajili ya demokrasia, ambayo kama ambavyo sasa inawazuia viongozi wa vyama vya siasa kufanya kazi zao, utafika wakati marufuku hizi zitaendelea kutanuliwa hadi katika mitandao ya kijamii, ambayo ni kielelezo kikubwa cha uhuru wetu.

Mkakati huo mpya usijumuishe maandamano ya kuasi Serikali kwa sababu licha ya ukweli kuwa watakaojitokeza ni wachache, lakini hata watakaojitoa mhanga uwezekano mkubwa ni kuwa hamna njia za kuwakinga na madhara ya kiuchumi na kijamii yatakayowakumba.

Katika mkakati mpya, vyama vya upinzani vianze kwa kuimarisha umoja wao na wakielewa kuwa wote wanaathirika kwa uamuzi wa Serikali usio rafiki kwa demokrasia.

Pili, wapinzani waangalie njia bora, yenye madhara kidogo kwao na ambayo ina ufanisi katika mapambano dhidi ya hicho wanachokiita, ‘udikteta’.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, anapatikana na kwa barua pepe: [email protected]