MAONI YA MHARIRI: Taasisi za Serikali zisimsubiri Rais kulipa madeni

Rais John Magufuli

Muktasari:

Rais Magufuli alisema atakachofanya ni kukata sehemu ya fedha za matumizi ya kawaida (OC) ya taasisi hizo hasa wizara, ili kulipa deni ambalo uongozi wa Uhuru unasema ni zaidi ya Sh1.6 bilioni.

Septemba 19, ilikuwa siku ya furaha ya aina yake kwa uongozi wa kampuni ya Uhuru Publications Limited inayochapisha magazeti ya Uhuru na Mzalendo, baada ya Rais John Magufuli kuitembelea na kuahidi kushughulikia madeni wanayozidai taasisi mbalimbali za Serikali.

Rais Magufuli alisema atakachofanya ni kukata sehemu ya fedha za matumizi ya kawaida (OC) ya taasisi hizo hasa wizara, ili kulipa deni ambalo uongozi wa Uhuru unasema ni zaidi ya Sh1.6 bilioni.

Alichokifanya Rais kwa kampuni hii, kimetugusa hasa kwa kuwa taasisi hizohizo zimekuwa pia ni wadaiwa sugu wa baadhi ya vyombo vya umma ambavyo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi.

Vyombo hivyo kama mifuko ya hifadhi ya jamii, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Nyumba (NHC) na vinginevyo, mara kwa mara vimekuwa vikilalamika kuwa taasisi za Serikali hususan wizara, ama hazitaki kulipa madeni yao kwa makusudi au hazioni umuhimu wa kufanya hivyo.

Kwa mfano, hadi Juni mwaka huu, taasisi mbalimbali za Serikali zilikuwa zikidaiwa kiasi cha Sh6 trilioni na mifuko ya jamii.

Pamoja na Serikali kuonyesha nia ya kulipa madeni hayo, utekelezaji umekuwa wa kusuasua, hali inayosababisha pengine tuamini kuwa haina nia ya dhati.

Kwa mfano, Juni mwaka huu akiwasilisha taarifa ya kamati ya Bajeti ya Bunge, mwenyekiti wa kamati hiyo, Josephat Kandege alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/16, Serikali iliahidi kutoa kiasi cha Sh150 bilioni pamoja na hati fungani za Sh2.6 trilioni ili kulipa deni la PSPF, lakini hadi muda huo ni Sh83 bilioni pekee zilizotolewa. Hakukuwa na hati fungani yoyote iliyotolewa.

Huu ni mfuko mmoja wa PSPF, hali si shwari pia katika mifuko mingine, ndiyo maana tunamsihi Rais kuwa msisitizo na njia anayotumia kulipa madeni ya gazeti la Uhuru, avihamishe kwenye mifuko hii ambayo wanachama wake wengi hawana uhakika kama bado ina nguvu ya kifedha.

Ukiondoa mifuko ya hifadhi ya jamii, madeni ya Serikali pia yamekuwa yakidhoofisha maendeleo ya mashirika ya umma kama Tanesco.

Kimsingi, shirika hili ni muhimu hasa wakati huu wa utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, azma ambayo mwishowe itaipeleka nchi katika kilele cha uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Rais Magufuli na Serikali yake hana budi kuyavalia njuga madeni haya, kwa kuhakikisha yanalipwa kwa njia yoyote ile endelevu pasipo kuathiri utekelezaji wa majukumu mengine ya Serikali

Njia anazoweza kutumia ni pamoja na aliyoitumia kwa kampuni ya Uhuru kwa kuamua kukata OC za wizara moja kwa moja au kutoa agizo la madeni hayo kulipwa kwa kipindi maalumu kama alivyofanya kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano alipoiagiza kulipa ndani ya siku saba deni la Sh 2bilioni inalodaiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Tunaamini kukiwa na utashi wa ofisi ya Rais, madeni haya yanaweza kulipwa na hivyo kuongeza ari na hamasa ya uwajibikaji kwa vyombo husika ili hatimaye vichangie vilivyo katika maendeleo ya Taifa letu.