Nyerere na wajibu wa watoto kifasihi

Tuesday March 13 2018

 

By Erasto Duwe

Mwalimu Julius Nyerere, licha ya kwamba alikuwa na majukumu makubwa ya uongozi kitaifa na kimataifa, kwa upande wa utamaduni anajipambanua kuwa mpenzi kindakindaki na mwalimu wa fasihi ya Kiswahili.

Hilo linajidhihirisha kupitia kazi zake mbalimbali za kifasihi alizoandika n ahata hotuba.

Mwaka 1964 wakati wa kusherehekea miaka 10 tangu kuanzishwa kwa chama cha TANU, Mwalimu Nyerere alitoa hotuba iliyokuwa na ujumbe mahususi kwa watoto wa Tanzania.

Pamoja na kuwasisitiza kusoma kwa bidii, Mwalimu Nyerere alitoa ujumbe mzito wa kizalendo kwa watoto unaohusiana na fasihi.

Alisema: “...watoto wote wanaosoma shuleni na wale wasiokuwa na bahati hiyo, yawapasa kujifunza kazi za asili za wazee wetu. Mjifunze kwa wazee wenu na babu zenu hadithi, mashairi na historia ya watu wetu maana mambo mengi sana hayakuandikwa vitabuni na kama hamkuyajua basi yatasahaulika.”

Aliongeza: “Hadithi hizi ni sehemu ya urithi wetu, ni lazima mzijue na kuwafundisha wengine pia wazijue zisisahaulike kizazi hata kizazi.”

Kauli hiyo ya Mwalimu Nyerere inahusu moja kwa moja fasihi ya Kiswahili, yaani fasihi simulizi na fasihi andishi.

Kwa maelezo ya Mwalimu, vipengele hivyo vya kifasihi vinabeba tunu kubwa za maisha ya wanajamii. Mathalani, katika hadithi kuna historia, maadili, elimu, mafunzo na maonyo mbalimbali. Kwa watoto, usimulizi wa hadithi una umuhimu mkubwa na athari chanya katika maisha yao.

Mashairi, halikadhalika, yana dhima kubwa katika uelewa, maendeleo, ustawi na makuzi ya watoto.

Kwa kuwa mengi yaliyokuwa yakitolewa na wazee wetu kwa njia ya masimulizi hayakuwa yakiandikwa, njia kubwa na rahisi ya kuyarithisha ilikuwa ni kwa mapokeo kwa wakati huo yaani kurithishwa kutokana na masimulizi ya wazee. Mwalimu aliwasisitiza watoto kupata urithi huo kutoka kwa wazee wao.

Licha ya kusisitiza ushairi na hadithi, katika hotuba yake hiyo, Mwalimu aliendelea kueleza: “...yawabidi kujifunza michezo yetu ya Kiafrika, pamoja na kupiga ngoma na kuimba.”

Aliongeza:, “Vitu hivi ndivyo tunavyoweza kujivunia, na tunapokutana na watoto wa nchi zingine ambao hutaka kutufundisha namna wao wanavyocheza ngoma za kikwao, basi nasi pia tuweze kuwaonyesha michezo yetu.”

Katika nukuu hiyo, Mwalimu anaendelea kuzungumzia fasihi. Anataja ‘ngoma’ ambacho ni kipengele cha sanaa za maonyesho na nyimbo yaani ushairi.

Kwa maoni yetu, Mwalimu Nyerere aliona mbali. Fauka ya mapenzi makubwa aliyokuwa nayo katika fasihi ya Kiswahili, vipengele anavyovitaja vinabeba tunu ya uzalendo ndani yake. Anaposisitiza kupenda hadithi, nyimbo, mashairi na ngoma anatufundisha kuthamini utamaduni wetu.

Kwa kuwa utamaduni ndiyo maisha, tunapaswa kuvithamini vyetu na kujitambulisha kupitia vipengele hivyo vya utamaduni wetu. Mtu asiye na utamaduni wake hata kama akiwa kwenye nchi yake, hana tofauti na mtumwa.

Kwa hotuba hii ya Baba yetu wa Taifa, watoto wapende kujifunza kazi za kifasihi kutoka kwa wakubwa wao. Wasipuuze kwa kuwa kazi hizo zina mchango mkubwa katika makuzi yao.

Wazazi, wazee na jamii kwa jumla waone umuhimu mkubwa wa kuwarithisha watoto masimulizi pokezi kama vile hadithi.

Jamii na taasisi zake zienzi ngoma, nyimbo, mashairi na kazi nyingine za kifasihi kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya watoto na jamii kwa jumla.

Hotuba hii ya Mwalimu, itukumbushe kuwa kila mwanajamii ana wajibu wa kufanya katika kuienzi fasihi ya Kiswahili.


Advertisement