Friday, July 21, 2017

Paul Clement, msanii wa injili anayependa kuimba live

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati muziki wa kizazi kipya au Bongo Fleva ukiendelea kutazamwa kwa ukaribu na mashabiki, kumefanyika mabadiliko makubwa kwenye muziki wa injili, hasa kutokana na ujio wa kizazi kipya.

Kama ukitakiwa kuwataja waimbaji wa muziki wa injili wa kizazi kipya, waliokamata chati hivi sasa hapa nchini kutokana na umahiri kwenye kazi zao, jina la Paul Clement haliwezi kukosekana.

Wimbo wake wa “Amenifanyia Amani” ndio ambao unamfanya atikise kila kona ya nchi kutokana na kubeba ujumbe mzito.

Licha ya wimbo huo, aina ya uimbaji wake unamfanya ajitofautishe na waimbaji wengine, na hivyo kukusanya mashabiki wengi wa nje na ndani ya nchi.

Clement anasema mafanikio anayojivunia tangu aingie kwenye muziki wa injili ni kuokoa roho za watu zilizokuwa zimepotelea dhambini na kuzirejesha kwa Mungu.

“Muziki umenikutanisha na watu wengi tofauti wa nje na ndani ya nchi lakini mafanikio makubwa sana, ni namna nyimbo zangu zilivyosaidia kuokoa roho za watu,” anasema.

Anachokifanya kwa sasa

Anasema kuwa anaendelea na mazoezi akijiandaa na project yake ya kurekodi ‘live’ anayotarajia kuifanya hivi karibuni.

Alisema albamu yake ya Amenifanyia Amani, imeshatoka na hivyo wapenzi wa muziki wake wanaweza kuipata sokoni.

Anasema changamoto kubwa anayokutana nayo ni watu wanaomualika, kushindwa kugharamia muziki wa live kwa sababu huenda na wapigaji ala.

“Watu wanaonialika huwa wanataka sana niende kuhudumu lakini kwa sababu mimi huwa nafanya live, wanashindwa kugharamia,” anasema.

“Mpaka hapa nilipofika si kwa akili zangu isipokuwa ni kwa neema ya Mungu.”

Chini ya uongozi

Clement ni kati ya wanamuziki wachache wa Injili waliofanikiwa kuwa chini ya kampuni ya menejimenti na hivyo kazi zake kuendeshwa kwa mafanikio.

Aliiingia mkataba na kampuni ya kutayarisha na kusimamia kazi za wasanii inayojulikana kwa jina la Fisher Records mwaka 2015 akiwa msanii wa kwanza kusimamiwa na kusimamiwa kazi zake zote. Studio ya Fisher Records ipo chini ya uongozi wa Godfrey Benjamin.

Hadi sasa ameshakamilisha albamu yake yenye nyimbo 13 na tayari video mbili za nyimbo za “Umerudi Nyuma” na “Amenifanyia Amani” zimeshatoka.

“Baadhi ya waimbaji niliowashirikisha ni pamoja na Angel Bernard, Amoke Kyando na Elandre.

Nyimbo na video zote zimetayarishwa Taz na Innocent wa Fisher Records na video imeongozwa na Einxer.

Alikotokea

Paul Clement alianza muziki mwaka mwaka 2008 akiwa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Azania jijini Dar es Salaam.

Haikuwa rahisi kwa Clement kuweza kuimba kwa sauti nzuri, lakini kwa usaidizi wa mfalme wa R&B nchini, Ben Paul, alijikuta akiwa mahiri ndani ya muda mfupi tu.

Baada ya kumaliza kidato cha nne mwaka 2011, alijiunga na kikundi cha uimbaji cha GC Glorious Celebrations na hapo kipaji cha Clement kilisikika kwa mara ya kwanza katika albamu ya kwanza ya kundi hilo inayoitwa Niguse.

“Katika albamu hiyo, niilimba nyimbo mbili; ‘Juu ya Mataifa’ na ‘Unaweza Yesu’. Katika albamu ya pili ya kundi hilo niliimba wimbo ‘Umenifanyia Ibada’ ambao ulinitambulisha vyema,” anasema.

Safari yake katika muziki wa injili ilimfikisha kuwa mwanamuziki wa kujitegemea na mwaka 2012 aliachia albamu yake ya Umeniita akiwa chini ya Studio za Mawila Son Production iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.

Alijiwekea rekodi ya kipekee mwaka 2014, wakati alipofanikiwa kurekodi albamu nzima iliyorekodiwa moja kwa moja (live recording) aliyoibatiza jina Atendaye ni Mungu.

Mwanamuziki huyo alizaliwa mwaka 1992, mkoani Ruvuma.

-->