Siyo siri mbuzi wa maziwa wanalipa

Tofauti na mbuzi wa kienyeji, mbuzi wa maziwa wanahitaji matunzo bora na uangalifu zaidi. Wasipotunzwa vizuri na kuangaliwa kwa ukaribu, hawatatoa maziwa ya kutosha na ni rahisi kupata madhara kiafya au kushambuliwa na magonjwa ya kitropiki

Muktasari:

  • Maziwa ya mbuzi yana virutubisho vingi na humeng’enywa haraka kuliko aina nyingine za maziwa

Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo mbuzi wa maziwa, wanapata umaarufu mkubwa kutokana na kuwa na faida nyingi

Faida hizo ni pamoja na kumwezesha binadamu kupata lishe itokanayo na maziwa na nyama na hata kuongeza kipato chake.

Katika sehemu ambazo ni vigumu kufuga ng’ombe wa maziwa,mbuzi wa maziwa ni muhimu katika kujibu changamoto za  lishe bora na kipato.

Hata hivyo, utaalamu na elimu bora ya utunzaji wa mbuzi wa maziwa haujaenea kiasi cha kutosha hapa Tanzania na ufugaji wa mbuzi hawa haujawa wenye tija kwa walio wengi.

Kwa sababu hiyo tangu mwaka 1983 watafiti kutoka idara ya sayansi ya wanyama, viumbe maji na malisho ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wakishirikiana na wenzao wa Koleji ya tiba za mifugo na afya ya binadamu na wengine kutoka Chuo Kikuu Cha Sayansi cha Norway (UMB) wamekuwa wakifanya utafiti na kutoa mafunzo ya ufugaji bora wa mbuzi wa maziwa katika maeneo mbalimbali nchini.

 Dk George Msalya ni mtafiti na mhadhiri  kutoka idara ya sayansi ya wanyama, anasema tangu wakati huo mbuzi wa maziwa hasa aina ya Norwegian Landrace wamesambazwa na kuenea maeneo mengi ya nchi kufuatia matokeo makubwa ya tafiti zao kwa msaada wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Norway (NORAD).

Mbuzi aina ya Norwegian

 Mbuzi aina ya Norwegian walijaribiwa SUA kwa miaka mitano na baadaye kupelekwa kwa  wafugaji wadogo maeneo ya milima ya Uluguru hasa tarafa ya Mgeta ambako  wamestawi vizuri.

Ingawa ni  kama mbuzi 10  hivi waliopelekwa kwa wafugaji, sensa inaonyesha  kuwa Tanzania ina zaidi ya mbuzi 400,000 wa aina hiyo katika maeneo mbalimbali.

Kwa mujibu wa Dk Msalya, mbuzi wamegawanyika katika makundi makubwa makuu matatu kutokana na umuhimu wao. Makundi hayo ni mbuzi wa nyama, mbuzi wa maziwa, na mbuzi wanaotoa manyoya (sufu).

Pia, anasema kwa sababu ya mazingira na hali ya dunia, mbuzi hugawanywa katika makundi makubwa mawili, yaani mbuzi wa nchi za baridi  na mbuzi wa nchi za joto.

 ‘’Kwa sasa makundi haya yote yanapatikana Tanzania lakini mbuzi wa kienyeji aina ya Small East African ndio wanapatikana kwa wingi sana (asilimia 98) na katika maeneo mengi,” anasema.

“Aina hii ya mbuzi inapendwa na wafugaji kwa sababu ya uwezo wa kustawi vizuri katika maeneo ya joto ya Afrika ya Mashariki, lakini hukua polepole, hawana nyama nyingi wala maziwa mengi.”

Mbuzi wa maziwa wanapatikana sehemu chache za nchi, hasa maeneo ya baridi na wanahitaji uangalizi wa karibu. Mbuzi hawa wana maziwa mengi na hukua haraka. Madume  yasiyotumika kwa uzalishaji huchinjwa na kuliwa.

 

 

Aidha, anasema hapa nchini kuna aina tano za mbuzi wa maziwa ambazo ni  Anglo-Nubian, Toggenburg, Alpine, Norwegian Landrace, na Saanen. Wengi katika hawa ni mbuzi chotara.

Faida na sifa za mbuzi wa maziwa

Kwanza; mbuzi wa maziwa humpatia mfugaji maziwa kwa ajili ya familia. Mahali ambapo ni vigumu kufuga ng’ombe wa maziwa ni rahisi kumfuga mbuzi.

 Maziwa ya mbuzi yana virutubisho vingi na humeng’enywa haraka kuliko aina nyingine za maziwa na hivyo ni maziwa bora sana kwa watoto wadogo, wazee na wagonjwa.

 Imethibitika kuwa watu wasioweza kutumia maziwa ya ng’ombe wanaweza kutumia maziwa ya mbuzi pasipo shida.

Mbuzi huleta kipato kwa familia. Kipato kutokana na mbuzi wa maziwa huweza kupatikana baada ya kuuza maziwa na mazao yake na  kuuza mbuzi hai wanaochaguliwa hasa madume yasiyo tumika kwa uzalishaji.

 Kwa mkoa kama  Morogoro, lita moja ya maziwa ya mbuzi huuzwa kati ya Sh 1,000 hadi 3,000 na mbuzi wa maziwa huuzwa kati ya Sh 100,000 hadi 150,000. Mkoani Arusha, mbuzi aina ya Toggernburg bei inafika Sh400,000.

Aidha, mbuzi wa maziwa humpatia mfugaji na jamii inayomzunguka mbolea kwa ajili ya kutumika mashambani na bustanini.

Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa mbolea inayotokana na mbuzi wa maziwa ina kiasi cha kutosha cha Naitrojeni, potashi na fosforasi (NPK), hivyo kustawisha vizuri mazao.

Pamoja na faida hizo, umuhimu na sifa za mbuzi wa maziwa zinatokana na mambo yafuatayo;

Ni rahisi kumfuga mbuzi kuliko ng’ombe kwa sababu huhitaji mtaji kidogo zaidi ukilinganisha na wanyama wakubwa kama ng’ombe.

Wanatumia gharama kidogo za chakula ukilinganisha na wanyama kama ng’ombe na ng’uruwe pamoja na sehemu ndogo au banda.

Hapa Tanzania na hasa maeneo ya Mgeta, mbuzi wa maziwa wameweza kutoa maziwa litambili  mpaka tano za maziwa kwa siku (wastani lita tatu) na hivyo huzidi mbuzi wa kienyeji wanaotoa lita 0.2 mpaka 0.5

Nchini Norway, mbuzi aina ya Norwegian hutoa lita nne mpaka sita  za maziwa kwa siku.

Mbuzi huzaa mapacha, mimba zao ni za muda mfupi (miezi mitano) na watoto hupandishwa kati ya umri wa miezi sita na nane; hivyo ni rahisi kupata idadi kubwa ya mbuzi ndani ya kipindi kifupi

Matunzo ya mbuzi wa maziwa

Tofauti na mbuzi wa kienyeji, mbuzi wa maziwa wanahitaji matunzo bora na uangalifu zaidi. Wasipotunzwa vizuri na kuangaliwa kwa ukaribu hawatatoa maziwa ya kutosha na ni rahisi kupata madhara kiafya au kushambuliwa na magonjwa ya kitropiki.

Utunzaji bora wa mbuzi wa maziwa humaanisha kuwa mnyama apewe chakula cha kutosha na kilicho bora, mbuzi atunzwe kwenye mazingira safi na salama na yanayoweza kumkinga na maradhi na wadudu wengine wa mwili kama vile kupe, viroboto, na minyoo.

Apewe huduma muhimu kama kupunguzwa kwato zilizozidi na kuogeshwa..

Ingawa mbuzi wa maziwa anaweza kulishwa na kupelekwa mbali na nyumbani, inasisitizwa kuwa mfugaji lazima atengeneze banda zuri la kuwahifadhi wanyama wake na ikiwezekana mbuzi wa maziwa aletewe chakula na kulishwa ndani ya banda. Anaweza  kutolewa tu kwa ajili ya mazoezi au wakati wa huduma nyingine zinazohitajika.

 Mbuzi wa maziwa huhitaji lishe bora au chakula chenye virutubisho vyote muhimu kama protini, madini,vitamini na maji.

 Kiasi cha kulisha hutegemea uzito wa mwili au kundi la mbuzi kama vile wazazi madume na majike, mbuzi wanaonyonyesha, mbuzi watoto, mbuzi wanaokuwa na wengineo.

Kwa kawaida inashauriwa mnyama apewe asilimia 2.5 hadi 4 ya uzito wake kama chakula kikavu ili kumpa lishe ya kutosha. Ifahamike kuwa majani ya asili na yasiyotunzwa vizuri hasa yale ya nchi kama Tanzania hayatoshelezi kama chakula bora cha mbuzi.

Ni muhimu kuangalia afya ya mbuzi wa maziwa na kuhakikisha afya zao kila siku. Mbuzi atakuwa na afya kama atakingwa dhidi ya magonjwa mbalimbali na kumuepusha na wadudu waletao magonjwa kama kupe, chawa na inzi.

Hii hufanyika kwa   kumuogesha na kwa kumtibu mara moja pale anapougua. Mbuzi afuatiliwe na kupandishwa mapema ili kumpa mfugaji faida.

Calvin Edward Gwabara ni mwandishi mwandamizi wa masuala ya kilimo na mifugo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo SUA [email protected], [email protected]