Rosemary Odinga katika kilimo cha konokono

Muktasari:

Rosemary anaeleza kuwa, alianza kufanya biashara hiyo mwaka 2007 aliporudi nchini Kenya akitokea Nigeria ambapo alikwenda kumtembelea Rais mstaafu wa nchi hiyo, Olesegun Obasanjo ambaye ni mmoja wa wakulima wakubwa wa kilimo cha konokono.

Huenda kilimo cha konokono ikawa si biashara ambayo wengi tunaifahamu, lakini ipo na mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya, Raila Odinga, Rosemry Odinga ni miongoni mwa watu wachache waliojikita katika biashara hii.

Rosemary anaeleza kuwa, alianza kufanya biashara hiyo mwaka 2007 aliporudi nchini Kenya akitokea Nigeria ambapo alikwenda kumtembelea Rais mstaafu wa nchi hiyo, Olesegun Obasanjo ambaye ni mmoja wa wakulima wakubwa wa kilimo cha konokono.

Anasema aliporudi Kenya alianza kufanya udadisi kuhusu konokono ikiwemo kutembelea Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo alikutana na mtaalamu mmoja wa wadudu hao aliyemsaidia kuwafahamu na pia alimpa konokono 12 kama mtaji katika biashara yake.

Rosemary anasimulia kwamba konokono 10 kati ya hao walikufa kutokana na joto, lakini aliipogundua hilo aliwatengenezea sehemu nzuri ambapo miezi kadhaa baadae, konokono wawili waliosalia walizaliana na sasa ana miliki zaidi konokono 3000.

Anasema soko la konokono ni mahoteli na migahawa mikubwa ambao huwatumia kama kitoweo, na yeye hupakia katika paketi ya gramu 160 yenye konokono 24 kila moja na kuuza.

Rosemary anawashauri wajasiliamali wengine hasa wanawake kujikita katika biashara hiyo ambayo bado haijapa ushindani mkubwa ilhali soko lake lipo la kutosha.