Posho za madaraka wakuu wa shule, maofisa elimu kata ziinue ubora wa elimu

Muktasari:

  • Maoni ya wengi ni kutaka hatua za makusudi zichukuliwe kuhakikisha mambo yanawekwa sawa ili kuwakwamua watoto hawa watakaokuwa muhimu kusimamia uchumi na rasilimali za Taifa huko mbeleni.

Wadau wengi wanatahadharisha kuhusu kushuka kwa ubora wa elimu hasa kwenye shule za umma ambako watoto wengi wa Kitanzania wanasoma.

Maoni ya wengi ni kutaka hatua za makusudi zichukuliwe kuhakikisha mambo yanawekwa sawa ili kuwakwamua watoto hawa watakaokuwa muhimu kusimamia uchumi na rasilimali za Taifa huko mbeleni.

Maoni hayo yanaongezeka zaidi siku za karibuni kutokana na matokeo kuonyesha shule nyingi, hata zilizokuwa zinaongoza zikiwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaofeli kwenye mitihani yao ya mwisho.

Mwenendo huu sio tu unapunguza ushindani wa Watanzania kwenye soko la ajira kimataifa, bali unapunguza ubunifu, uvumbuzi na uwezo wa kusimamia miradi ya maendeleo au kutatua changamoto mbalimbali zitakazokuwa zinajitokeza.

Pamoja na hali hiyo, Zipo jitihada nyingi zinazofanywa na Serikali kuinua ubora wa elimu nchini kwa kuwekeza fedha nyingi kuimarisha miundombinu ya yakiwamo madarasa, vyoo, madawati, viti, meza na nyumba za walimu.

Kwa kutambua ukweli kwamba miubombinu bora pekee haitoshi bila kuwapo waalimu na wasimamizi bora wa elimu, Serikali inatoa Sh200,000 kila mwezi kwa kila mkuu wa shule ya msingi na Sh250,000 kwa kila mkuu wa sekondari na ofisa elimu kata.

Takwimu za Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zinaonyesha kulikuwa na wastani wa sekondari 4,800 hadi Januari mwaka huu na shule za msingi 17,000 nchini kote.

Shule hizo zipo kwenye kata 3,000 zilizopo Tanzania nzima.

Kwa takwimu hizo, kila mwezi, Serikali inatumia wastani wa Sh1.2 bilioni kulipa posho za madaraka kwa wakuu wa shule za sekondari. Aidha, inatumia wastani wa Sh3.4 bilioni kila mwezi kulipa posho za aina hiyo kwa wakuu wa shule za msingi.

Kwa upande wa maofisa elimu kata, Serikali inatumia wastani wa Sh750 milioni kulipa posho za madaraka kwa ajili ya ufuatiliaji na usimamizi wa elimu katika maeneo yao.

Takwimu zinaonesha Serikali inatumia wastani wa Sh64.2 bilioni kwa mwaka, sawa na Sh5.4 bilioni kwa mwezi kulipa posho za madaraka kwa makundi yaliyoainishwa hapo juu.

Posho za madaraka ni fedha inayolipwa kwa wakuu wa shule za msingi na sekondari pamoja na maofisa elimu kata nje ya mishahara yao ya kawaida.

Hii ina maana kuwa pamoja na mishahara na stahiki nyingine wanazopata, fedha hii ni maalum kwa ajili ya usimamizi wa elimu katika maeneo yao na haina uhusiano na mshahara wala marupurupu mengine.

Kwa miaka mitano, hadi mwaka 2020, Serikali itatumia wastani wa Sh321 bilioni kulipa posho za madaraka kwa makundi hayo matatu.

Hiki ni kiasi kikubwa sana cha fedha. Makadirio yanaonyesha, kiasi hicho kinaweza kujenga madarasa 17,833 kwa wastani wa Sh18 milioni kila moja.

Vilevile, zinaweza kutengeneza madawati milioni 6.4 kila moja likigharimu Sh50,000 au kujenga vyoo 32,100 vyenye matundu 12 kwa wastani wa Sh10 milioni kwa kila kimoja.

Ni vyema kufahamu matumizi mbadala ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kulipa posho za madaraka ili kuona dhamira ya iliyopo ya kuinua ubora wa elimu nchini.

Ikumbukwe, fedha hizi hazina uhusiano na Sh23 bilioni zinazotolewa na Serikali kila mwezi kugharamia elimu bila malipo.

Baadhi ya mikoa iliyopo chini ya mradi wa kuinua ubora wa elimu Tanzania (Equip-T) inaneemeka zaidi kwani maofisa elimu kata wote wamepewa pikipiki huku gharama zake zikiwa chini ya mradi.

Walimu wakuu wa shule za msingi na wakuu wa sekondari hupewa mafunzo na nyenzo mbalimbali kuhakikisha wanatumia muda na maarifa yao kusimamia njia kuu za uwasilishaji wa elimu katika maeneo yao.

Wakuu wa shule za msingi na sekondari pamoja na maofisa elimu kata wote nchini wanapaswa kuona dhamana kubwa waliyopewa na wananchi kupitia Serikali yao kusimamia ubora wa elimu kwa watoto wanyonge kutoka familia nyingi masikini.

Kufanikisha malengo ya Serikali ni lazima baadhi ya watu wapewe majukumu ya kusimamia mpango uliopo. Makundi haya mamatatu yamepewa dhamana hii kwa niaba ya Watanzania wote hivyo ni muhimu kuhakikisha wanatekeleza wajibu wabu wao kwa manufaa ya wananchi wote.

Posho za madaraka ziwe sehemu ya kuongeza ufanisi na uwajibikaji na zitumike kuhakikisha lengo la Serikali kutoa elimu bila malipo kwa wananchi masikini wasiokuwa na uwezo wa kupeleka watoto wao shule binafsi linafanikiwa.

Mwandishi ni mtakwimu na ofisa mipango