Nyerere aliweka msingi wa ukuaji uchumi nchini

Muktasari:

Miongoni mwa mawazo yake ni mapambano dhidi ya maadui wakubwa watatu yaani ujinga, umaskini na maradhi.

Ikiwa imepita miaka 17 tangu kitokee kifo cha Rais wa Kwanza wa Tanzania (Tanganyika), Mwalimu Julius Nyerere, bado Watanzania wameendelea kuyaishi mawazo yake.

Miongoni mwa mawazo yake ni mapambano dhidi ya maadui wakubwa watatu yaani ujinga, umaskini na maradhi.

Mwalimu Nyerere aliichukua nchi mikononi mwa Wakoloni wa Uingereza uliokuwa ukiendesha Serikali kwa mfumo wa ubepari. Lakini mwenyewe alifanya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi.

Kwanza aliifanya nchi kuwa Jamhuri hivyo akapanda kutoka uwaziri mkuu aliokuwa nao na kuwa Rais mwaka 1962. Mwaka 1965 alifuta mfumo wa vingi vya siasa na kukifanya chama tawala cha Tanu kushika hatamu zote za uongozi.

Mabadiliko ya kiuchumi yalirasimishwa mwaka 1967 baada ya kuzinduliwa kwa Azimio la Arusha lililokwenda sambamba na utaifishaji wa rasimali za maendeleo kama vile viwanda, shule na hospitali na kuzifanya kuwa mali ya Serikali.

Licha ya kukuza maendeleo ya viwanda na huduma za jamii kama vile elimu, afya na kujenga uchumi shirikishi, ilipofika miaka ya 80 mambo yakawa magumu. Mwalimu Nyerere aling’atuka mwaka 1985 wakati ambao hali ya uchumi nchini ilikuwa mbaya.

Nini kilisababisha sera ya Ujamaa na Kujitegemea kushindwa kuwa endelevu? Je, mfumo wa soko huria umelifikisha wapi Taifa letu leo?

Wakizungumza na gazeti hili kuhusu mchango wa Mwalimu Nyerere katika mapambano dhidi ya umaskini, baadhi ya wataalamu wa uchumi wanasema mchango huo umesaidia ukuaji wa uchumi mpaka leo.

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi anachambua utendaji wa Mwalimu Nyerere akisema alijenga uchumi shirikishi.

“Kauli ya maadui watatu aliitoa wakati wa utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano, mwaka 1969 hadi 1974. Wakati huo Mwalimu Nyerere kwanza alitaka kila mahali nchini kuwe na usawa wa maendeleo, ikiwamo elimu na afya,” anasema Profesa Moshi na kuongeza: “Ni wakati huo alipohimiza dhana ya kujitegemea na katika usawa wa maendeleo na ujenzi wa viwanda kila mkoa ili watu wasikimbilie mijini. Tunaona kwa mfano Mkoa wa Tanga ulijengwa viwanda vingi.”

Profesa Moshi anaendelea kusema kuwa utekelezaji wa mipango hiyo ulizaa matunda katika miaka ya 70, kulikuwa na viwanda vinavyofanya kazi huku huduma za elimu na afya zikitolewa bure.

Kuhusu mazao ya biashara kama vile kahawa, chai, mkonge na korosho, anasema nayo uzalishaji wake uliongezeka.

“Tanzania ilikuwa inalima na kuuza nje mazao ya biashara kama kahawa, chai na mkonge kwa wingi. Maendeleo vijijini nayo yakaongezeka kwa kasi. Ukiangalia kwa mfano, miaka ya 60, Serikali ilikuwa ikimiliki chini ya asilimia tano ya viwanda, lakini miaka ya 70 vilifikia asilimia 70,” anasema.

Akizungumzia sababu ya kushuka kwa uchumi nchini mwishoni mwa miaka ya 70, Profesa Moshi anasema ni pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta ya kuendeshea mitambo na vita dhidi ya Idd Amin wa Uganda.

“Kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia, viwanda vilianza kuzalisha chini ya kiwango. Kwa upande mwingine, vita ya Uganda ya mwaka 1979 iliathiri uzalishaji bidhaa nchini badala yake tukaagiza nyingi kutoka nje ya nchi,” anasema.

Akigusia ushauri wa nchi za kigeni kubinafsisha rasilimali za umma kama mashirika na huduma za jamii, anasema Nyerere alikuwa na nia njema.

“Wakati ule viongozi wa Uingereza, Margareth Thatcher na Ronald Regan wa Marekani walizionya Serikali za nchi zinazoendelea kutohodhi rasilimali za uchumi. Lakini Mwalimu alikuwa na nia njema, ndiyo maana kwa miaka 24 aliyokaa madarakani hakuwa na nyumba Butiama hadi alipojengewa,” anasema.

Huku akigusia suala la ushirikiano wa biashara kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea (Epa), Profesa Moshi anasema ushirikiano huo unaweza kuua viwanda kwa sababu utazifanya nchi changa kiuchumi kununua bidhaa badala ya kuzalisha.

Mtafiti wa uchumi wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Danford Sango anasema licha ya msingi wa uchumi alioweka Nyerere kuna maboresho ya uchumi ya mwaka 1997 hadi 2012.

“Kuna maboresho ya uchumi yaliyoanza tangu wakati wa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, lakini utekelezaji wake ulianza 1997 wakati wa Rais Benjamin Mkapa. Yalihusisha kuondoa vikwazo vya kibiashara,” anasema na kuongeza: “Pamoja na viashiria vya ukuaji uchumi kwa maisha ya watu havionekani, uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi.”

Anatoa mifano ya ukuaji wa uchumi katika utoaji wa huduma za jamii hasa afya na elimu. “Kiashiria kizuri ni elimu na afya. Katika elimu kumekuwa na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi tangu shule za msingi hadi vyuo vikuu. Katika afya umri wa kuishi kwa Watanzania umeongezeka; kwa mfano 1967 ulikuwa miaka 42, mwaka 2002 ukawa miaka 52, mwaka 2012 umefikia miaka 61. Hiyo ni ishara ya kukua kwa uchumi,” anasema.