Taaluma inatakiwa sana nyumbani sasa hivi- Sehemu ya 2

Muktasari:

  • Lengo la makala haya ni kulenga kiini. Msingi wa tatizo uko katika uelewa na utamaduni. Jamii mbalimbali duniani zimefanya mambo yake kufuatana na mila, saikolojia na desturi zake asilia.
  • Ndiyo maana maendeleo hutofautiana kati ya nchi na nchi.
  • Ila hapo hapo maendeleo yana mstari mmoja kama ambavyo sote hula, huenda msalani , hulala, hufa, nk.

Juma lililopita mada hii iliangalia televisheni na vyombo vya habari. Ulikuwa mfano wa upungufu wa taaluma nyumbani. Tunaweza kuangalia mambo kadhaa – bila kuyamaliza.

Lengo la makala haya ni kulenga kiini. Msingi wa tatizo uko katika uelewa na utamaduni. Jamii mbalimbali duniani zimefanya mambo yake kufuatana na mila, saikolojia na desturi zake asilia.

Ndiyo maana maendeleo hutofautiana kati ya nchi na nchi.

Ila hapo hapo maendeleo yana mstari mmoja kama ambavyo sote hula, huenda msalani , hulala, hufa, nk.

Nilipoishi Brazil miongo kadhaa nyuma, niliendesha gari la Kijerumani. Ingawa gari liliitwa VW Golf (familia ya magari ya VolkWagen), lilitengenezewa Brazil, likabatizwa jina Gol. Viwanda vilimilikiwa na Wabrazili. Mafundi Wabrazili. Petroli ilitokana na miwa ya Brazili. Leseni ya utengenezaji wa gari hili la Gol (“patent”), ilimilikiwa na Wajerumani. Hapa, misingi ya kisheria na kibiashara.

Pande zote mbili zinafaidi, Wajerumani wanapata sifa ya magari yao ( faida za kiuchumi au “branding”) na Wabrazili hali kadhalika.

Ulikuwepo pia unafuu wa gharama. Bei ya gari nafuu kuliko ukiagizia Ujerumani.

Petroli ya miwa ( “Alcool” kwa Kireno) si aghali kama ya Urabuni au ardhini. Wabrazili hutumia taaluma zao kisayansi, kiteknolojia na kitamaduni.

Hakuna jambo lililonifurahisha Brazil kama wanavyojipenda.

Juu ya kujipenda wana utalaamu wa juu sana kwa mambo yao.

Tuchukue mfano chuo nilichojifunza nadharia na vitendo vya muziki. Waalimu wangu wote walishakwenda Marekani ( na kwingineko) kusoma. Mfano mwalimu wa Piano alisoma shule maarufu ya jazz – Berkley, Marekani. Alichapa Kiingereza ( na kikwao Kireno) na alizingatia misingi ya kimataifa. Mwalimu wa kuimba alijifunza Italia ambapo waimbaji wakubwa hunyanyuka. Alikuwa pamoja na marehemu mwimbaji maarufu wa Opera, Luciano Pavarotti. Vyombo vilivyotumiwa chuoni havikuwa vya kubabaisha. Wabrazil mbali ya kutengeneza zana zao za muziki huagiza pia nje. Zile zao safi kwa miziki yao mathalan, Samba, Capoeira, Samba Reggae, nk. Basi tuyaache.

Ninachokumbusha hapa nini?

Hatuwezi kusonga mbele tusipozingatia maarifa ya kidunia, kisayansi na kileo. Hapo hapo tusinyofoke nje ya tamaduni na mambo yetu. Kuna msomaji aliyeniandikia kuwa nilipomhoji Mtaalamu Sam Kitojo akashauri tuwekeze fedha zaidi katika zana bora za TV , si vizuri.

Msomaji : “ Siye Watanzania...vitu vyetu ni vya bei poa, si unaona Wachina walivyotuweza, bei rahisi, mambo yetu ni ya kwetu tu...” Nilipenda aliposema mambo yetu ni “ya kwetu tu”. Ndivyo walivyo Wajapani na Wabrazili . Wanafanya kila kitu kivyao. Lugha na tamaduni zao. Tena ninamkubalia kuhusu “urahisi” na kutafuta vitu visivyo vya gharama. Ndiyo sababu iliyonipeleka Marekani ya Kusini badala ya vyuo vya gharama Ulaya.

Walakin, sharti kuzingatia taaluma.

Wenzetu wanaheshimu tamaduni zao (Samba, Toyota,nk) lakini wako katika mitandao ya kidunia na kiteknolojia. Haina maana ukizingatia mila zako basi unabangaiza, unababaisha na mambo kiholela, bila elimu. Unatoa sinema au kazi duni. Hapo ni kutukuza umaskini, njaa na kutoendelea. Wananchi wanahitaji maendeleo na maisha rahisi. Lakini si kugeuzwa vipofu.