Samatta ni kila kitu aisee

Muktasari:

Kama si uzembe wa mabeki, tulishailaza Zambia 1-0, lakini waliposawazisha dakika ya 90+ ikatumaliza, tukatoka kwa kuwa pointi zetu hazikutosha, Zambia ikaenda robo fainali.

       Miaka ya 2006 hadi 2010 ukitaja Taifa Stars, jina linalofuata ni Marcio Maximo, na ukimtaja Maximo kinachofuata ni soka ya Taifa Stars. Kipindi ilea cha kabisa, angalau tuliambulia kucheza Fauinali za Chan, zilizofanyika Ivory Coast.

Kama si uzembe wa mabeki, tulishailaza Zambia 1-0, lakini waliposawazisha dakika ya 90+ ikatumaliza, tukatoka kwa kuwa pointi zetu hazikutosha, Zambia ikaenda robo fainali.

Hivi sasa, katika kundi la mashabiki 10 wa soka Tanzania wanaoizungumzia Taifa Stars, wanane kati yao hawawezi kumaliza mazungumzo yanayohusu mchezo huo unaoongoza kwa kupendwa ulimwenguni bila kulijumuisha jina la Mbwana Samatta.

Si jambo la kushangaza na kwa vyovyote ni lazima iwe hivyo kutokana na mafanikio makubwa ambayo mshambuliaji huyo ameyapata katika medani ya soka katika miaka ya karibuni kulinganisha na wachezaji wenzake waliomtangulia sambamba na wale wa kizazi cha sasa.

Ubora wake katika soka ulimsaidia kutwaa tuzo ya mwanasoka bora Afrika kwa wachezaji ambao wanacheza ligi za ndani.

Amekuwa mfungaji bora wa mashindano ya ngazi ya klabu Afrika mara mbili lakini pia ametwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na timu yake ya zamani TP Mazembe.

Pengine mafanikio hayo makubwa ambayo Samatta ameyapata ndani ya uwanja ndio yaliishawishi timu ya KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji kumsajili nyota huyo wa zamani wa timu za Simba na Mbagala Market.

Si KRC Genk tu, bali hata benchi la ufundi la timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ lilimpa jukumu zito la unahodha mshambuliaji huyo huku pia akiwa ndio tegemeo kwenye upachikaji wa mabao kwenye kikosi cha timu hiyo.

Samatta ni jicho la timu ya taifa na amekuwa akitazamwa na kila mmoja kuanzia wachezaji wenzake, makocha pamoja na mashabiki wa soka nchini. Ni aina ya lulu ndani ya Taifa Stars.

Spoti Mikiki lilimfuatilia kwa karibu Samatta hasa wakati wa mazoezi. Ni mchezaji anayeonyesha ushirikiano na wenzake. Maisha yake ya Ulaya hayajamweka mbali na wenzake tofauti na wengine ambao wanaona kucheza Ulaya ndiyo kila kitu.

Hufanya mazoezi yake na wakati mwingine huwa na wachezaji wenzake muda mwingi hasa pale kocha anapowahitaji kwa mazoezi ya pamoja. Hana maringo wala kujidai, ana nidhamu na ni mchezaji anayetamani kuona mwingine akipiga hatua.

Aliwahi kusema kuwa anaona wachezaji wana vipaji, lakini anaumizwa kuona hawana utayari kucheza soka nje.

Picha halisi ya maisha ya Samatta nje ya uwanja imeonwa hata wachezaji wenzake wa Stars ambao wamekuwa wakiishi naye kwenye kambi ya timu ya taifa pindi inapoitwa.

Mshambuliaji wa Yanga, Saimon Msuva anafichua kuwa Samatta ni mtu wa aina yake anapokuwa kwenye kambi ya timu ya taifa, ni mchezaji ambaye anajiheshimu na kufanya vitu kwa umakini mkubwa jambo linalomfanya awe mfano bora kwao.

“huyu jamaa kila anachokifanya ni kwa utaratibu, anahakikisha kinakwendana na muda na ana nidhamu ya hali ya juu pamoja na kumheshimu kila mmoja.”

Kama ni wakati wa kula, anahakikisha yeye anakuwa wa kwanza kufika sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya chakula. Muda wa mazoezi yeye anakuwa wa kwanza kuvaa na kuingia uwanjani na pia hata kulala yeye analala kwa muda ule ule uliopangwa bila kuzidisha. Lazima utaona aibu, nawe utafuatisha vile, sisi huku hatujafikia hatua hiyo.

“Kiukweli tunajifunza mambo mengi sana kupitia yeye na maisha yake ni mfano tosha kwetu sisi kwa mwanasoka na kama ni mchezaji wa kulipwa, wengine ambao tuna ndoto na malengo ya kupiga hatua kwenye mchezo wa soka, inabidi kujipanga sana,” anasema Msuva.

“Msuva anafichua kuwa Mkwasa hakukosea kumpa Samatta unahodha wa Taifa Stars, ukweli anastahili.

“Samatta ni kiongozi halisi ni mfano wa kuigwa kwani pia licha ya kuwa kiongozi wa uwanjani, pia amekuwa akiwashauri mambo mbalimbali na jinsi ya kufanikiwa kimaisha na zaidi kupitia soka.

“Mimi binafsi amekuwa akinishauri mambo mengi na kwa kiasi kikubwa amenibadilisha maisha yangu ya kisoka tofauti na hapo nyuma.

“Amekuwa akituasa na kutuhamasisha tujitume na kutokata tamaa ili tuweze kusonga mbele zaidi na pia amekuwa akitusisitiza tuwe na nidhamu ya maisha.

“Unajua wengine wakishapata nafasi wanajisahau na kuona kuwa wao ndio wao. Samatta anaipinga sana hiyo,” anasema Msuva.

Mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mbaraka Yusuf safari hii alipata fursa ya kuitwa kwenye kikosi cha Stars baada ya kufanya vyema kwenye Ligi Kuu msimu huu na ndipo alipata fursa ya kukutana na Samatta ambaye anamuelezea kama mtu mwenye tabia za kipekee.

“Hii ndio mara ya kwanza kwangu kuwemo kwenye kikosi cha Stars na kuzoeana na Samatta lakini kikubwa ambacho nimefaidika nacho kutoka kwake, ni jinsi ya kuishi maisha ya kisoka nje na ndani ya uwanja.

Ni mchezaji anayejua nini anachokifanya na hapendi kuona mwenzake anakata tamaa au kushindwa kufanya jambo fulani. Hana tatizo na mtu na kila mchezaji anampa heshima sawa kama anavyofanya kwa wengine. Kiukweli najivunia kucheza naye pamoja,” anasema Yusuf.

Andrew Vincent anasema: “Nimejifunza mengi kupitia yeye pindi tunapokutana kwenye kambi ya timu ya taifa ambayo kimsingi yananijenga kwenye maisha yangu ya soka.”

“Ni mchangamfu kwa wachezaji wenzake na hajisikii. Kwa ufupi tumekuwa tukiishi naye vizuri na hana maringo,” anasema beki wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’.

Vincent anasema kuwa licha ya kucheza soka ya kulipwa kwenye timu kubwa Ulaya, Samatta hana majivuno na maringo kwa wenzake na mara zote amekuwa akijichanganya na wenzake wakati wote na ninavyomwangalia anatamani sana tuwe na kiwango sawa na chake.

Mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya anasema kuwa kinachomkosha zaidi kwa Samatta ni jinsi anavyowajenga wenzake kisaikolojia na pia anavyoleta umoja ndani ya timu.

“Yeye ndiye mhamasishaji wetu mkuu na anapenda kuwa mfano bora kwa kila jambo linalohusu timu ndio maana anaheshimika na kila mmoja kwenye kikosi. Mimi binafsi ninamheshimu kwa jinsi anavyoishi vizuri na sisi, mnapiga stori, asipoelewa anauliza, mnacheka yaani iko hivyo,” anasema Kichuya.