Sababu zinazochangia meno ya watoto kutoboka na kuoza

Picha na Mtandao

Muktasari:

Mpana meno ya mtoto mchanga yaanze kuonekana yanaweza kupata maambukizi endapo kinywa kitakuwa hakitunzwi vyema. Wakati yakiota, yanaweza yakaanza kutoboka hivyo ni vizuri kuanza kumzoesha mtoto husika usafi wa kinywa na meno.

Afya ya kinywa ni muhimu hata kwa mtoto mchanga ambaye hana meno kinywani mwake. Ingawa meno ya mtoto mchanga huanza kuonekana miezi sita baada ya kuzaliwa, mzazi anashauriwa kuanza kusafisha kinywa chake siku chache baada ya kuzaliwa kwa kufuta fizi zake kwa kitambaa kisafi.

Mpana meno ya mtoto mchanga yaanze kuonekana yanaweza kupata maambukizi endapo kinywa kitakuwa hakitunzwi vyema. Wakati yakiota, yanaweza yakaanza kutoboka hivyo ni vizuri kuanza kumzoesha mtoto husika usafi wa kinywa na meno.

Kuanza kutunza meno ya mtoto tangu anapokua mchanga huweza kumkinga na kutoboka kwa meno na magonjwa mengine ya kinywa kwa miaka mingi ijayo. Pindi mtoto anapozaliwa, taya zake huwa zimeshabeba meno yote 20 ya utotoni.

Anza kusafisha kinywa cha mtoto wako siku chache baada ya kuzaliwa kwa kufuta fizi zake kwa kitambaa kisafi. Meno ya mbele ya utotoni huweza kujitokeza miezi sita baada ya kuzaliwa ingawa baadhi ya watoto kuchelewa kuota meno mpaka miezi 12 au 14.

Mpaka ujiridhishe kuwa mwanao anaweza kupiga mswaki mwenyewe, endelea kumsaidia kupiga mswaki mara mbili kwa siku kwa kutumia mswaki wa watoto pamoja na dawa ya meno yenye madini ya floridi.

Kwa mtoto wenye umri wa chini ya miaka mitatu, wazazi ama walezi wanatakiwa waanze kumpigisha mswaki mara tu meno yanapoanza kutokeza kinywani. Mswaki huo unatakiwa uwe mdogo na dawa ya meno yenye madini ya floridi ukubwa wa punje ya mchele.

Upigaji wa mswaki unapaswa kufanywa kwa umakini asubuhi baada ya kifungua kinywa na usiku kabla ya kulala. Mzazi anatakiwa akikishe mtoto hamezi dawa ya meno inayotumika wakati wa kusafisha kinywa na meno, mtoto aiteme yote na kusukutua kwa maji safi.

Kwa watoto wa umri wa kati ya miaka mitatu mpaka sita, wakati wa kupiga mswaki, mzazi anatakiwa ahakikishe dawa ya meno inayotumika ina madini ya floridi na ukubwa wa punje ya harage.

Kwa kawaida, meno ya utotoni yanapoanza kujitokeza miezi sita mpaka mwaka mmoja baada ya kuzaliwa, baadhi ya watoto huvimba na kuhisi maumivu kwenye fizi.

Inashauriwa, hali hii inapotokea, pitisha taratibu kidole ama kitambaa kisafi ili kutuliza hali hiyo. Watoto wengi wafikapo umri wa miaka mitatu, huwa na meno yote 20 ya utotoni.

Meno ya utotoni muhimu

Siyo tu meno ya utotoni humuwezesha mtoto kutafuna na kuzungumza vizuri, hutumika kutunza nafasi kwa ajili ya yale ya ukubwani ambayo huwa chini ya hayo meno ya utotoni.

Inapotokea meno ya utotoni yanatoka mapema na kabla ya wakati wake, huweza kusababisha kuvuruga kwa mtiririko wa uotaji na mpangilio mzima wa meno. Ndiyo maana ni muhimu kuanza kufuatilia afya bora ya kinywa na meno tangu utotoni ili kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza na kuleta athari za kudumu.

Mtoto kama alivyo mtu mzima anahitaji huduma za daktari wa kinywa na meno ili kumtazama na kujua hali ya uotaji wa meno kulinganisha na ukuaji pamoja na afya ya kinywa kwa ujumla.

Ni vizuri zaidi, kama inawezekana, daktari huyu awe yule anayetibu wana familia husika ili itamrahisishia kuangalia kinywa cha mtoto na kulinganisha na wana familia wengine.

Mtoto anaweza kupelekwa kwa daktari wa meno kuanzia anapotimiza mwaka mmoja au zaidi tangu azaliwe. Huu ni wakati mzuri kwa daktari wa kinywa na meno kuangalia vizuri maendeleo ya ukuaji wa kinywa cha mtoto husika.

Mara nyingi matatizo ya kinywa huanza mapema hivyo unapompeleka kwa daktari mapema, inakuwa rahisi kuchukua hatua pale inapobidi. Halikadhalika, daktari anaweza kupendekeza hatua za kuzuia tabia ambazo si nzuri kwa afya ya kinywa kama vile unyonyaji wa kidole.

Watoto huanza kung’oka meno ya utotoni kuanzia wanapofikisha miaka mitano. Meno ya mbele huanza kung’oka na mengine hufuatia kwa zamu. Hali hii huendelea huku meno ya ukubwani yakiota mpaka atakapofikisha miaka 12 au 13 ambapo meno yote ya utotoni, kwa watoto wengi, huwa yameng’oka yote.

Kumziba Meno

Ni jambo zuri kuhakikisha meno ya utotoni yanaendelea kuwapo kinywani kwa muda wote mpaka wakati wake wa kung’oka utakapofika. Hii ni kwa sababu mbali na kumuwezesha mtoto kula vizuri, meno haya huwa yanatunza mpangilio mzuri wa meno ya ukubwani.

Kama jino la utotoni litaondolewa mapema kutokana na kutoboka au kuoza, nafasi hiyo itahitaji gharama kubwa za matibabu kuitunza ili kuepuka mpangilio mbaya wa meno.

Ili kuepuka kuathirika kwa meno ya utotoni, yapo mambo kadhaa ambayo mzazi au mlezi akiyafanya itasaidia kuyatunza. Haya yote yanaweza yakafanyika nyumbani bila kuhitaji msaada wa daktari.

Mosi ni kusafisha fizi za mtoto kwa kutumia kitambaa safi na kilicholowanishwa na mara tu jino la kwanza linapoanza kujitokeza, anza kumpigisha mswaki kwa kutumia dawa ya meno yenye madini ya floridi.

Jambo jingine muhimu ni kumsaidia mtoto kupiga kama inavyoshauriwa na anapofikisha umri wa kuanzia miaka mitano anaweza kuanza kupiga mswaki mwenyewe akifuata maelekezo ya mzazi au mlezi.

Ili kumsaidia kuelewa suala hilo kwa ufasaha, inashauriwa kumfundisha mtoto kwa mfano yaani mzazi au mlezi kumruhusu mtoto atazame wakati yeye akipiga mswaki.

Usafi wa kinywa na meno ya mtoto ni muhimu ili kuepusha kutoboka na kuoza, na madhara yake. Mara nyingi, kutoboka hutokea kwa meno ya juu ya mbele ingawa hata meno mengine huweza kuathirika.

Wazazi wanaweza wasifahamu kutoboka ama kuoza kwa meno ya mtoto kwa sababu ni suala linaloweza kujitokeza mara tu meno yanapoota kwa mara ya kwanza.

Kutoboka kisha kuoza wakati mwingine huweza kuufikia mfupa wa taya hali ambayo huathiri ukuaji wa meno ya ukubwani. Hali hii husababishwa na meno hayo kukutana kwa muda mrefu na vitu vya sukari ambavyo hutumiwa na bakteria wanaoishi kinywani kutengeneza tindikali ambayo huyaozesha na kuumiza fizi.