MAONI: Siasa isipiku utaalamu katika miradi ya maendeleo

Muktasari:

Miradi mingi iliyotajwa kusahauliwa ipo vijijini, ambayo ni pamoja na ujenzi wa madarasa ya shule, nyumba za walimu, vituo vya afya na masoko.

Hivi karibuni vyombo vya habari vya Zanzibar vimetoa taarifa kuhusu namna miradi ya maendeleo ilivyokwama kwa muda mrefu visiwani humo.

Miradi mingi iliyotajwa kusahauliwa ipo vijijini, ambayo ni pamoja na ujenzi wa madarasa ya shule, nyumba za walimu, vituo vya afya na masoko.

Katika orodha hiyo ya majengo yaliyogeuka magofu lipo jengo la Ikulu ndogo Micheweni, Kusini Pemba, ambalo jiwe lake la msingi liliwekwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete miaka 13 iliyopita. Jengo jingine ni ofisi ya Wizara ya Fedha katika mji wa Chake Chake, Pemba.

Baadhi ya majengo haya yaliwekewa mawe ya msingi karibu miaka 20 iliyopita na kuelezwa kwamba ujenzi ungekamilika baada ya kipindi cha muda mfupi.

Hata hivyo, hivi sasa majengo haya ni mazalio maarufu ya wanyama kama paka na mbwa na mengine yamegeuzwa vituo vya vijana wanaotumia dawa za kulevya na vitendo vingine vya uhalifu.

Baada ya sherehe kubwa wakati wa uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi hiyo, majengo yameachwa kwa muda mrefu kiasi kwamba baadhi yameporomoka huku mengine yakizungukwa na vichaka.

Badala ya Serikali kuisimamia miradi iliyoanza kutekeleza, imeacha na kuendelea kuibua miradi mipya kila siku. Matokeo yake ni kuwa ile iliyoanzishwa imetelekezwa.

Kwa muhtasari, tunachoona muhimu ni kuweka mawe ya msingi ya miradi mipya kila tunapokuwa na sherehe za kitaifa za Zanzibar za Muungano au Mwenge wa Uhuru ukifika katika sehemu hizo katika safari zake za nchi nzima kila mwaka.

Miradi hii ya maendeleo iliyotumia fedha nyingi za umma iliwapa matumaini wanananchi wa sehemu husika kuwa wangenufaika kwa njia moja au nyingine iwapo ingekamilika.

Hivi sasa ndoto za wananchi zimetoweka na wanabaki kujiuliza na kuulizana “kulikoni?”

Hali hii haipaswi kuachiwa kuendelea na lazima tufanye juhudi za kuirekebisha kwa sababu badala ya kutupeleka mbele kimaendeleo inaturudisha nyuma.

Ukichunguza utaona kilichotokea ni matokeo ya kuwa na mipango mibovu au kutokuwa nayo kabisa.

Mara nyingi miradi huanzishwa haraka haraka kwa vile huwa tunataka kujifurahisha kutokana na utashi wa kisiasa tulionao bila ya kujali mazingira ya kiuchumi na kijamii.

Kwa mfano, nyumba ya mwalimu inajengwa bila ya kuzingatia mambo muhimu katika maisha ya kila siku, kama upatikanaji wa maji safi na salama karibu na hapo inapojengwa.

Miradi mingi hufanyika bila kuwapo utafiti wa kina na hata ukifanyika ushauri wake hauzingatiwi. Mara nyingine hufanyika uzembe, kiasi ambacho mtu anaweza kujiuliza “Hivi hao walioidhinisha utekelezaji wa miradi hiyo walikuwa watu wenye akili timamu?”

Wizara ya Elimu ya Zanzibar ilijenga kiwanda cha uchapaji kule Mbweni bila ya kuwapo choo na ilichukua zaidi ya mwaka mmoja baada ya wafanyakazi zaidi ya 10 wa kiwanda hicho, kulalamikia shida waliyokuwa wakipata ya kwenda kujisaidia vichakani hasa nyakati za usiku.

Vile vile, Serikali imewahi kujenga masoko ya kisasa ya samaki katika vijiji vilivyopo kando ya bahari ili kuwaondolea wavuvi na wafanyabiashara shida ya kupigwa na jua na kunyeshewa mvua kwa kufanya shughuli zao katika maeneo ya wazi.

Kinachoshangaza ni kuwa baadhi ya masoko, kama la Kijiji cha Uroa, ambalo linatumiwa na wafanyabiashara wapatao 300, wanaume na wanawake, lilitumika kwa muda mrefu bila kuwa na vyoo.

Kwa kweli haya siyo mambo yanayostahiki kuwa vichekesho, bali ni vitendo vya kuhatarisha maisha ya watu kwa kuwalazimisha kwenda kujisaida baharini au vichakani.

Mambo haya ni matokeo ya miradi iliyofunguliwa kwa shangwe na vigelegele, lakini baadaye hutelekezwa kabla haijakamilika. Haitakiwi masuala kama haya kuachwa tu bila hatua muhimu kuchukuliwa.

Zinapokaribia sherehe za kitaifa baadhi ya viongozi huibuka na mapendekezo ya miradi ambayo haikufanyiwa utafiti. Matokeo yake gharama kubwa hutumika katika miradi isiyo kamilika.

Ni lazima tujenge utamaduni wa kutumia wataalamu tunapoanzisha miradi ya mandeleo na siyo kutumia wanasiasa ambao mara nyingi huamua kwa utashi wa kisiasa.

Ni muhimu pia, kuhakikisha kwamba hatuanzishi miradi mipya kabla ya ile tuliyokuwa nayo haijamalizika. Huu mtindo uliopo sasa wa kutumia lugha za kisiasa za kila wakati kutoa visingizio vya tupo njiani kutafuta fedha za kumalizia miradi hausaidii.

Ni aibu kuona jengo la darasa la shule, nyumba ya mwalimu au kituo cha afya kinakaa miaka 20 bila ujenzi wake kukamilika.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa. Baruapepe: [email protected]