MAONI: Safari bado ndefu kutekeleza mpango wa elimu jumuishi

Muktasari:

Katiba ya Tanzania, ibara ya 11(2) imetoa haki ya kupata elimu, japo haisemi mtu atapataje haki hiyo ikiwa hana uwezo kifedha au kimaumbile.

Duniani kote elimu inachukuliwa kuwa haki ya msingi, bila kujali hali ya mtu kifedha au kimaumbile.

Katiba ya Tanzania, ibara ya 11(2) imetoa haki ya kupata elimu, japo haisemi mtu atapataje haki hiyo ikiwa hana uwezo kifedha au kimaumbile.

Licha ya haki ya kupata elimu, bado kuna Watanzania wengi wameshindwa kuipata, huku wengine wakikwazwa kutokana na ulemavu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) linatafsiri elimu jumuishi kama mchakato wenye lengo la kuwaunganisha wanafunzi kwa kuongeza ushiriki na kupunguza ubaguzi katika elimu.

Mjumuiko huo unahusisha wanawake na wanaume, umri, ulemavu wa akili na maumbile, ukabila, rangi ya mtu, utajiri na asili ya mtu (mhamiaji au mzawa).

Katika makundi hayo, kundi la walemavu linapata shida zaidi kwani watoto hao wanahitaji usaidizi kama kubebwa, kusafishwa, kulishwa, na kufundishwa.

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) linakadiria kuwa asilimia 51 ya wavulana na asilimia 42 ya wasichana wenye ulemavu duniani, humaliza shule za msingi. Ukosefu wa elimu kwa Watanzania wenye ulemavu ni asilimia 48 ikilinganishwa na asilimia 25 ya wasio na ulemavu.

Kutokana na kukosa taarifa na kushindwa kujumuika na jamii ili kujiendeleza kifikra, walemavu wanashindwa kupata ajira na hivyo kuishia kwenye lindi la umaskini. Kutokana na hali hiyo, elimu jumuishi inapaswa kupewa kipaumbele ili makundi yasiyo na uwezo nayo yaipate.

Kwa muda mrefu kundi la watoto wenye ulemavu wa viungo na akili limekuwa likitengwa au kubaguliwa na jamii na hivyo kushindwa kupata elimu ya kuwakwamua kwenye lindi la umaskini.

Tanzania imeridhia mikataba ya kimataifa ya kutoa elimu kwa wananchi wote na inatambua haki ya elimu kwa wananchi wote.

Kwa kutambua hilo, Tanzania ina mkakati wa kitaifa wa Elimu Jumuishi wa mwaka 2009-2017. Kutokana na hali hiyo wananchi wamekuwa na uelewa kuhusu elimu jumuishi kama haki ya wote na kumekuwa na upanuzi wa baadhi ya shule ili kujumuisha makundi mengine.

Kutokana kutambua pia, kumekuwa na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi kwa shule za msingi na sekondari kila mwaka. Uandikishwaji huo pia umevutiwa na sera ya elimu bure iliyotangazwa na Rais John Magufuli.

Kumekuwa pia na ongezeko la elimu ya watu wazima ikihusisha watu walioikosa wakiwa na umri mdogo. Elimu hiyo pia imevutia wadau kama mashirika binafsi kujitolea kusaidia utoaji wa elimu.

Pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto nyingi, huku elimu yenyewe ikiwa inatolewa kwa kiwango cha chini.

Bado kuna tatizo la walimu wa elimu maalumu, huku waliopo wakifundisha na kuishi katika mazingira magumu.

Kuna tatizo pia la ubaguzi wa jinsia ambapo inaonekana watoto wa kike hubaguliwa katika elimu na jamii na wengi hushindwa kuendelea na masomo kuliko watoto wa kiume kutokana na mtazamo wa kijamii na mila na desturi.

Licha ya Serikali kuitambua elimu jumuishi, bado haitoi bajeti ya kutosha ili kugharimia miundombinu kama madarasa, kuongeza walimu na vifaa vya kufundishia.

Kutokana na ukosefu wa walimu wenye sifa, watoto wenye mahitaji maalum wamejikuta wakitengwa na kukosa elimu iliyokusudia huku wengine wakifundishwa na kulelewa na watu wasio na sifa.

Kuna tatizo pia la umasikini katika jamii. Baadhi ya watoto wamezaliwa na kulelewa na upande mmoja. Mara nyingi wanaume huwatelekeza wanawake wanapoona wamejifungua watoto walemavu.

Hali hiyo humpa mzigo mwanamke kutafuta ujira wa kutunza familia na wakati huo huo kumhudumia mtoto mlemavu, hali inayosababisha wengi kushindwa.

Kinachotakiwa kufanyika ni kuongeza kampeni ya elimu bora jumuishi kwa wote. Serikali ina jukumu kubwa la kuhamasisha jamii ikubaliane na elimu hii na itoe ushirikiano.

Serikali pia iongeze bajeti ya elimu ili iweze kujenga miundombinu wezeshi kwa watu wenye mahitaji maalum, kuongeza walimu wenye sifa na vifaa.

Vilevile Serikali iongeze fedha kwa ajili ya tafiti na kuboresha sera zilizopo ili zioane na mkakati wa kuboresha elimu hiyo. Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto ikazie sheria zake ili kuwabana wanaume wanaotelekeza familia zao kwa sababu ya ulemavu.

Mbali na Serikali, jamii nayo inapaswa kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kuwatoa watoto au watu wazima waliokosa elimu ili waipate kwa mfumo wa elimu jumuishi.

Elias Msuya ni mwandishi wa Mwananchi. Anapatikana kwa baruapepe: [email protected]